Tujifunze kanuni za Mungu

Biblia kwa kina, Uncategorized No Comments

Tujifunze kanuni za Mungu

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Ni muhimu kujua kanuni kadhaa za ndani ya biblia ambazo Mungu anataka tuzifuate ili tufanikiwe (kimwili na kiroho),

Zipo kanuni nyingi katika biblia ambazo Mungu anataka tuzifuate, lakini leo tuangalie baadhi ya kanuni chache.

1 Kanuni ya kubarikiwa/kufanikiwa

Marko 4:24 “Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho NDICHO MTAKACHOPIMIWA, na TENA MTAZIDISHIWA”.

Hapo nataka tuyatazame hayo maneno miwili. 1)Kipimo mpimacho ndicho mtakachopimiwa. na 2) tena mtazidishiwa

Maana yake ni kwamba Kama utampimia mwingine kwa kumpa “sh.elfu moja”..basi Bwana atahakikisha anakurudishia kwa njia nyingine hiyo “elfu moja” uliyoitoa. (Huenda ikawa siku hiyo hiyo, au wakati mwingine ambao haupo mbali sana).

Lakini haiishii hapo tu kukurudishia hiyo elfu moja..bali anaendelea kwa kusema “na tena mtazidishiwa”.

Ikiwa na maana kuwa Bwana akishakurudishia kile ulichokitoa, sasa kinachofuata ni yeye kukulipa wema ulioufanya kwa “kwa kukuzidishia”.

Maana yake atakupa na kingine kingi zaidi ya hiyo elfu moja uliyoitoa,

Sasa ili tuelewe vizuri ni kiasi gani tutazidishiwa, hebu tuyatazame tena maneno ya Bwana Yesu katika Luka 6:38.

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.

Hiyo ndiyo kanuni ya kiMungu unapomuomba akubariki, hivyo ukitumia hii kanuni bila shaka utafanikiwa sana, lakini kama unataka tu kupokea kwa Mungu na wewe hutoi kwa moyo wako kumtolea Mungu.. haijalishi utafunga na kuomba ili ufanikiwe, Mungu anaangalia hiyo kanuni yake.

2 Kanuni ya kusemehewa deni/makosa yetu

Marko 11:25 Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [

[26]Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

Unataka Mungu akusamehe deni zako.. kanuni ni hiyo kusamehe wengine,

Mathayo 18:23 Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.

[24]Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.

[25]Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.

[26]Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

[27]Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.

[28]Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, Nilipe uwiwacho.

[29]Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

[30]Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.

[31]Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.

[32]Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi;

[33]nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?

[34]Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.

[35]Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.

3 Kanuni ya kuinuliwa kihuduma/kimaisha

Tukitaka sifa zetu zienee katika nyanja yoyote ile maishani iwe ni katika Utumishi, shughuli zetu, au chochote kile tukifanyacho, tuhakikishe tunatoa kilicho bora kwanza, kisha tukae kimya, tusijikweze, tukatae kutukuzwa tukuzwa na watu, Kwa kufanya hivyo ndio tutasifiwa, yule yule aliyekipokea ndiye atakayekisambaza kwa nguvu kuliko hata wewe unavyodhani..Hiyo ndio ilikuwa kanuni ya Bwana..alisema “ajikwezaye atashushwa na ajishushaye atakwezwa”…Kwahiyo yeye mwenyewe alijishusha ili akwezwe.

Mathayo 23:12 Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.

4 Kanuni ya kuongezewa Neema

Yakobo 4:6 Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.

Unataka neema ya Mungu izidi juu yako, kanuni ni kuwa mnyenyekevu, lakini ukiwa na kiburi neema inapunguzwa au kuondolewa kabisa..kwasababu kiburi na neema havipatani, bali neema na unyenyekevu huwenda pamoja.

1 Petro 5:5 Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.

5 Kanuni ya kufanikiwa rohoni (kuwa tajiri rohoni)

Mathayo 5:3 Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Ukitaka kufanikiwa rohoni (kumjua Mungu katika utimilifu wote) kanuni ni kuwa maskini wa rohoni, lakini ukijiona tayari unajua, ukijiona wewe umekomaa kiroho na hivyo ukajikinai kusoma biblia kila siku, kuomba kila siku..ujue bado hujui kitu na unahitaji msaada wa kiMungu.

Hizo ndizo baadhi ya kanuni za Mungu ambazo anataka tuzifuate Sisi kama watoto wake.Washirikishekanuni za Mungu ambazo anataka tuzifuate Sisi kama watoto wake.

Je umeokoka? Unahabari kuwa tunaishi ukingoni mwa nyakati? Kama bado hujaokoka unasubiri nini? Saa ya wokovu ni sasa, tubu dhambi zako mpokee Bwana Yesu kabla mlango wa neema haujafungwa juu yako.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *