Jihadhari usipoteze nafasi ya kuingia mbinguni.

Biblia kwa kina No Comments

Jihadhari usipoteze nafasi ya kuingia mbinguni.

(Sehemu ya kwanza)

Ni vizuri tufahamu kuwa sio watu wote wanaojulikana kama wakristo wataingia mbinguni! Ni wale tu waliokuwa waaminifu mpaka mwisho ndio watakaongia katika ile mbingu mpya na nchi mpya.

Na tunaingia tu kwa neema, lakini ni vizuri tuelewa mapema kuwa hii neema sio kama tunavyodhania kuwa tukishaokolewa tu kwa neema inatosha, tayari tumepata ticket ya kuingia mbinguni hata kama tutafanya dhambi.

Ndugu Yangu ukiamini hivyo utakuwa umepotea, kuokolewa kwa neema na kwenda mbinguni ni jambo lingine kabisa.

Kama ingekuwa ni hivyo, basi Bwana asingesema maneno haya…”waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.” (Mathayo 22:14).

Maana yake katika safari ya kwenda mbinguni kunaanza kwanza kwa kuitwa kisha kuteuliwa. Na kuitwa maana yake umechaguliwa, na hapa ndipo hilo neno tunaokolewa kwa neema inapokaa, kwasababu hatua hii ya kuchaguliwa/kuitwa haingalii kigezo chochote…mtu anajikuta tu anashawishika kumwamini Yesu Kristo na kuamua kumtii na kumfuata.

Na hii nguvu inayotuvuta tumwamini Mwana wa Mungu haipo kwa watu wote..bali ni wale tu waliochaguliwa tangu awali kabla kuwekwa msingi wa ulimwengu.. Ndio maana tunapaswa kuithamini sana hiyo neema pindi inaposhuka juu yetu, wapo watu ambao hawamwamini kabisa Kristo.. ni kwasababu neema ya Mungu haijafunuliwa juu yao. Na pasipo neema haiwezekani kamwe kumwamini Yesu na kumfuata.

Na hii neema inapokuja kwa mtu, haingalii wingi wa dhambi zake au maisha yake kwa ujumla, awe ni tajiri au maskini, mfupi au mrefu, anafaa au hafai,  neema haingalii hivyo vyote.. kwa ufupi hakuna sababu yoyote inayomfanya mtu achaguliwe, tunasema ni neema tu, hatuwezi sisi kujua zaidi ya hapo kwamba kwanini huyu achaguliwe na huyu asichaguliwe…ikiwa umechaguliwa unapaswa kushukuru tu na kuithamini hiyo neema.

Kumbuka neema haimlazimishi mtu lakini inakushawishi tu wewe ufanye maamuzi ya kumwamini Yesu na kutubu dhambi zako.

Na utajuje kuwa upo miongoni mwa waliochaguliwa? Bila shaka utasikia msukomo ndani yako inayokusukuma kumfuata Yesu, utasikia tu sauti inayokupa kila sababu ya kumwamini Yesu, ukisikia hivyo ujue kuwa umechaguliwa. Lakini pia ukisikia mahubiri ya kweli kumhusu Yesu au yanayokemea dhambi utasikia kuugua moyoni mwako..au ukitenda dhambi unasikia kuchomwa ndani..hiyo ni ishara kuwa Mungu anakuita.. hivyo ni vyema ukatii hiyo sauti maana sio kila mmoja anasikia hivyo, ni neema tu wewe kusikia na usipoithamini itaondoka na haitakurudia tena, ndio hapo utakuwa hausikii tena kuhukumiwa hata ukifanya dhambi kubwa kiasi gani, ukizini utaona tu kawaida, ukijichua hausikii sauti yoyote inayokuhukumu kuwa jambo ulifanyalo ni hatari kwa nafsi yako, hata ukihubiriwaje hausikii tena hata kuchomwa na Neno la Mungu maana neema haipo kwako tena, na ukishafikia hapo hauwezi tena kuokoka daima… utakuwa umekufa kwa habari ya wokovu na mwisho utaungana na ibilisi katika hukumu ya ziwa la moto. Hayo ndiyo madhadhara ya kuupuzia neema ya Mungu.

Sasa baada ya kuchaguliwa na ukamwamini Yesu Kristo, hatua inayofuata ni uteule, yaani kuteuliwa. Na hapa sio kusikia tena msukomo kama ule wa wito, hapa ni kila mmoja anapaswa apige gharama ya kukubaliana na vigezo vya kuingia katika hii hatua… maana yake sio jambo la kusema tunateuliwa kwa neema tu hapana..ukikidhi vigezo ndio neema inafanya kazi kukusaidia. Na hapa ndipo watu wengi wanaporudi nyuma kwasababu hawataki kukubaliana na vigezo hivyo.

Na vigezo vyenyewe tunasoma katika..

Luka 14:25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

[26]Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

[28]Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

[29]Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

[30]wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.

[31]Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?

[32]Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.

[33]Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”

Umeona gharama ya kufanyika kuwa mteule wa Bwana? Ni kujikana nafsi na kubeba msalaba wako kumfuata Yesu, sio kusema nimekwisha mwamini nitaokolewa tu kwa neema. Hapana neema haifundishi hivyo, bali inatufundisha kujikana nafsi na kuacha maovu yote na tamaa za kidunia baada ya kumwamini mwana wa Mungu Yesu Kristo soma Tito 2:11-12.

Wanaotubu dhambi zao ni wengi lakini wanaodhamiria kumfuata Kristo ni wachache sana. Unapoamua kuwa binti wa kikristo, uwe tayari kuukana uzui wako, na kuacha kuvaa vimini na suruali, nguo za kikahaba, na mapambo ya kiulimwengu…ili ufanyike mteule wa Bwana vinginevyo bado huwezi kuingia katika ile nchi takatifu.

Hata kama utasema umeokoka. Vile vile kijana unapokuja kwa Kristo uwe tayari kukataa tamaa zote za ujanani, disco, miziki ya kidunina, pombe na sigara, uasherati, unavipiga vita unaamua kumwangalia Kristo kuanzia huo wakati na kuendelea. Ni mambo ambayo ungeweza kuyafanya kama vijana wengine katika ujana wako lakini unajikana kwa ajili ya kuujua uzuri ulio katika Kristo. Na Bwana Yesu akishaona huo moyo wako hapo ndipo na yeye anapochukua nafasi ya kukufanya kuwa mteule na mwanafunzi wake. Unafanyika kuwa mwanafunzi wake kweli kweli kama mitume wake.

Je baada ya kumwamini Yesu umeikana nafsi na kumfuata kweli kweli au bado upo kwenye kundi lile la walioitwa tu?

Kumbuka ni walioitwa na  kuteuliwa na kuwaminiwa ndio watakao shiriki karamu ya mwanakondoo.

Ufunuo wa Yohana 17:14 Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio WALIOITWA, NA WATEULE, NA WAAMINIFU.

Unaweza ukawa mteule na usiwe mwaminifu ukakosa mbingu. Yuda alikubali wito na baada akawa mteule wa Bwana lakini mwisho alikosa mbingu kwasababu hakuwa mwaminifu…akapoteza nafasi yake.

Bwana atusaidie.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *