HEKALU LA BWANA LIKO TAYARI

Siku za Mwisho No Comments

HEKALU LA BWANA LIKO TAYARI

Hekalu la kwanza kama tunavyofahamu lilitengenezwa na Mfalme Sulemani, Ni hekalu lililochukua kipindi cha miaka 7 mpaka kukamilika, Tunasoma..

1 Wafalme 6:38 ”Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga”.

Kama biblia inavyosema Kanisa la Kristo ni Hekalu la Mungu,(1Wakorintho 3:16). Na kama vile Sulemani alivyokuwa analijenga Hekalu lile, vivyo vivyo YESU KRISTO naye analijenga HEKALU lake, ambalo ndilo kanisa takatifu (bibi-arusi safi).

Na kama vile lile la Sulemani lilikamilika ndani ya miaka 7, kadhalika na hili la Kristo nalo linakamilika katika nyakati 7 za kanisa (Ufunuo 2&3).

Na kitu cha kipekee tunachoweza kujifunza katika ujenzi wa lile hekalu la Sulemani, ni jinsi uundwaji wake ulivyokuwa. Maandiko yanatuambia katika kipindi chote cha ujenzi, hakukusikika mlio wa nyundo, wala shoka au mlio wa nyenzo yoyote ya ujenzi. Tunasoma;

1Wafalme 6: 7 “Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, IKAJENGWA KWA MAWE YALIOKWISHA KUCHONGWA CHIMBONI; WALA NYUNDO, WALA SHOKA, WALA CHOMBO CHA CHUMA CHOCHOTE, SAUTI YAKE HAIKUSIKIWA ILIPOKUWA IKIJENGWA NYUMBA”.

Unaweza ukajenga picha ni JENGO la aina gani hilo linajengwa pasipo kusikika kilele ya aina yoyote ile?, ni wazi kuwa litakuwa limejengwa kwa utashi wa hali ya juu sana ambao kwa namna ya kawaida haujazoleka katika ujenzi tulionao..

Ghafla tu wananchi waliokuwa wanakaa Yerusalemu wakati ule walishangaa JENGO hili hapa limeshakamilika, wakati wanadhani kwamba jengo ndio linaanza kujengwa, kumbe hawajui kuwa ndio linakaribia kumalizika..kwasababu wakati wa ujenzi wake wenyewe walitegemea wasikie milio ya nyundo, na mashine, na mashoka, na misumeno, na sauti za kelele nyingi za wafanyakazi, ili wajue kuwa ujenzi ndio unaanza lakini mambo hayakuwa hivyo. Kwa nje! Ilionekana kama ni kazi iliyolala tu,

Lakini biblia imetupa siri ni kwanini haikusikika kelele wakati wa ujenzi wake, tunasoma hapo juu ni kwasababu “mawe ya ujenzi yalikuwa yanachongewa mbali sana huko machimboni na kukamilika huko huko kisha kuletwa eneo la ujenzi, tayari kwa kuchomekwa tu! kimya kimya.”..Muda wa mamiezi mengi ulipotea huko machimboni kuchonga miamba, lakini baada ya kukamilika kipindi cha ujenzi kilichukua muda mfupi sana.

Nini tunajifunza hapo, hata sasa Hekalu la Bwana yaani kanisa lake takatifu lipo katika hatua ya mwisho ya ujenzi.

Na kama vile watumishi wa Sulemani walivyokuwa machimboni duniani kote kutafuta na kushughulika na uchongaji wa yale mawe vivyo hivyo na Bwana Yesu Kristo leo amewatuma watumishi wake waaminifu duniani kote kuwatengeneza watu wake wateule kwa ujenzi wa mwisho kanisa lake tukufu litakalokwenda kukamilika hivi kwaribuni kwa tukio la unyakuo…[hao ndio yale mawe yachongwayo chimboni]

Na kama vile mwishoni mwa mwaka wa 7 jengo la Sulemani lilikamilika na utukufu wa Mungu kushuka mwingi juu yake siku ile. kadhalika na hili kanisa la mwisho la 7 la Laodikia tunaloishi mimi na wewe, ndio tutakalolikamilisha HEKALU la Mungu kisha kumalizia na unyakuo siku ile, jiwe la mwisho litakapoletwa eneo la ujenzi (yaani kondoo wa mwisho atakapoingia katika neema ya msalaba).

Hii inatuonyesha wazi kuwa hatua za UNYAKUO hazitajulikana na watu wengi [yatakuwa ni mambo ya siri]…Wakati watu wanadhani kwamba kanisa la Mungu bado sana linyakuliwe, hawajui kuwa ndio lipo katika hatua za mwisho mwisho, wakati wanasubiri waone na wasikie milio ya matarumbeta na maonyesho, na kushuka moto, hawahafamu kuwa mawe yalishakamilika kuchongwa tangu mwambani.

Ndugu Leo hii Mungu anawaanda watu wake Ki-binafsi, (yaani mmoja mmoja)..na sio kimkusanyiko au kidhehebu, Mungu hawaandai watu kama shirika au jumuiya au kusanyiko hapana, Mungu anamwandaa mtu wake ki-binafsi.

Unaweza ukadhani sasa hakuna watu wa Mungu duniani, kwasababu haulioni kanisa lililosimama lenyewe kikamilifu mbele za Mungu, lakini jua tu kanisa halisi la rohoni la Kristo linazidi kuimarika siku baada ya siku. Na moja ya hizi siku litakamilika, hapo ndipo watapokusanywa wote kwa pamoja kama mtu mmoja na kukutanika mawinguni kwenda mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo.

JE! NA WEWE NI JIWE LINALOCHONGWA CHIMBONI SASA??…Au unasubiria wakati Fulani ufike ukagongelewe kwenye jengo?…Jenga maisha yako kwa Kristo sasa, tubu dhambi zako, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na uwe ni kwa jina la YESU KRISTO ndipo upokee kipawa cha ROHO MTAKATIFU.

MAANA SIKU ILE KANISA LITAKAPONYANYULIWA JUU, HAKUTASIKIKA KELELE WALA TAHARUKI YOYOTE DUNIANI..ITAKUWA NI TENDO LA GHAFLA TU!..ee!! fulani hayupo!!, mbona sikuwahi kumwona kama alikuwa ni mtu wa dini sana? Ee!! Mbona tulitazamia tuone kwanza jambo fulani likitokea duniani? Hawajui kuwa mawe yalikuwa yanachongewa machimboni.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *