Kusudia kukua kiroho
Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Wakristo wengi sana wanatamani kukua kiroho, wanatamani kumjua zaidi Mungu na kutembea na Mungu kwa viwango vingine vya juu zaidi. Bahati mabaya wengi wanaishia tu kutamani hivyo na hakuna jambo linafanyika wanakuwa hawajakusudia ndani yao.
Lakini ukweli ni kwamba “ukuwaji wa kiroho ni kukusudia wewe mwenyewe ndani yako. Na kuchukua hatua”
Mungu hawezi kukupeleka katika viwango fulani ikiwa wewe mwenyewe hujawa tayari/kudhamiria/kukusudia kwenda katika viwango hivyo.
Mungu hawezi kujifunua kwako ikiwa wewe mwenyewe hujachukua hatua madhubuti za kutaka Mungu ajifunue kwako haiwezekani.
Maandiko yanasema..
Yeremia 33:3“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”
Kwa nini anaanza na neno hili “Niite, nami nitakuitikia…” kwa nini asiseme tu “Nitakuonye mambo makubwa, magumu usiyoyajua bila hata kuniita..” kumbe ni jukumu lako wewe kuita..
Ukisoma pia..
Isaya 55:6“Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu;”
Kwa nini anasema “Mtafuteni Bwana?” Je Mungu amejificha mahali mpaka tumtafute? Jibu ni la Mungu hajajifucha kwa yeyote aliekusudia kumjua.
Yeremia 29:13“Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”
Kumbe ili tumuone na kumuelewa Mungu ni lazima tutafute yaani tukusudie kumjua yeye bila hivyo tutaendelea kutamani na kuishia kuwaza tu lakini hakuna kitu kitafanyika.
“Ukuaji wa kiroho sio bahati ambayo mtu anaipata la! Bali ni matokeo ya mtu kukusudia moyoni mwake kuwa mtu wa tofauti.”
Kama vile fedha isivyoweza kukufata ukiwa umelala ndani ni lazima utoke na ukusudie kutoka nje kwenda kutafuta kazi ufanye ili uipate hiyo fedha!, nje na hapo hata kama utalala unawaza pesa na kuota una pesa nyingi ukisema ukae usitoke kutafuta kamwe utaishia kuhadithia tu ndoto na watu watakuona umerukwa na akili.
Ndivyo ilivyo unasema unatamani kukua kiroho kusoma biblia hutaki halafu unasema “nataka nimuelewe Mungu nimsukie akisema na mimi na nitembee katika njia zake nk” halafu hutaki kusoma biblia.
Unataka kuisikia sauti ya Mungu? Soma biblia maana sauti ya Mungu iko kwenye biblia. Unataka kumuelewa Mungu? Soma biblia maana yupo wazi kabisa, unataka kutembea katika njia zake Soma biblia maana njia zote za Mungu ziko katika neno lake wala hakuna njia mpya isiyokuwa katika maandiko.
Unataka Mungu akuitikie Omba, pasipo kuomba wala Mungu hatakuitikia haijalishi unasoma sana biblia usiku na mchana..
Mungu yupo anapatikana wakati wote na majira yote na saa zote ni wewe tu, je umekusudia? Ukuwaji wa kiroho sio sapraizi inatokea tu ghafula la!.
Mtafakari Musa
Unaweza kufikiri Musa alipata nafasi fulani ya upendeleo.. nataka nikwambie ndugu sivyo hivyo kwa Mungu hakuna upendeleo.
Musa anakubali kukaa siku 40 bila kula akizungumza tu na Mungu, Musa anamgoja Mungu kwa kipindi kirefu akiwa amefunga milimani alikusudia kumuelewa Zaidi Mungu na ndio maana alijitoa kikamilifu kwa Mungu pasipo kujalisha chochote kile..
Musa alikuwa na kiu ya kutaka kuuona hata utukufu wa Mungu.
Kutoka 33:18“Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako.”
Musa anamsihi Mungu juu ya jambo hili hebu fikiri kwa dakika chache vipi Kama Musa asingesema na kutaka kuuona utukufu wa Mungu je? Musa angeweza kusema maneno haya…
Kutoka 34
5 Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana.
6 Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;
7mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.
Ni wazi Musa asingemuelewa Mungu katika viwango hivi kama asingetaka kumwambia Mungu vile lakini asingetaka kukaa kule mlimani Sinai hili jambo linsingejitokeza kwa bahati mbaya au kwa upendeleo.
Je wewe unaweza kusubiri kwa muda wa siku 40? (Unaweza kufunga na kumgoja Bwana kwa kipindi kirefu?) Simaanishi ukae siku 40 bila kula bila uongozi wa Roho Mtakatifu utakufa.
Lakini katika hali ya kawaida unaweza kumgoja Bwana na unatamani kumuelewa Mungu na kuuona utukufu wake? Utukufu wa Bwana utauona katika maandiko hakijafichwa kitu Kristo amekuja kumfunua Mungu kwetu jinsi alivyo ukitaka kuuona utukufu wa Mungu msome Yesu Kristo, ukitaka kutembea na Mungu soma maandiko na mfate Kristo kaagiza nini..
Lakini unataka kumuona Mungu, husomi, huombi, kufanyi uinjilisti, wewe ni jumapili kwa jumapili ndugu Mungu utaishia kumsikia tu nakupata taarifa zake kama wana wa Israeli kule jangwani walikuwa wanaishia kupata taarifa tu kutoka kwa Musa Mungu kasema nini.
Kwa nini iwe hivyo kwako ikiwa uko katika agano bora kuliko lile? Kwa nini ? Chukua hatua leo kusudia kukua kiroho fanya maamuzi leo anza kusoma sana biblia anza kuwa muombaji sana.. jitahidi kuwafundisha wengine kile ambacho umejifunza utaona jinsi ambavyo unaanza kumuelewa Mungu katika viwango vingine.
Je umemwamini Yesu Kristo ikiwa bado je unasubiria nini? Na ikiwa umemwamini Yesu Kristo unauhakika kwa kwenda Mbinguni? Kama huna kwa nini? Ishi maisha matakatifu na maisha yako ndio yatakayokupa hakikisho kwa Roho wa Bwana kukushuhudia.
Ubarikiwe sana.
Maranatha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.