
MACHO YAKO YAMETIWA NURU?
Biblia inasema katika…
Waefeso 1:18 “macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo”
Biblia inapozungumzia mioyo..haimaanishi hii mioyo iliyomo ndani ya vifua vyetu inayosukuma damu…hapana bali inazungumzia utu wa ndani ambao ni roho zetu.
Hivyo anaposema macho ya mioyo yetu yatiwe nuru analenga macho ya rohoni, moyo wa nyama hauwezi kuwa na macho.
Na huwezi kuwa mtu wa rohoni kama macho yako ya rohoni yajatiwa nuru. Na mtu wa rohoni sio mtu anayeona wachawi, au anayeota ndoto, au anayeona maono, mtu anaweza akawa na vipawa hivyo vyote lakini bado asiwe ni mtu wa rohoni.
Mtu wa rohoni ni mtu aliye na ufahamu wa kuzitambua siri za Mungu kwa Roho Mtakatifu. Na siri kuu ya Mungu ipo katika kumjua Yesu Kristo, ambayo biblia inasema kama watawala wa dunia hii wangeijua , wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;(1Wakorintho 2:8)..
Hivyo ukiona wewe kila siku unamjua Kristo katika viwango vingine, basi ujue kuwa wewe ni mtu wa rohoni mwenye viwango vya hali ya juu..Ukiona kila usomapo Biblia unaziona habari za Yesu, kila ukitazama vitu vya asili unaiona injili ya Yesu, kila Ukitazama Maisha ni kama unayasikia maneno ya Yesu yanazungumza na wewe masikioni yanakuonya kila unalotaka kulifanya unatamani liwe linalompendeza Yesu… hapo wewe ni mtu wa rohoni…Na sio ukisoma biblia unaona wachawi, au ukisali unaona wachawi hapo bado hujawa mtu wa rohoni na macho yako hayajafumbuliwa.(hayajatiwa nuru)
Kwahiyo ni muhimu sana kutafuta kufumbuliwa macho ya rohoni, wengi wanatafuta kuona wachawi!, huko sio kufumbuliwa macho, wengine wanatafuta kuona maono..huko nako sio kufumbuliwa macho ya rohoni! Wala kuota ndoto za kimiujiza sio kufumbuliwa macho……kupata kuelewa Kwanini Yesu alikuja duniani, anataka nini sasa, na yupo wapi sasa, na kuyaelewa mapenzi yake na kuyafanya huko ndio kufumbuliwa macho ya rohoni…Na hapo utamwona Yesu kila siku katika Maisha yako..huhitaji macho ya damu na nyama kuhakiki, tayari macho yako ya ndani yanamwona kila siku katika Maisha yako.
Na mtu wa namna hiyo ndiye mtu wa rohoni, na ndiye mtu aliyetiwa nuru katika macho yake..biblia inasema mtu wa namna hii hutambua yote, lakini yeye hatambuliwi na mtu..
1Wakorintho 2:15 “Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu”?

Umeona, ukiwa mtu wa rohoni utakuwa na uwezo wa kuyatambua mambo yote, na siri zote za Mungu wanadamu wasizozijua…hakuna jambo lolote litakuwa ni jipya machoni pako na zaidi ya yote bado utakuwa hautambuliwi na yeyote.. Yaani maana yake, hakuna mwanadamu yeyote mwenye tabia ya asili atakayeweza kukutambua, akikuangalia ataishia tu kuona vya nje, watasema umerukwa na akili kama vile Paulo alivyoambiwa, wengine watasema una mapepo, kama vile Yohana Mbatizaji alivyoambiwa..Wengine watakauambia umelogwa..
Ni kwasababu ufahamu wao umeishia hapo kwenye mambo ya nje, hawawezi kuona zaidi ya hapo..furaha na tumaini lililopo ndani yako..Hawajui kuwa ndani yako ni Roho Mtakatifu anakufundisha, lakini wewe utakuwa na ufahamu wa kuelewa yao yote. Utagundua kuwa wanavyokufikiria wewe sivyo ulivyo.
Na mtu anayeenenda katika mwili (mtu wa mwilini) bado hajafumbuliwa macho, na hivyo hawezi kuona mambo ya rohoni na ni upuuzi kwake.
Mtu anayevaa vimini, nguo za kubana, nguo za jinsia nyingine hajafumbuliwa macho ni mtu wa mwilini, mtu anayezini na anayefanya uasherati, na anayefanya mambo mengine ya kidunia sawa sawa na “Wagalatia 5:19-21” bado ni kipofu wa rohoni, haijalishi anaona maono au anatabiri..bado ni kipofu! Kulingana na biblia.
Halikadhalika mtu ambaye haoni maisha ya mbele baada ya kifo.. mtu huyo ni kipofu haijalishi amefanikiwa sana, mtu ambaye haoni majira na nyakati anazoishi kuwa ni nyakati za mwisho huyo ni kipofu hata kama ana elimu kubwa kiasi gani!!.
Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kufumbuliwa macho ya rohoni..Yaani kutiwa nuru na kuwa mtu wa rohoni.
Na tunafunguliwaje macho ya rohoni?..kwanza kwa kukubali kwamba sisi ni wakosaji, na kisha kwenda chini yake kwa unyenyekevu na kuomba rehema na toba…baada ya hapo kumtii maagizo yake ya kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi na kwa jina lake..kisha kupokea Roho wake mtakatifu..Huyo ndiye aliye na jukumu la kufumbua macho yetu ya rohoni na kutufanya kuyaelewa maandiko..lakini pasipo huyo kamwe hatuwezi kumwelewa Mungu wala kumjua…tutakuwa tu kama Wanyama ambao wana macho lakini hawaoni.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.