Je baraka za kweli za wazazi kwa watoto ni zipi?

Watoto No Comments

Shalom, karibu tuongeze maarifa ya kumjua Mungu wetu,

Na leo kwa Neema za Bwana tutaangazia jinsi gani tunaweza kuwabariki watoto wetu, na kujua ni kanuni ipi tutaitumia ili tuzifikishe kwa Watoto, tofauti na inavyodhaniwa kuwa kumtamkia baraka kwa vinywa vyetu inatosha, ni sawa kufanya hivyo lakini leo tutaenda mbali zaidi,

Wewe kama mzazi au mlezi yakupasa uyafahamu haya ili umlee mtoto wako kwenye njia inayompendeza Bwana..na kukua Katika maadili mema.. kwasababu ukisema unabariki tu kwa kinywa bila kufanya kwa matendo basi uwezakano wa kutokea hiyo baraka utakuwa hauna nguvu kabisa..

Hizi ni njia bora zikazokwenda kufanya baraka yako uliyoitoa kwa mtoto ifike kwa viwango vingine kama ukiambatanisha na haya,

1) KUWA NA DESTURI YA KUMFUNDISHA SHERIA ZA MUNGU,

Hili ni jambo unalopaswa kulizingatia wewe kama mzazi au mlezi, hakikisha unamfundisha mtoto kuzijua sheria za Mungu zilizopo kwenye maandiko, huku ukifanyika kuwa kielelezo mbele yake kama mmoja wapo wa wewe unazishika sheria za Mungu, kwasababu haiwezekani kumfundisha mtoto halafu wewe huziishi,huzitendi, lazima aone kwanza kutoka kwako ukizitenda ili imfanye na yeye kuwa rahisi kuzipokea na kuzishika, usipofanya hivyo itakuwa kama ni kazi bure,itamchukua muda kukusikiliza..

Mithali 1:8 “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

9 Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako”.

2) USIMNYIME MAPIGO

Watu wengi wamekuwa wakilipinga hili hasa kwa Watoto,wakiamini kwamba ukimpiga mtoto ni kama humpendi au unamyanyasa, jambo ambalo si kweli, kwasababu maandiko yanasema ukimuadhibu Mtoto hatakufa bali unamwokoa na kuzimu, na hii itaonekana ni njia isiyo nzuri lakini ndio mojawapo ya njia itakomfanya mtoto wako apokee baraka zaidi..

Na hapa si anaadhibiwa tu bali ni kwa yale makosa yanayofanyika kwa makusudi au ni makosa yanayojirudia sana,

Mithali 23:13 “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.

14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu”.

3) MFUNDISHE UMUHIMU WA KUISHIKA ELIMU

Hili ni jambo ambalo wazazi wengi wamekuwa wakianza nalo kwa asilimia kubwa juu ya watoto wao, jambo ambalo si baya, lakini lazima ufahamu ni elimu ipi utakayomfundisha,wengi wamekuwa wakiwafundisha umuhimu wa elimu za shuleni,na kwanini wanapaswa wasome, lakini  nakwambia elimu anayotakiwa kuifahamu na kujua umuhimu wake ni elimu ya ufalme wa Mungu, (Elimu ya Mungu kwanza) ndipo elimu ya shuleni, (duniani) ifuate

Sasa kwa kufanya hivyo utakuwa unazitamka baraka zake si katika Maneno tena bali kwa kupitia vitendo maana  kuanzia hapo ataanza kupata uelewa zaidi..

Mithali 4:13 “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako”

4) MFUNDISHE PIA KUZISHIKA SHERIA ZA NCHI PAMOJA NA KUWAHESHIMU WENYE MAMLAKA,

hakikisha Mtoto wako unamfundisha kuzijua sheria za nchi yake na jinsi ya kuzitunza bila kushurutishwa, na kuwaheshimu viongozi wote wanaotawala Katika kila ngazi bila ubaguzi, na hiyo itakuwa ni baraka kwake kwa siku za mbeleni au atakapokuja kuwa mtu mzima..

Mithali 24:21 “Mwanangu, mche Bwana, NA MFALME; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;

5) MFUNDISHE NJIA YAKE INAYOMPASA

Wazazi wengi wamekuwa wakiwaachia Watoto wao wafanye kama wanavyotaka wao Watoto, utakuta ni mtoto analilia simu ya mzazi wake na mzazi wake bila kuwa na maarifa anampa achezee magemu au pengine anamuekea yeye mwenyewe, na wamefika mbali zaidi wanawanunulia Mpaka watoto simu wamiliki, jiulize hiyo ndio njia inayompasa aipite mwanao katika umri huo na jinsia yake?

Jiulize hayo mavazi unayomvisha mwanao ndio njia anayotakiwa kupita, vimini na vibukta, matusi na masengenyo unayotao Mbele yake, jiulize unamfundisha apite njia gani? mtoto masaa mengi anaangalia tv,tamthilia zimejaa kwenye kichwa chake zinaanza sangapi na zinaishaje, je hiyo njia inayompasa mwanao, ni wakike, wakiume lazima ujue ni njia gani anayopaswa kuipita ili aendelee kusimama kwenye nafasi yake kama mtoto..

Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”

Yazingatie hayo kila siku kwa mwanao na huku ukizidisha kumuombea, na kuomba kwa ajili ya familia,uzao,ukoo wako, kwa kufanya hayo,hapo utakuwa unawatamkia baraka nyingi zenye nguvu zaidi bila hata kuzitoa kwenye kinywa, na Mungu atambariki na kumpenda mtoto wako..

Marko 10:14,16

[14]Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.

[16]Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *