KILA MTU NA AMHESABU MWENZIWE KUWA BORA KULIKO NAFSI YAKE

Uncategorized No Comments

KILA MTU NA AMHESABU MWENZIWE KUWA BORA KULIKO NAFSI YAKE

Wafilipi 2:3-5 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

[4]Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

[5]Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;”

Soma pia 1Wakorintho 10:24. Biblia inasema..

Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.”

Unafahamu nia ambayo Bwana Yesu alikuwa nayo.. ambayo anataka na sisi tuliomwamini tuwe nayo.

Hebu tusome tena hapo juu, maandiko yananasema..

“Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

Sasa tuendelee kushuka na mstari wa 6, anasema..

ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

[7]bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

[8]tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Umeona nia iliyokuwa ndani ya Kristo, yeye alikuwa ni Mungu aliyekuja katika mwili wa binadamu (1Timotheo3:16), lakini biblia inatuambia hapa..”yeye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa na mfano wa wanadamu.”

Kristo alifanya hayo yote kwa ajili yetu sote, alitaka tuwe na uzima wa milele..kama yeye alivyo. Ni upendo wa ajabu sana Mungu kuacha enzi na mamlaka yake akaja kuwa mtumwa ili tu atupate. (Kristo aliingia gharama kubwa sana ili tupate huu wokovu). Na sasa anatutaka na sisi tuwe na hiyo hiyo nia aliyokuwanayo.

Tusiifurahie tu kuwa ndani ya Yesu na huku ndugu zetu wanaenda kupotea, tunapaswa tuingie gharama..hata kupoteza mali zetu, na heshima yetu ili wengine wapate wokovu wa kweli, ikibidi wakati mwingine tujihatarishe maisha yetu kupeleka injili kwa wengine, tuhatarishe kazi zetu, ndoa zetu, elimu yetu n.k ili wengine wamjue Yesu.

1 Yohana 3:16 Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.

Lakini sio tu kuhudumiana kwa mambo ya rohoni, bali hata na yale ya mwilini. Kristo alikuwa na utajiri wa kila kitu lakini maandiko yanasema alijifanya maskini ili sisi tuwe matajiri.

Na halikadhalika na sisi tuwe na nia hiyo hiyo, tusiifurahie tu kuwa na maisha mazuri, tunalaa vizuri, tunakula vizuri na huku ndugu zetu wanalala nje, wanateseka na njaa, tujitoe kuwahudumia wenzetu kwa kadri tulivyojaliwa, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. (Wakristo tunatakiwa tufikie hapo).

Ni jambo lisilopendeza kabisa kumuona mkristo mwenzako anatembea na mavazi yaliyochakaa na wewe umejaza sanduku hayo mavazi, haipendezi kabisa kumuona ndugu yako katika imani anataabika na njaa na wewe unao huo uwezo halafu unamzuilia usimsaidie. Huo sio upendo wa Mungu.

1 Yohana 3:17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?

Tabia ya ubinafsi na kujijali zaidi ya wengine ni tabia waliyonayo watu wa kidunia ambao wajapata neema ya wokovu, Lakini sisi tuliofanyika wana wa Mungu, tunapaswa kuwajali wengine kama tunavyojijali wenyewe. Hata kama hatuoni faida kutoka kwao. Kipindi fulani Daudi alitoka vitani na nyara walizoziteka, lakini kulikuwa na watu ambao hawakwenda vitani, hivyo wengine wasiofaa kitu waliona hawastahili kupewa kitu chochote isipokuwa kurudishiwa tu watu wao, lakini tunaona Daudi yeye kwakuwa alikuwa ni mtu wa Mungu, hakuona hilo jambo ni sawa kufanya hivyo..aliona ni jambo lisilopendeza Mungu.

1 Samweli 30:20-24 Naye Daudi akatwaa makundi yote ya kondoo na ng’ombe, ambao waliwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine, wakasema, Hao ndio nyara za Daudi.

[21]Kisha Daudi aliwafikilia wale watu mia mbili, waliokuwa wametaka kuzimia, hata wasiweze kumfuata Daudi, wale waliowaacha wakae karibu na kijito cha Besori; nao wakatoka nje ili kumlaki Daudi, na kuwalaki hao watu waliokuwa pamoja naye, naye Daudi alipowakaribia hao watu, aliwasalimu.

[22]Ndipo watu waovu wote na wale wasiofaa, miongoni mwa hao waliokwenda pamoja na Daudi, wakasema, Kwa kuwa watu hawa hawakuenda pamoja na sisi, hatutawapa kitu cho chote katika hizo nyara tulizozitwaa tena, isipokuwa kila mtu atapewa mkewe na watoto wake, wawachukue na kwenda zao.

[23]Ndipo Daudi akasema, La, ndugu zangu, msitende hivyo katika hizo nyara alizotupa BWANA, ambaye ndiye aliyetuhifadhi, akalitia mikononi mwetu lile jeshi lililokuja kinyume chetu.

[24]Tena ni nani atakayewasikiliza ninyi katika jambo hili? KWA KUWA KAMA LILIVYO FUNGU LAKE YEYE ASHUKAYE VITANI, NDIVYO LITAKAVYOKUWA NA FUNGU LAKE HUYO AKAAYE KARIBU NA VYOMBO; WATAGAWIWA SAWA SAWA.

Hivyo basi, Kwa hitimisho ni kwamba Mungu anataka tuwe na nia ya Kristo.. tuwajali ndugu zetu kama tunavyojijali wenyewe, wale ambao hawajafahamu ukweli tusiache kuwahubiria, na halikadhalika tusiache kusaidiana sisi kwa sisi.

Bwana atubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *