Mapambo yanachochea uzinzi.
Je! Ni kweli kujipamba kwa kutumia mekaups, lipustiks, wanja, wigi, hereni, n.k ni urembo tu? Je! Biblia inasemaje kuhusu kujipamba?
Biblia inasema kujipamba kwenu kusiwe kwa nje. Ahaa kumbe tunatakiwa kujipamba lakini sio kwa nje! sasa kama sio kwa nje, basi itakuwa kwa ndani. Maana yake wanawake wa kikirsto wanapaswa wajipambe kwa mapambo yale ya ndani..na sio yale ya nje, Tunasoma..
1 Petro 3:1 Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;
[2]wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.
[3] KUJIPAMBA KWENU, KUSIWE KUJIPAMBA KWA NJE, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
[4]bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.
[5]Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.
Umeona mapambo yetu!, si kwa kusuka nywele au kuweka nywele bandia (mawigi), sio kujitia madhabahu kama hereni, bangili, au kutia rangi kwenye kucha na mdomoni, sio kupaka mekaups, na kutia wanja. Bali ni kuwa na roho ya upole, na utulivu iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu, hiyo inatosha kwa mwanamke wa kikirsto..kwa maana ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani. Kumbuka sio kwamba zamani hakukuwa na mapambo ya nje! yalikuwepo tu sana, tunasoma wapo wanawake wa kimataifa kama wakina Yezebeli ndio waliokuwa wanajipamba kwa hayo mapambo (soma 2Wafalme 9:30).
Sasa kwanini hatupaswi kujipamba kwa nje kama watu wa kidunia?
Jibu ni kwasababu kwanza Neno la Mungu limetukatasa.. hivyo tunapaswa kutii bila kuulizauliza. Lakini pia siri iliyopo katika mapambo ni kuwa yanabeba maroho ya uzinzi.
Hili ni jambo ambalo watu wengi hawalifahamu, lakini ukijaribu kuchunguza wanawake wanaojipamba, yaani wanapaka mekaups, wanaotia uwanja, lipusticks, n.k utakuta wanatumika sana kuwazinisha watu wengi.. hata uvaaji wao ni wa kizinzi, utakuta wamevaa vimini, kaptula, suruali, au mavazi yaliyobana na kuchora maungo yao.
Utauliza tunalithibitishaje hili kimaandiko?
Kama we ni msomaji wa biblia, utakuwa unafahamu habari ya Yezebeli vizuri, Yezebeli ni mwanamke pekee katika biblia nzima ambaye alikuwa anajipamba, na biblia inatuonyesha alikuwa anajipamba ili awavutie wanaume kwenye uzinzi. Utakumbuka alipopata habari kuwa mwanae amekufa, badala hata ahuzunike na kuomboleza..anakimbilia kwenye kioo ili akajipodoe, akaenda kujipamba, akapamba kichwa, na akajitia uwanja..lengo lake ni ili yule anayekuja kumtafuta amuone na umtamani halafu azini nae. Ndio maana alienda kuchungulia dirishani baada ya kujipamba, Tunasoma..
2 Wafalme 9:22 Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?
[30]Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani.
Umeona hapo, kuna mahusiano makubwa sana kati ya mapambo na uzinzi…bila shaka kama huwa unajipamba kwa pambo lolote lile.. utakuwa we mwenyewe una ushuhuda kwa zile ndoto za uzinzi unazootaga mara kwa mara.
Hivyo leo umeujua ukweli, usiendelee kung’ang’ania mapambo..ni heri uonekane sio mrembo lakini unaenda mbinguni kuliko kusifiwa na ulimwengu lakini sehemu yako ikawa ni jehanum ya moto.. itakufaidia nini?
Biblia inaweka wazi kabisa kuwa wazinzi hawana sehemu katika ufalme wa Mungu bali sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kibiriti soma Ufunuo 21:8.
Ni heri leo uamue kutubu kwa kumaanisha kuondoa mapambo yote na kuviteketesa kabisa pamoja na mavazi yote ya kizinzi.
Rudi kwenye uasili wako maana Mungu anapendezwa na jinsi alivyokuumba, usikubali kubadili uumbaji wake kwasababu tu ya kutaka kuwapendeza wanadamu, usikubali kutumiwa na ibilisi kama chombo cha kuwazinisha wengine.
Kama umeokoka na ulikuwa uyafahamu haya, basi leo umeyafahamu fuata ukweli..na kama hujaokoka basi huu ndio wakati wako sahihi wa kumpa Yesu maisha yako. Fahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa siku za mwisho na we mwenyewe haujui mwisho wako.. kuna hatari kubwa itakutokea ukifa nje ya Yesu.
Maran atha.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.