Je! Unawaza kumfanyia Mungu nini katika maisha yako?
1 Wafalme 8:17 “Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
[18]Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ULIFANYA VEMA KUWAZA HIVI MOYONI MWAKO”.
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze maneno ya uzima.
Daudi ni mtu aliyempendeza moyo wa Mungu kuliko Wafalme wengine waliotawala Israeli, kwasababu alikuwa na moyo wa kitofauti.
Utakumbuka baada ya Wana wa Israeli kutoka Misri na kuingia katika nchi yao ya ahadi, watu wote baada ya kuiona ile nchi ni nzuri walitawanyika na kila mtu kwenda kukaa sehemu yake, walijenga na kupanda na kufanikiwa wakamsahau Mungu, Wao walifanikiwa lakini Mungu katikati yao hakuwa na nafasi yoyote, wao walikaa kwenye makasri lakini Mungu alikaa kwenye mahema ya giza. Na iliendelea hivyo kwa kipindi kirefu cha zaidi ya mamia ya miaka, na hakukuwa na mtu yeyote kutia moyo wake ufahamu kuona kwamba kwanini sanduku la Mungu linakaa kwenye mahema yenye giza leo huku kesho kule, Mungu mkamilifu anayetujali hapaswi kukosa sehemu ya kukaa, Ndipo Daudi siku moja akatia moyo wake ufahamu na kusema nimtengenezee Mungu wangu mahali pa kukaa, haiwezekani yeye akae kwenye jumba la kifahari wakati Bwana Mungu wake hajamjengea nyumba, ndipo Daudi kwa bidii akaiteka ngome ya Sayuni (YERUSALEMU), Kisha akakusudia kuanzia huo wakati amjenge Mungu wake nyumba ( yaani HEKALU). Na ndipo Mungu akamwambia Daudi.
2 Samweli 7: 2 “Mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.
3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe.
4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,
5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, JE! WEWE UTANIJENGEA NYUMBA, NIKAE NDANI?
6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.
7 Mahali mwote nilimo kwenda na wana wa Israeli wote, JE! NIMESEMA NENO LOLOTE NA MTU YO YOTE WA WAAMUZI WA ISRAELI, NILIYEMWAGIZA KUWALISHA WATU WANGU ISRAELI, NIKISEMA, MBONA HAMKUNIJENGEA NYUMBA YA MIEREZI?
8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;
9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.
10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza;”
Umeona moyo wa Daudi, kumbe! Kuna mambo ambayo Mungu hasemi wala hamwambii mtu afanye, japo anatamani sana, lakini anasubiri aone ni nani atatia moyo wake ufahamu na kuwaza kufanya..Daudi alipowaza tu kumjengea Mungu nyumba, ndipo akafungua mlango wa Mungu kusema nae juu ya wazo hilo! Kumbe, Mungu alikuwa anataka ajengewe nyumba lakini hakusema na mtu yoyote, alitaka mtu ambaye atatia moyo wake ufahamu kuwaza jambo hilo ndipo sasa aseme na mtu huyo na kumpa njia ya kufanikisha.
Hata sasa, Mungu anatafuta mtu ambaye atatia moyo wake ufahamu kuwaza kufanya jambo lolote kwa ajili yake. hivyo mimi na wewe hatuna budi kutia mioyo yetu ufahamu kuwaza kufanya kazi ya Mungu.
Jiulize je! tangu ulipookoka, umewahi kuwaza kupeleka injili kwa watu ambao hawajaokoka? Umewahi kuwaza kumtumikia Mungu kwa kazi yako hata kama kipato ni kidogo? We ni mwanafunzi upo shuleni, umewahi kuwaza kuwahubiria wanafunzi wenzako? Kumbuka Mungu anatafuta tu mtu ambaye atatia moyo wake ufahamu kuwaza, yeye anajua jinsi ya kufanikisha mawazo yako.
Hivyo leo anza kutia moyo wako ufahamu kuwaza kufanya jambo lolote kwa ajili ya kazi ya Mungu (Injili), anza kuwaza kuboresha nyumba ya Mungu (kanisa), angalia ni nini kimepungua pale kanisani, usiwe tu mkristo wa kwenda kanisani na kurudi. Yapo mambo mengi ambayo Mungu anatamani utie moyo wako ufahamu kuwaza kuyafanya.
Lakini kama hujaokoka, unapaswa leo kutia moyo wako ufahamu na kuwaza juu ya hatima yako, maana muda tuliobakiwa nao ni mfupi. Unyakuo wa kanisa umekaribia na vilevile siku zetu nazo za kushi hapa ni chache. Jiulize je! utaenda kuwa mgeni wa nani kule ng’ambo na umesikia injili mara nyingi?
Chukua leo uamuzi wa busara kumpa Yesu maisha yako kabla hujachelewa! Na unampa Yesu maisha yako kwa kutubu dhambi zote na kumaanisha kuacha ulimwengu na tamaa zake, kisha unaenda kubatizwa kwa maji mengi na Kwa jina lake yaani jina la Yesu Kristo wa Nazareth sawa sawa na matendo 2:38.
Ubarikiwe.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.