ITAFAKARI HEKIMA YA MUNGU KATIKA UUMBAJI WAKE

Biblia kwa kina No Comments

ITAFAKARI HEKIMA YA MUNGU KATIKA UUMBAJI WAKE.

Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Libarikiwe siku zote. Karibu tuongeze maarifa ya kumjua Mungu.

Na leo tutajifunza umuhimu wa kutafakari hekima ya Mungu ipatikanayo katika uumbaji wake.

Hekima ni nini?

Hekima ni Neno pana ambalo linajumuisha elimu au ujuzi/akili au uwezo wa kupambanua, kuhukumu, na kufanya maamuzi sahihi.

Sasa ni vizuri kufahamu kuwa hekima ya Mungu ni Mungu mwenyewe!! maana yake unapochunguza au kutafakari hekima ya Mungu ipatikanayo katika uumbaji wake unamuona Mungu mwenyewe.

Ni sawa na wewe ukutane na mtoto wa mtu fulani ambaye unamfahamu, kwa vile unavyofahamu akili na tabia za yule mtu, hutopata shida kumuelewa huyo mtoto..utahisi tu kuwa huyu ni mtoto wa mtu fulani kabla hata yeye mwenyewe hajakuthibitishia. Ni kwanini? Ni kwasababu yeye na baba yake ni kitu kimoja.

Ni vivyo hivyo tunapotafakari viumbe vya Mungu, ukitaka kumuelewa Mungu kwa upana jifunze kutafakari sana uumbaji wake, ukitaka kuelewa hekima ya Mungu..tumia sana muda wako mwingi kutafakari uumbaji wake huko ndiko utajua Mungu yukoje, tabia zake, uweza wake, n.k bila kusahau pia kuwa hekima ya Mungu ni Yesu Kristo mwenyewe (1Wakorintho2:7), unaweza ukamfahamu Mungu kupitia uumbaji wake, lakini ukitaka kumfahamu katika utimilifu wote..mfafahamu sana Yesu Kristo yeye ndiye hekima ya Mungu ambayo ilikuwa imefichwa.

Lakini siku ya leo tutajifunza umuhimu wa kutafuta hekima ya Mungu kwa kutafakari uumbaji wake.

Je! tunaweza kufanya utafiti na kufahamu akili za Mungu kama wanasayansi wanavyotafiti akili ya mwanadamu?

Jibu ni ndio, tunaweza takafanya utafiti na kugundua akili za Mungu kupitia uumbaji wake isipokuwa hatuwezi kufikia mwisho wa kuchunguza akili za Mungu na kutoa hitimisho kuwa akili zake iko hivi au vile, tutaishia tu kufahamu kwa sehemu ndogo, kwani Mungu wetu ni MKUBWA sana akili zake hazichunguziki. Yeye ndiye aliyetuumba, hivyo hatuwezi kujua kila kitu kuhusu yeye.

Isaya 40:25 Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye?…

28 Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.

Ila ni vizuri kufahamu kuwa andiko hili halijatuwekea mipaka ya kuchunguza akili za Mungu, hapana! Ingekuwa hivyo basi Bwana Yesu asingesema tutafakari ndege wa angani, kwasababu kitendo cha kutafakari viumbe vya Mungu maana yake kuna kitu cha kiMungu tutagundua kwao, na kitu hicho si kingine zaidi ya akili na tabia zao, na kufanya hivyo ni sawa na kuchunguza akili za Mungu. Maana akili walizonazo viumbe wote ni akili za Mungu, ndiye aliyewapa.

Ayubu 39:26 Je! Mwewe huruka juu kwa akili zako, na kunyosha mabawa yake kwenda kusini.

Hivyo ni vizuri kuchunguza akili za Mungu kila siku kupitia uumbaji wake, ila pia ni vema kufahamu kuwa akili za Mungu hazichunguziki.. Kwahiyo wakati tunazidi kuchunguza akili zake tusitafute kufikia mwisho wa kufahamu maana hutuwezi kufikia..hata tukichunguza maisha yetu yote bado hutuwezi kujua akili za Mungu kwa utimilifu maana akili zake hazichunguziki, Mungu wetu ni Mkuu sana, akili zake hazina mpaka..unaweza ukasema yuko hivi kumbe siyo, unaweza ukasema atanijibu kwa njia hii kumbe siyo, akili zake hazina mpaka.

Zaburi 147: 5 Bwana wetu ni Mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka.

Sasa kama akili za Mungu hazichunguziki..kwanini tuchunguze bure?

Ni kwasababu kwa njia hiyo tutamheshimu sana Mungu na kumwogopa. na kufanya hivyo tutazidi kumwabudu yeye peke yake ikiwa ndiyo kusudi la sisi kuwepo hapa duniani.

Kadri unavyozidi kumuona Mungu kupitia uumbaji wake ndivyo utakavyozidi kumpenda na kuwa naye karibu, Na Mungu akishaona hilo, naye atakupenda sana na kukuonyesha mambo ya ajabu usiyoyajua.

Hebu leo anza kumwona Mungu kupitia chochote kinachokuzunguka, anza  na mwili wako tafakari jinsi ulivyoumbwa, angalia na wanyama, ndege, wadudu na viumbe vyote.. chunguza akili zao huku ukimtafakari Mungu aliyewapa hiyo akili, jiulize maswali ndani ya fikira zako kuhusu akili zao, jiulize kwanini awe hivi au vile? Nani aliyewapa hiyo akili?hakuna kiumbe ambayo hajapewa akili isipokuwa akili zao hazifanani, hata sisimizi anayo akili.

Na ukijumlisha akili zote walizonazo viumbe vyote mpaka ile waliyonayo wanasayansi ni sehemu tu ndogo ya akili ya Mungu..bado hujamfahamu.

Je! unapotazama jinsi ulivyoumbwa, je! unagundua nini? je! unamwona Mungu? umewahi kujiuliza kwanini Mungu amekuumbia hizo kucha na hizo nywele ulizobadiilisha rangi, au kope, n.k hebu leo tambua akili za Mungu kupitia hata mwili wako, anza kujiuliza sababu ya Mungu kukumbia hizo viungo vya mwili wako? Na kadri utakavyozidi kuchunguza akili za Mungu ndivyo utazidi kumtukuza na kumshukuru, na vilevile kuogopa kumfanyia dhambi ukijua yeye ni Mkuu, anaweza akakuadhibu vibaya na usipate msaada.

Zaburi 139:14 Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana.

Warumi 11:33 Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!

34 Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mashauri wake?

35 Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena?

36 Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.

Je umempokea Yesu? Kama bado fahamu kuwa huwezi kukwepa hukumu ya Mungu! Hata Kama wewe unajiona una akili nyingi.. fahamu kuwa hiyo akili ni sehemu ndogo ya akili za Mungu.. hivyo huwezi kumkimbia aletapo hukumu duniani!

Saa ya wokovu ni sasa.. dhamiria kumpa Yesu maisha yako kweli kweli ili uokoke na hukumu ya ziwa la moto.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *