
Je umekusudiwa uzima wa milele?
Matendo ya Mitume 13:48 “Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.”
Shalom, karibu tujifunza Neno la Mungu..
Ni jambo la kuogopesha kusikia kuwa wapo watu waliokusudiwa uzima wa milele, na wapo ambao hawajakusudiwa uzima wa milele. Na hilo linatupa picha kuwa suala la wokovu sio jambo la kubabaisha bali ni mpango wa Mungu mkamilifu ambao ulishapangwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu..alishakuwa na Idadi kamili ya watakaokolewa na akawaandika katika kitabu chake cha uzima..
Ufunuo 17:8 “ Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama…”
soma pia Waefeso 1:4
Na ndio maana Bwana Yesu alisema..
Yohana 6:44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho”.
Ikimaanisha kuwa tendo la kumwamini tu Kristo na kumfuata kwa uaminifu wote sio jambo la mtu tu kujiamulia, bali ni jambo ambalo Mungu alishalipanga kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu na hivyo akamchagua mtu huyo, kisha akamwekea mwiitikio huo ndani yake na ndio maana akamwamini na kumfuata bila kigugumizi chochote..
Sasa nitajuaje kama nimekusudiwa uzima wa milele?
Kama tulivyosoma hapo juu anasema wote walioakusudiwa uzima wa milele WALIAMINI..Unaona? Waliamini kile walichohubiriwa wakati ule ule, maana yake wakaenda kubatizwa, wakadumu katika imani, na utakatifu, wakawa kila siku wanalitendea kazi lile Neno walilokuwa wanafundishwa na mitume..
Vivyo hivyo na wewe unaposikia Neno la Mungu likakuchoma na ukaliamini ukaamua kutubu/kubadilika hapo tayari umekusudiwa uzima.
Kwa mfano unapolisikia hili Neno linasema “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa MAVAZI YA KUJISTIRI pamoja na kuwa na adabu nzuri, na moyo wa kiasi;.…” (1Timotheo2:9) ukaliamini hilo Neno ukaenda kutoa mavazi yote yasiyo heshima kama zile zinazobana mwili na kuchora maumbile yako na zile fupi zinaonyesha mapaja yako (vimini), na zile za kifua wazi na mgongo wazi ukatoa zote na kuchoma moto pasipo kuangalia pembeni hiyo ni ishara kuwa umechaguliwa tangu awali kupokea uzima wa milele.
Halikadhalika unaposoma Neno la Mungu katika kumb.22:5 kuwa “mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanye mambo hayo ni MACHUKIZO KWA BWANA, Mungu wako.” Ukaliamini hilo Neno na kulitii kwa kuamua kuondoa mavazi yasiyopasa jinsia yako ukayachoma moto, hapo ni wazi kuwa upo miongoni mwa wateule waliokusudiwa uzima wa milele.
Na maagizo yote yaliyoandikwa ndani ya biblia takatifu ikiwemo mapambo (1Petro3:3), kufunika kichwa ibadani kwa mwanamke (1Wakorintho 11), na mengineyo ukiamini hayo maagizo kwamba yametoka kwa Mungu na sio kwa wanadamu, ukaamua kutii, hapo ni wazi kuwa upo miongoni mwa waliokusudiwa uzima tele.
Vile vile kijana unaposoma ujumbe huu na ukakutana na andiko hili 1Wakorintho6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu; wala waabuduo sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.” Na kwamba watu wa namna hiyo sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti sawa sawa na Ufunuo21:8, ukalisikia Neno hili likakuchoma na ukaliamini ukajutia makosa yako ukatubu kwa kumaanisha kuziacha kabisa na kuamua kumfuata Yesu kwa gharama zote, basi fahamu kuwa umekusudiwa uzima wa milele.
Lakini ukilipuuzia ukaendelea na ulevi wako, ukaendelea na uasherati, kuishi na mke/mume wa mtu, ukaendelea kujichua au kujisaga (masturbation), ukaendelea kumtumikia dhambi, ukaendelea kuupenda ulimwengu na tamaa zake, ukaendelea na usengenyaji, rushwa, uchawi, kujipamba kwa mapambo ya kiulimwengu na kuvaa mavazi ya kiulimwengu, ukaendelea kusikiliza miziki za kidunia, na kutazama picha chafu (pornography), ukaendelea kufanya mambo yote mabaya na unasikia kila siku Neno la Mungu na wala hauhukumiwi moyoni mwako, wala huna mpango wa kugeuka/kutubu, basi huwenda hujakusudiwa uzima wa milele.
Lakini kama unasikia kuchomwa au kuhukumiwa kila unaposikia mahubiri kama haya au unapolisikia Neno la Mungu linalokukataza kufanya dhambi, basi fahamu kuwa Mungu anakupenda na amekukusudia kukupa uzima wa milele, unachopaswa kufanya ni wewe tu kutii na kuamua kumpa Yesu maisha yako kwa asilimia zote. Naye atakubadilisha na kukupa nguvu ya kuishi maisha ya utakatifu siku zote.
Hivyo usiendelee kujifanya hausikii sauti ya Mungu inayozungumza ndani ya moyo wako… maana kuchaguliwa ni neema tu. Wala usiseme nitaokoka baadaye maana neema ya Mungu haitakusubiria..ikiondoka hairudi tena, na wala hautaweza kupata hii nafasi tena, utakuwa umepotea milele.
Hivyo ikiwa upo tayari kumpa Yesu maisha leo na inahitajika msaada tutafute kwa namba zetu hapo chini nasi tutakusaidia.
Bwana akubariki.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.