ITHAMINI NEEMA YA WOKOVU

Biblia kwa kina No Comments

ITHAMINI NEEMA YA WOKOVU

Biblia inatuambia..

…utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa KUOGOPA na KUTETEMEKA”.(Wafilisti 2:12)

Unajua kwanini tunapaswa kutimiza wokovu wetu kwa kuogopa na kutetemeka?

Ni kwasababu, wokovu ni jambo lisilo la kawaida, ni jambo la kushangaza sana. Ukitafakari kwa kina namna ilivyopatikana na jinsi tulivyoipokea..tunabaki tu kushukuru..basi!.

Hii neema ya wokovu ambao unapatikana sasa bure, tusidhani yule aliyetuletea hakuingia gharama yoyote kuupata,…haikuwa ni jambo la kutamka tu na kusema niaminini mimi mtaokoka!.

Kristo ilimlazimu aingie gharama ili kukamilisha kitu kinachoitwa WOKOVU. Kwani wokovu ili ipatikane ina kanuni yake, ilimpasa mtu apatikane ambaye atatolewa kama sadaka, na hiyo sadaka ni sadaka isiyo na hatia yoyote…ndipo hapo sasa Kristo alikubali kuacha enzi na mamlaka yote mbinguni..ashukuke hapa duniani, awe hana kitu, aishi kama mwanadamu mwingine yoyote yule, apitie maisha kama ya wanadamu, aumwe wakati mwingine, audhiwe, apitie umaskini, kisha na yeye pia ajaribiwe na shetani, aonekane kama atashinda au la,

Lakini kama tunavyosoma aliyashinda yote kwa muda wa miaka 33 bila kutenda dhambi yoyote ijapokuwa alipitia majaribu yote ya kibinadamu.

Na baada ya hapo sasa, ilimgharimu atoe uhai wake ili aweze sasa kukikamilisha hicho kitu kinachoitwa WOKOVU KWA MWANADAMU…Ndipo hapo Kristo akalazimika aende msalabani akapigwe afe, damu imwagike ili kusudi mimi na wewe tupokee huu wokovu kwa gharama alizoingia.

Wengi wetu tunadhani mateso aliyoyapitia yalikuwa ni ya kawaida tu, biblia inatuambia Bwana aliharibiwa uso wake, na mwili wake, Zaidi ya mwanadamu mwingine aliyewahi kuishi hapa duniani..

Soma..

Isaya 52:13 “Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana.

14 Kama vile wengi walivyokustaajabia, (USO WAKE ULIKUWA UMEHARIBIWA SANA ZAIDI YA MTU YE YOTE, NA UMBO LAKE ZAIDI YA WANADAMU),

15 ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu”.

Jaribu kuchua muda utafakari!, chukua muda utafakari hata dakika 15 au 20, fikiria huo uso uliwezekanikaje kuharibiwa Zaidi ya mtu yoyote hapa duniani, na mwili wake vivyo hivyo, ndipo utakapofahamu kuwa mapigo aliyopigwa Bwana hayakuwa ya mwanadamu wa kawaida, alikuwa kama nyama buchani, kile unachokifahamu kwenye filamu ni mfano mdogo wa jinsi Bwana alivyokuwa anaonekana, na hiyo yote ilimpasa apitie vinginevyo mimi na wewe tusingeupata wokovu..

biblia inasema..

Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, NA KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA”.(Isaya 53:5)

Uso wake na mwili wake usingeharibiwa kwa mapigo mabaya kama yale ambayo mengine hata hayajaandikwa kwenye biblia, mimi na wewe leo hii tusingeufikia uponyaji wa roho zetu.

Ndio maana biblia inatuambia katika..

Waebrania 2:3 “sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia;

Hiyo ndiyo sababu tunapaswa kutimiza wokovu kwa kuogopa na kutetemeka, kwasababu ulipatikana kwa gharama kubwa sana…na tulipokea tu bure pasipo hata kustahili.

Watu wengi leo wanaorudi nyuma na kuacha wokovu ni kwasababu hawataki kutafakari maana ya wokovu kwa kina na kujua gharama ambayo Bwana ameingia ili sisi tupone.

Ndugu yangu, ithamini wokovu kuliko kitu chochote kile, na Fahamu kuwa huu wokovu haupo kwa watu wote, ni kundi dogo tu ndio wamekusudiwa. Hebu tafakari mfano huu..

Tuchukulie we ni mwanafunzi..umeshindwa kuendelea kusoma kutokana na hali ya kimaisha kuwa ngumu, lakini kama bahati, akatokea mtu mfulani mkuu akatangaza nafasi za kuwafadhili wanafunzi watano bure, ambao watasomeshwa katika shule kubwa kubwa, yenye madhari mazuri..huko watakula vizuri bure, watapatiwa kila kitu bure..na baada ya kuhitimu watatafutiwa kazi. Sasa wakajitokeza wanafunzi Elfu moja ambao wanaomba hiyo nafasi na wewe ukawa miongoni mwao, lakini cha ajabu wewe pasipo kufanya hata chachote, pasipo hata kwenda kwenye vipimo (interview), ukajikuta umeitwa miongoni mwa wale watano. Bila shaka utashukuru vya kutosha, utaona ni muujiza! na hakika hautapuuzia maelekezo yoyote ambayo utapewa, tena utakuwa makini sana huko shuleni, kwa ufupi utaithamini sana hiyo nafasi kuliko chochote kwasababu unajua jinsi ulivyoipata ni muujiza tu…na kila ukiangalia idadi ya wanaoitafuta nafasi kama hiyo..utaogopa na kuitetemekea kwani kuna wengine tu ambao wamekuzidi kwa kila kitu lakini hawajapata.

Ndivyo ilivyo kwa swala la wokovu, biblia inasema ule mlango ni mwembamba sana, ni wachache tu ndio wanaoingia.

Mathayo 7:14 Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.

Kumbuka hapa tunazungumzia wokovu wa kweli, na wala sio ule wa madhehebu na theolojia.

Wokovu tunaouzungumzia hapa ni ule wa kuacha vyote na kuwa mwanafunzi wa Yesu kama yeye mwenyewe alivyosema..

Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” (Luka 14:33)

Kuacha vyote ambayo Kristo anamaanisha hapo, ni kuondoa kila kitu kwenye moyo na vile ambavyo vitakusuia kumfuata Yesu ikiwa ni mzazi, mke/mume, rafiki, na hata nafsi yako unaikana.

Hivyo kama umefanyika mwanafunzi wa Yesu…basi fahamu kuwa unapaswa kuithamini sana hiyo nafasi maana ni wachache waliopata wewe ukiwa miongoni.

Hivyo “shika sana ulicho nacho, ASIJE MTU AKAITWAA TAJI YAKO” 

Usikubali kitu chochote kikurudishe nyuma kiimani, usikubali ndugu, marafiki, anasa, tamaa za ulimwengu, tamaa za ujanani, udandanyifu wa mali n.k usikubali kabisa ikufanye kurudi na kuwa viguvugu. ITHAMINI WOKOVU uliopewa bure. Ni heri ulale njaa na upitie mateso ikiwa ni mapenzi ya Mungu kuliko kuacha wokovu… ndivyo biblia inavyotufundisha.

1 Petro 3:17 Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.

Ithamini neema ya wokovu, neema ikiondoka hairudigi, hivyo usikubali kurudi rudi nyuma kwasababu ya tamaa za mwili, jifunze kwa Esau, aliuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwasababu ya njaa..akaja baadaye kulilia kwa uchungu lakini hakuupata tena (Mwanzo 25;32).

Na kama we ni mmojawapo ya wanaoidharau injili, Fahamu kuwa ipo siku utautafuta wokovu kwa machozi mengi na kulia na kusaga meno na hautaupata.. Siku hiyo utakapoona, wenzako hawapo tena duniani wameshanyakuliwa wameenda mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo, wanashangalia, kwa furaha isiyo na kifani, na wewe upo hapa duniani, huna lolote nakuambia siku hiyo utalia sana..Leo unacheka lakini hiyo siku utalia sana,.

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Mpaka sasa hakuna asiyejua kuwa unyakuo upo karibuni kutokea, tumebakiwa na siku chache sana pengine wiki, au miezi, lakini tujue kizazi chetu kimekidhi vigezo vyote vya kushuhudia tukio la kurudi kwa pili kwa Yesu duniani. Swali ni je! Wewe umejiwekaje tayari leo? Je! Ni kama Yakobo ambaye usiku na mchana alikuwa anautafuta urithi usioharibika kwa hali na mali, au kama Esau aliyedharau Baraka za mbali kwa mafanikio, na pesa za muda tu.

Waebrania 12:16 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja.

17 Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi”.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *