Madhara ya kupunguza Maombi.
Katika Maisha usijaribu kufanya kosa la kupunguza maombi…Ni heri ukapunguza muda wa kufanya mambo mengine ambayo unaona ni ya muhimu lakini usipunguze kuomba hata kidogo!..Kama tayari ulishaanza kuwa muombaji, halafu ukaanza kupunguza unamtengenezea adui nafasi ya kufanya uharibifu mkubwa sana katika maisha yako.
Na kitu ambacho watu wengi huwa hutujui ni kuwa maombi ni nguvu za Mungu, bila nguvu za Mungu hatuwezi kudumu katika kuomba, tutajitahidi kwa nguvu zetu lakini tutachoka tu.
Lakini tunapoanza kuomba katika Roho Mtakatifu kadri tunavyozidi kuendelea mbele, ndivyo tunazidi kuwa hodari katika kuomba, ndio hapo unakuta mwanzoni ulikuwa huwezi kuomba hata nusu saa lakini kadri ulivyokuwa unafanya bidii kuomba Kila siku, ipo nguvu ya Mungu ambayo ilikuwa inaachiliwa kidogo kidogo kukuwezesha kuendelea mbele… Ndio maana leo unaweza kuomba masafa marefu bila kuchoka.
Sasa unapoanza kupunguza kuomba ndivyo unazidi kujipunguzia nguvu za Mungu kidogo kidogo na hatimaye maombi yanakuwa ni mtihani mgumu kwako. Hata ukija kurudi tena utaona ni afadhali jana kuliko leo.
Safari ya maombi kila siku kwa mwamini ni kama safari ya kukimbia riadha, unapoanza kukimbia halafu ukafika mahali ukaacha kukimbia ukakaa, unafahamu ili uje kuwasha tena ule moto wa kukimbia kama hapo mwanzo itakugharimu kidogo, kwasababu inchini imeshapoa na kadri utakavyo kaa ndivyo ugumu wa kukimbia tena unaongezeka. Kwahiyo wanachofanyaga wanariadha wanapokuwa safarini, wakitaka kupumzika sio wanakaa kabisa! hapana, wanapunguza tu mwendo wa kukimbia kidogo kisha wanaendelea tena… kwasababu wanajua mwili ukishapoa mpaka urudi tena kama mwanzo ni ngumu.
Na halikadhalika katika safari ya maombi kwa mwamini hatupaswi kupunguza kuomba kabisa, ikitokea labda siku moja imepita iwe ni mara chache sana tena siku hiyo umekosa kweli muda wa kuomba aidha upo katika mazingira yasiyo rafiki.. lakini kupitisha siku tatu mpaka week hiyo ni hatari sana.
Kwahiyo ule mwendo ambao ulikuwa nao katika kuomba hupaswi kupunguza kabisa.
Ukipunguza fahamu kuwa itakugharimu kuja kurejea tena katika mwendo huo.
Leo ukiacha kuomba ukasema utaomba kesho, ni sawa utaomba..lakini utakuwa na mzigo mkubwa wa kuomba kama hapo mwanzo, kadri unavyokaa muda mrefu bila kuomba ndio kiwango chako cha kuomba kinazidi kushuka na hatimaye baadaye utaacha kabisa kuomba.
Utabaki tu na kumbukumbu kuwa zamani ulikuwa unaomba sana…hapo utakuwa umekufa kimaombi, na ukishafikia hapo fahamu kuwa wokovu utakushinda tu, usijidanganye kuwa unaweza kushikilia wokovu bila maombi hiyo haiwezekani, utaanguka tu kwenye majaribu na tamaa za ulimwengu huu. Ndio maana Bwana aliwaambia wanafunzi wake wakeshe wombe wasije wakaingia majaribuni, alijua bila maombi kushinda majaribu ya adui ni vigumu.
Hebu jitathimini hali yako kimaombi ikoje ukilinganisha na ulipoanza, huwenda ulikuwa moto kweli kweli lakini leo hii umebaki tu na historia.
Ulikuwa unaomba kila siku zaidi ya lisaa lakini ukaanza kupunguza..ukawa unaomba chini ya hapo au hata ukapitisha siku bila kuomba, ukazidi kushuka..ukaanza kupitisha siku mbili, tatu, wiki mpaka mwezi, ukiulizwa mara ya mwisho kuomba masaa mawili hukumbuki, mara ya mwisho kukesha ni miezi mitano iliyopita, mara ya mwisho kufunga ni mwezi uliopita wakati ulikuwa haupitishi week bila kufunga walau siku moja, ukiona hivyo ujue upo hatarini kuzama kabisa…unahitaji kupiga yowe kumlilia Mungu akusaidie urudi kama hapo kwanza.
Adui anachowinda kwa mwamini ambaye yupo moto kimaombi ni kupunguza ule moto ili aweze kumrudisha nyuma katika imani vinginevyo hawezi kamwe.
Hivyo atafanya juu na chini atafute mbinu za kumpunguzia ule muda wa kuomba, adui anajua kabisa mwamini akipunguza muda wa kuomba kuna nguvu zinapungua ndani yake, anajua akiacha kuomba siku moja ipo nguvu inapungua ndani, akipitisha siku mbili ndivyo anavyojimaliza … Kwahiyo anatafuta mazingira yoyote ya kumfanya mtu huyu akae mbali na maombi.. apitishe hata mwezi bila kuomba.
Ndicho kilichomtokea Danieli, Adui alipoona Danieli ni mwaminifu kwa Mungu wake na hawezi kumuasi Mungu, alijua ni kwasababu ya maombi anayoyaomba kila siku mara tatu. Hivyo akaanza kutafuta jinsi ya kupunguza huo moto wa maombi, alijua kabisa akifanikiwa kumdhibiti Danieli asiombe kwa mwezi mmoja atakuwa ameshamaliza kabisa nguvu zake za kuomba..hata baadaye akitaka kurudi kuomba ni ngumu na atakuwa ameshamtenga na Mungu kwa kumuangusha kwenye majaribu yake.
Lakini Danieli alishinda hilo jaribu, hakukubali kitu chochote kimurudishe nyuma kimaombi, alikuwa tayari hata kufukuzwa kazi au kushushwa cheo, alikuwa tayari kutupwa kwenye tundu la simba lakini asipunguze muda wake wa kuomba maana alijua ni hila za adui. Hebu tusome kwa ufupi hiyo habari. (Zingatia maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa)
Danieli 6:4 ”Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; KWA MAANA ALIKUWA MWAMINIFU, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.
[5]Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.
[6]Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.
[7]Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, KATIKA MUDA WA SIKU THELATHINI, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.
[8]Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.
[9]Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.
[10]Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) AKAPIGA MAGOTI MARA TATU KILA SIKU, AKASALI, AKASHUKURU MBELE ZA MUNGU WAKE, KAMA ALIVYOKUWA AKIFANYA TOKEA HAPO.
[11]Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.
[12]Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.
[13]Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, BALI AOMBA DUA MARA TATU KILA SIKU.
Umeona hapo, jiulize kwanini iwe ni siku 30, hebu tafakari sheria inatolewa kuwa hakuna kuomba siku thelathini, ni lazima kuna uhusiano kati ya hizo siku na maombi.
Siku thelathini ni siku za kummaliza mwamini nguvu zake za maombi, Adui akishafanikiwa kukufikisha hapo tayari ameshakuweza na kuanzia hapo wokovu wa kweli utasahau… utabakia tu kuwa mkristo wa kawaida vuguvugu. Ndicho ibilisi anachotafuta watu wafikie hapo halafu mwisho watapikwe na Mungu..
Na mwanzoni atakupa ujasiri kwamba unaweza kuishi bila maombi, utajiona unaweza kushinda dhambi, unaweza kushinda tamaa, lakini fahamu kuwa kila unapopunguza muda wa kuomba ndivyo unazidi kuzama taratibu.
Wakristo wengi ambao walikuwa moto kimaombi wamerudi nyuma kwasababu hiyo, hawajarudi tu ghafula, hapana,..walianza kidogo kidogo kupunguza muda wa kuomba, saa baada ya saa, siku baada ya siku na hatimaye mwezi baada ya mwezi..hata wakitaka kuomba hawaoni tena ule uwepo, watajitahidi dakika kadhaa wanashindwa kwasababu wameshajimaliza siku nyingi.
Ndugu kama umekwisha kuanza safari ya maombi, usijaribu kufanya kosa kupunguza huo mwendo, usikubali adui akurudishe nyuma, kuwa kama Danieli ambaye yeye hakukubali mtu yoyote au kitu chochote kiingilie ratiba yake ya maombi.
Usikubali kazi, familia, sheria au chochote kile ikupunguzie mwendo wa maombi, Danieli alikuwa ni waziri mkuu, alikuwa na kazi nyingi lakini bado alikuwa anapiga magoti kila siku mara tatu kuomba. Alijua bila maombi mambo hayaendi hata hiyo kazi hataweza kufanya vizuri, alijua hatoweza kusimama na Mungu vizuri pasipo maombi.

Tunaishi ukingoni mwa nyakati na Yesu yupo mlangoni. ALISEMA
“Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
[35]kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.
[36]Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.” (Luka 21:34-36).
Huu si wakati wa kupunguza kuomba ni wakati wa kuongeza kwasababu siku zimeisha na adui anafahamu.
Hivyo ng’oa nanga leo anza safari ya maombi ya kina kila siku!..kama umerudi nyuma rudia desturi yako kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya.
Maran atha.
Je! Umempokea Yesu wa kweli?
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.