JITENGE NA MKUTANO WA WATU WAOVU

Biblia kwa kina, Dhambi No Comments

JITENGE NA MKUTANO WA WATU WAOVU.

Jina la Mkuu wa Uzima na Mkuu wa wafalme wa dunia, YESU KRISTO libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu Mungu wetu.

Biblia inatufundisha kuwapenda watu wote, lakini si kuambatana na watu wote.

2Wakorintho  6:14  “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani KATI YA HAKI NA UASI? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”

Umeona?..maana yake ni kwamba kama unaambatana na mtu ambaye si wa aina yako, basi unajiharibu mwenyewe!, Baada tu ya kumkiri Yesu, jambo lingine la muhimu linalopasa kufuata ni KUCHAGUA AINA YA WATU, utakaoanza kuwa nao karibu, kuanzia huo wakati na kuendelea.

Kama we ni msomaji mzuri wa biblia utakuwa unaifahamu ile habari ya wana wa Israeli katika lile jambo la Kora na Dathani.

Wote tunafahamu kilichowatokea wale watu walipojaribu kwenda kinyume na Musa na kumuasi Mungu, sasa ukisoma ile habari kwa umakini utagundua kuwa adhabu ya Mungu haikuwalenga tu wale watu 250 waliokuwa wameungana na Kora kufanya ule uasi,bali ni watu wote isipokuwa tu Musa na Haruni ndio walikuwa wanapona, ingekuwa sio maombi ya Musa, habari ya wana wa Israeli ingeishia pale..Hebu tusome kwa umakini,

Hesabu 16:19 Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote.

[20]Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

[21]JITENGENI NINYI MKAONDOKE KATI YA MKUTANO HUU, ili nipate kuwaangamiza mara moja.

[22]Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote?

[23]BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

[24]NENA NA MKUTANO, NA KUWAAMBIA, ONDOKENI NINYI HAPO KARIBU NA MASKANI YA KORA, NA DATHANI, NA ABIRAMU.

[25]Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye.

[26]Akasema na mkutano, na kuwaambia, NAWASIHI, ONDOKENI PENYE HEMA ZA HAWA WATU WAOVU, WALA MSIGUSE KITU CHAO CHO CHOTE, MSIANGAMIZWE KATIKA DHAMBI ZAO ZOTE.

[27]Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo.

Umeona hapo, kitendo tu cha kushikamana na huo mkutano mwovu, mkutano wote unaharibiwa, ndio maana sehemu nyingine biblia inasema “Chachu kidogo huchachua donge zima” (Wagalatia 5:9), Soma pia Warumi 11:16. Hivyo inatusihi tujitenge/tuondoe ile Chachu ili tuwe safi.

1 Wakorintho 5:6 Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima?

[7]Basi, JISAFISHENI, MKATOE ILE CHACHU YA KALE, MPATE KUWA DONGE JIPYA, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;

Kama vile Musa alivyowasihi ule mkutano usiokuwa na hatia, watoke/wajitenge na hema za wale watu waovu ili wasiangamizwe katika dhambi zao, vivyo hivyo Kristo naye anatusihii tutoke/tujitenge katika kampani za watu wa kiulimwengu, na mifumo ya dini za uongo na kamba za madhehebu ili tusije tukashiriki adhabu ya dhambi zao.

Ufunuo wa Yohana 18:4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.

[5]Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.

Soma pia..

2 Wakorintho 6:17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. 18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi.

Ndugu, ikiwa unataka kuwa salama, ni heri leo ukatii sauti ya Kristo anapokuambia utoke katika huo mkutano wa watu waovu, utoke katika kampani za walevi, wasengenyaji, watukanaji, wahuni, waasherati, waabudu sanamu kwa maana hakika watu wa jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu..bali wataishia tu kushuka shimoni (kuzimu) wasipotubu kama tu ule mkutano wa akina Kora na wenzake mwisho wao walishuka kuzimu wakiwa hai na mali zao, na kiburi chao.

Ujumbe wa saa hii ni kutoka katika mapokeo ya ki-Madhehebu? Na kurudi katika Neno kama lilivyohubiriwa na Mababa (Mitume watakatifu). Toka katika mapokeo yanayokwambia ubatizo wa maji mengi au maji machache haujalishi! Hiyo ni roho ya Mpinga-kristo. Toka katika dhehebu linalokuambia tunaweza kuwaombea wafu watoka katika mateso huko waliko, hilo ni sinagogi la shetani!! Toka katika dhehebu linalokuambia Bikira Mariamu anaweza kutupatinisha sisi na Mungu. Hiyo ni injili iliyotengenezwa kuzimu kabisa ndugu yangu…Mpatanishi wa sisi na Mungu ni mmoja tu!!! YESU KRISTO, Usidanganyike na mafundisho ya mashetani!!.. Toka katika madhehebu yanayokuambia Mwanamke anaruhusiwa kuvaa suruali!! Na nguo fupi.. HAYO NI MAKUTANO YA WATU WAOVU,  Kwa nje ni mazuri lakini ndani Kristo ameyakataa!..hawakwambii ukweli kwasababu anayeabudiwa humo ni shetani! Na shetani analohitaji ni kuipeleka nafsi yako kuzimu! Hilo tu!! Toka katika madhehebu yanayokuambia bado miaka mingi Kristo aje!, ni roho zinazoshawishi kukulewesha ili siku ile ikujie kama mwivi.

Leo umeisikia sauti hii, Je utaendelea kubaki hapo ulipo? 

Unapousikia ujumbe huu, ufanye hima utoke, na sio utoke kwa miguu au ubadilishe kanisa, hapana bali utoke kwa kuutafuta ukweli na kuoana na neno la Mungu, ujazwe Roho wa Mungu. na Roho ndiye atakayekuongoza katika kuijua kweli yote, sio dhehebu wala shirika lolote la dini wala kanisa, tafuta uhusiano wako binafsi na Yesu Kristo na ndipo utakapokuwa bikira safi.

Kama hujamkabidhi Yesu Kristo maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo, kabla mlango wa Neema hujafungwa, kabla unyakuo haujapita na ukaachwa, kabla ya mpinga-kristo kunyanyuka ulimwenguni na kulazimisha watu kuipokea ile chapa ya mnyama. Unachotakiwa kufanya hapo ulipo ni kutenga dakika chache angalau sio chini ya dakika 15, funga mlango wako kaa peke yako zungumza na Mungu wako, mweleze maisha yako ya nyuma, tubu kwa ajili ya hayo, usifiche chochote, mwambie akusamehe na pia mwahidi hutafanya hayo tena, na baada ya kutubu usifanye tena hayo uliyokuwa unayafanya, Bwana atakusamehe yeye ni mwenye rehema na atakukubali tena, haijalishi umemkosa kiasi gani!. Kisha usikawie nenda katafute ubatizo sahihi kulingana na imani ya mababa(Mitume)..huo utaupata katika kitabu cha Matendo 2:38, Matendo 8:16, Matendo 10:48 na Matendo 19:5, ubatizo huo ni wa maji mengi na KWA JINA LA YESU KRISTO..Na baada ya kubatizwa Bwana atakupa kipawa chake cha Roho Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na hapo utakuwa umezaliwa mara. Kumbuka hakuna mtu atakayeurithi ufalme wa Mbinguni kama hajazaliwa mara ya pili. (Yohana 3:3)

Maran atha.

  1. Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *