JE! UNATAMBUA WAKATI TULIOBAKIWA NAO?

Siku za Mwisho No Comments

JE! UNATAMBUA WAKATI TULIOBAKIWA NAO?

Shalom, Nakusalimu kwa jina lipitalo majina yote Mbinguni na duniani jina la YESU KRISTO wa Nazareti.

Karibu tujikumbushe majira na nyakati tunayoishi. Ni muhimu sana kufahamu nyakati na majira tunayoishi.

Kwa kawaida katika jambo lolote kufahamu wakati uliobakiwa nao, ni nyenzo kubwa ya kukusaidia kuamua mtindo wa maisha utakaoendana nao sasa.

Kwamfano mwanafunzi anayetambua kuwa muda wake wa masomo umekaribia kuisha, bado wiki 2 afanye mtihani wa taifa, utaona tu kusoma kwake kunavyobadilika, ataongeza bidii kumalizia viporo vilivyosalia vya masomo na wakati mwingine hata kukesha.

Mfanyabiashara anayefanya kazi katika soko, akijua muda wa jioni wa kufungwa soko umekaribia, huwa uuzaji wake unabadilika, utaona pengine atapunguza bei za bidhaa ili auze haraka, na pia hatatumia muda mrefu kubangaizana na mteja, bali atakuwa ni mchacharikaji tofauti na alivyokuwa wakati wa asubuhi au mchana.

Hiyo yote ni kwasababu gani? Ni kwasababu anajua muda wake ni mchache baada ya hapo hakutakuwa na kazi tena.. hivyo wakizembea watapata hasara ya kazi yao.

Na biblia inatuambia hivyo…tuweze kupima wakati tuliobakiwa nao, ili tuishi ipasavyo sasa. Ni muhimu sana.

Inashangaza, kuona shetani anatambua muda aliobakiwa nao, kwamba ni mchache sana, lakini sisi wengi hatujui wakati tuliobakiwa nao…ni hatari sana.

Ufunuo wa Yohana 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”

Umeona, shetani anajua muda wake umeisha, na ndio maana hatushangai kuona kazi zake zinavyozidi sana ulimwenguni sasa kuliko zamani.

Maovu yanafanyika nje nje, uzinzi sasa ni hadharani unasambazwa kwenye mitandao ya kijamii, anasa kila kona, vitendo viovu, chuki, vita, uchawi, wizi, matusi, ndoa kuvunjika, ushoga, rushwa n.k. Vyote hivi kila kukicha vinakithiri.

Kwasababu gani? Kwasababu utendaji kazi wa shetani umebadilika, anafanya kazi kwa nguvu ili akupate mtu kama wewe/mimi atupeleke jehanumu.

Hivyo, na sisi hatupaswi kuwa kama wajinga, huu si wakati wa kusubiri subiri, au kungojea ngojea…MUDA UMEKWISHA!!, unyakuo wa kanisa upo karibuni. Yesu yupo mlangoni kuja kuwachukua watakatifu wake. Usiseme siku moja nitaokoka.

Tambua kuwa muda uliobakiwa nao ni mchache, huwenda leo usiku ndio Yesu anarudi. Akikukuta katika hali hiyo utasema nini? Utasema sikujua?

Hii ni saa ya kuamka usingizini, ukijua kuwa kifo kinaweza kukuta wakati wowote..Okoka ndugu, wokovu si dini fulani tu au dhehebu fulani, wokovu ni kwa watu wote walio chini ya jua.

Warumi 13:11 “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini.

Waefeso 5:14 Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

Mlango wa neema upo wazi sasa, lakini hautakuwepo sikuzote. (Luka 13:24-25). Embu leo fanya uamuzi huo wa kumgeukia Yesu, na yeye mwenyewe atakupokea.

Ikiwa upo tayari kumpa Yesu maisha yako leo, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *