KWANINI MAKUHANI WALIAMRIWA KUTWAA MKE MWANAMKE AMBAYE NI BIKIRA TU? (Walawi 21:14)

SWALI: Ni kwanini Makuhani katika agano la kale waliamriwa kutwaa mke mwanamke ambaye ni bikira tu?

JIBU: Ni kweli kabisa kuwa, ipo sababu ya kwanini Mungu aliamuru kuhani yo yote yule katika Israeli atakapooa mke ni lazima huyo mke awe bikira. Katika taifa la Israeli, kuhani yo yote yule, aliye Mkuu au asiye mkuu, alipotaka kuoa hakuruhusiwa kuoa mwanamke ambaye ni kahaba, au mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, bali mwanamke Bikira pekee, ndivyo sheria ilivyosema.

Walawi 21:7 WASIMWOE MWANAMKE ALIYE KAHABAAU HUYO ALIYE MWENYE UNAJISI; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake. 

Unaweza Soma tena 

Walawi 21:12 wala asitoke katika mahali patakatifu, wala asipatie unajisi mahali patakatifu pa Mungu wake; kwa kuwa utakaso wa hayo mafuta ya kutiwa ya Mungu wake u juu yake; mimi ndimi Bwana.

13 NAYE ATAMWOA MWANAMKE KATIKA UBIKIRA WAKE

Lakini hii haina maana kwamba, binti ambaye si bikira aliyetubu dhambi zake, au binti kahaba aliyeacha kufanya ukahaba na kutubu dhambi zake hapaswi kuolewa. La hasha! Au haina maana kwamba, kijana aliyeacha kuishi maisha ya anasa na uasherati na kutubu dhambi zake hapaswi kuoa, hapana! Bali sheria hiyo ILIKUWA INAMFUNUA KRISTO

Kumbuka, maandiko matakatifu yanasema kuwa, torati ni kivuli cha agano jipya (Waebrania 10:1), kumaanisha kuwa, mambo yote ya sheria yalioandikwa katika torati yalikuwa ni kivuli cha mambo yajayo bali mwili ni wa Kristo (yaani kumfunua Kristo), Kwa mfano; kulikuwa na sheria mbali mbali zilizoamriwa katika torati kama vile sikukuu za mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya pasaka, mzaliwa wa kwanza, sabato za siku, wiki, miezi, sikukuu ya vibanda, baragumu, utoaji wa sadaka za dhambi, na zingine nyingi ambazo zote hizo kwa pamoja zilikuwa zinamfunua Kristo ikiwemo na hiyo sheria ya Kuhani kujitwalia mke mwanamke ambaye ni safi na bikira.


SASA SHERIA HIYO INAMFUNUA KRISTO KIVIPI?


Kumbuka kwamba, Kristo Naye ni Kuhani Mkuu (Waebrania 4:14), na wa milele. Na kama ni kuhani Mkuu maana yake ni kwamba, sheria hiyo ya kujitwalia mke safi, bikira, asiye kahaba, asiye na doa na asiye najisi ni lazima itimie kwake kwa sababu torati na manabii haviwezi tenguka, ni lazima yote yaliyoandikwa yatimie (Mathayo 5:17-18).

Hivyo basi, kama ni Kuhani wa milele ni lazima na Yeye ajitwaliea Mwanamke Bikira safi wa milele ambaye ni KANISA TUKUFU NA TAKATIFU, lisilo na doa wala unajisi (makunyanzi na mawaa)

Waefeso 5:27 apate kujiletea KANISA TUKUFU, LISILO NA ILA WALA KUNYANZI WALA LO LOTE KAMA HAYO; BALI LIWE TAKATIFU LISILO NA MAWAA.  

Soma tena.

2 Wakorinto 11:2 Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea MUME MMOJA, ILI NIMLETEE KRISTO BIKIRA SAFI

Umeona hapo? Hivyo basi, sheria hiyo ya kuhani kujitwalie mke safi na bikira pekee ilikuwa inamfunua Kristo (kuhani Mkuu) na Bikira wake safi ambaye ni kanisa litakalokwenda kumlaki hewani siku ile (1 Wathesalonike 4:16-17)


Je! Na wewe ni miongoni mwa Bikira safi (Kanisa) au kahaba na uliyetiwa unajisi? Kama bado unangoja nini? Chukua uamuzi leo wa kutubu dhambi zako na kusafishwa kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa kuzamiashwa katika maji tele na kwa jina la Yesu Kristo, nawe utaoshwa dhambi zako zote kwa damu na maji, na kupokesa kipawa cha Roho Mtakatifu Aliye muhuri wake Mungu.

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

Kwanini Bwana Yesu alijeruhiwa ubavuni pale msalabani?


Msaidizi wa kufanana naye ni nani ambaye Mungu alimfanyia Adamu? (Mwanzo 2:18)


Kwanini biblia inalitambua kanisa kama mwanamke?


Bwana alimaanisha nini aliposema “Heri ayawe yote asiyechukizwa nami?” (Mathayo 11:6)


Kwanini Adamu na Hawa, Mungu aliwaita kwa jina moja ADAMU ?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *