MTASITA-SITA KATIKATI MAWAZO MAWILI HATA LINI?

Biblia kwa kina No Comments

MTASITA-SITA KATIKATI MAWAZO MAWILI HATA LINI?

1Wafalme 18:20 “Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli.

[21]Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? BWANA akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.

Je! U miongoni mwa wanaosita-sita katikati ya mawazo mawili?

Kusita-sita ni nini?

Ni hali ya kusuasua kufanya maamuzi yaliyo sahihi kwa jambo sahihi na kwa muda au wakati sahihi. Au kutangatanga kunakotokana na kutaka mambo mawili kwa wakati mmoja na kushindwa kuchagua jambo moja lililo sahihi zaidi.

Na siku zote mtu anayesita-sita katikati ya mawazo mawili, au nia mbili, ni vigumu afanikiwe katika jambo analolitaka. Kwa mfano tuchukulie mkulima ambaye anataka kumwaga mbegu shambani, asipoweka imani dhabiti kuwa zile mbegu zitaota, na kuzaa mazao mengi, akabaki katikati ya mawazo mawili, Kwamba nioteshe au niuze? Mwisho wa siku msimu wa kuotesha utapita na pia bei ya hiyo mbegu itashuka, hivyo ataishia kupata hasara. Kwasababu alisita-sita kufanya maamuzi sahihi kwa muda sahihi. Aliogopa kumwaga mbegu shambani kwa hofu ya kuogopa kuota wakati biblia inasema…

Asubuhi panda mbegu zako, Wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa, kama ni hii au hii, au kama zote zitafaa sawasawa.” (Mhubiri 11:6)

Ndicho kilichomkuta yule mtumwa ambaye Bwana wake alimpa talanta moja akafanye biashara(akaoteshe)ili alete faida, wakati wenzake walienda kufanya kazi bila kisita-sita, yeye alienda kuficha talanta yake ambayo ni kama mfano wa mbegu, na baadaye Bwana wake alipokuja kudai mavuno, wakati wenzake wanaleta mazao, yeye analeta mbegu zake kama alivyopewa.. hakuna faida alichozalisha, bali ni hasara tu na kupoteza muda, kwasababu gani? Kwasababu aliogopa, aliogopa nini? Aliogopa kumwaga mbegu, aliogopa kufanya biashara! Hivyo akabaki katikati ya mawazo mawili na mwishowe akaja kutupwa katika giza la nje, Tunasoma..

Mathayo 25:13 Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.

[14]Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.

[15]Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.

[16]Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.

[17]Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.

[18]Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.

[19]Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.

[20]Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.

[21]Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.

[22]Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.

[23]Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.

[24]Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;

[25] BASI NIKAOGOPA, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.

[26]Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;

[27]basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

[28]Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

[29]Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

[30]Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Umeona hapo! hebu jiulize na wewe ndugu unayesoma ujumbe huu, je! upo katika nia ipi? nia ya Kristo au nia ya ulimwengu? Au upo katikati ya nia mbili/ mawazo mawili? angalia biblia inasema..

Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote”. (Yakobo 1:8).

Mtu wa nia mbili hawezi kufanikiwa, atabaki kusita-sita katika njia zake zote! Na mwisho wake ni kuishia kupata hasara kama yule mkulima, au kama yule mtumwa ambaye alishia kutupwa nje.

Na ndivyo itakavyokuwa, siku ile watu wengi sana watatupwa nje, biblia ilisha tabiri na ni lazima itimie.

Mathayo 8:11 Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

[12]BALI WANA WA UFALME WATATUPWA KATIKA GIZA LA NJE, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Hebu linganisha hayo maneno na ile habari ya yule mtumwa asiyefaa..

Mathayo 25:30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali KATIKA GIZA LA NJE; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Huku anasema wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, na huku pia anasema mtumwa asiyefaa atatupwa katika giza la nje, ambapo ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Wana wa ufalme ni wakina nani? Ni watu wanaomjua Yesu (wakristo) lakini hawajawa tayari kuingia ndani yake, na mtumwa asiyefaa ni watumishi wote wanaomhubiri Yesu lakini hawapo tayari kuzalisha faida, hawapo tayari kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu wote, wana nia mbili…wanashikilia udunia na utumishi kwa pamoja, hao ndio watatupwa katika giza la nje.

Ndugu yangu, unapoamua kumfuata Yesu na kuwa mwanafunzi wake, kanuni ni kuacha vyote. Kama yeye mwenyewe alivyosema.

Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,

Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” (Luka 14:27&33)

Kuacha vyote ni kuondoa kila kitu ambacho kimeshikilia moyo wako, iwe ni mali, cheo, elimu, umaarufu n.k na vile ambavyo vinakusuia kumfuata Yesu ikiwa ni ndugu, marafiki, kazi, mume/mke, na hata nafsi yako unaikana. Mfano nafsi yako na mwili wako vinakushawishi uupende na uufurahie ulimwengu, uende kwenye anasa mbali mbali, uende na fashions na mitindo za kiulimwengu, unasema HAPANA.

Halikadhalika bosi wako anakuambia usipokubali rushwa, au anakuambia usipovaa mavazi fulani ambayo kwa mkristo si halali mfano mavazi ya jinsia nyingine kama suruali na wewe ni mwanamke, anakuambia usipotumia mkorogo kidogo, usipovaa wigi kichwani, usipopaka rangi kwenye kucha na mdomoni huwezi kukaa kazini! hapo unapaswa useme HAPANA, kama ni kupoteza kazi ni heri upoteze maana sio mapenzi ya Mungu akupe kazi halafu uende kutupwa nje, sio mapenzi ya Mungu ukupe mtoto halafu huyo mtoto awe tanzi kwako, au mume/mke awe kikwazo.

Hivyo katika kumfuata Yesu wa kweli ni lazima uache hayo yote yanayokinzana na yeye..pasipo kujalisha watu watakuonaje, au ni nini kitakutokea, kama ni kuachwa na ndugu unakubali, kama ni kupoteza kazi unakubali, kama ni kuitwa mshamba unakubali, kama ni kuachwa na marafiki unakubali, unakubali kila kitu…huko ndiko kuwa mwanafunzi wa Yesu… kinyume na hapo utakuwa unajidanganya umeokoka, unamjua Yesu, unaenda kanisani , unamtumikia lakini hutaki kuacha vyote, hutaki kuacha ulimwengu, hutaki kuacha fashions na mapambo ya kiulimwengu, hutaki kuacha mavazi ya kiulimwengu, hutaki kuacha biashara haramu, hutaki kutoa hiyo mali moyoni mwako, hutaki kuacha kiburi cha uzima…hapo ndugu fahamu kuwa upo katikati ya mawazo mawili, na leo Bwana anakuambia utasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini?

Kama ni kuwa baridi ni heri uchague kuwa hivyo..kuliko kuwa vuguvugu, si baridi wala sio moto. Bwana anasema atawatapika watu kama hao wenye kusita-sita katikati ya mawazo mawili. (watu vuguvugu).

Ufunuo wa Yohana 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; INGEKUWA HERI KAMA UNGEKUWA BARIDI AU MOTO.

[16]Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.”

Je! unataka kutapikwa na Bwana? Kama hutaki acha uvuguvugu? Kama hutaki kutupwa katika giza la nje acha kusita-sita katikati ya mawazo mawili. Amua kumfuata Yesu kweli kweli kwa kuikana kwanza nafsi yako na mwili wako na kukubali kubeba msalaba wako yaani kuachwa na marafiki, ndugu, kupoteza kazi ikibidi, kudharauliwa na kuonekana mjinga, kubaliana na hayo yote maana ndivyo itupasavyo kupitia kama yeye alivyopitia… Lakini baada ya hapo kuna taji imewekwa. Hivyo hatupaswi kuogopa kupoteza maana sharti tupoteze ndio tupate..hiyo ndiyo kanuni ya ki-Mungu.

Mathayo 16:24 Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

[25]Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

Usiogope kupoteza?

Yule mtumwa asiyafaa aliogopa na hatima yake tumeona alikuja kutupwa katika giza la nje.

Aliogopa nini?

Aliogopa atakapojaribu kuifanyia biashara ataipoteza…aliogopa kupata hasara..hivyo akaona ni heri aihifadhi tu..mahali fulani mpaka Bwana wake atakaporudi amrudishie kilicho chake wamalizane..

Aliogopa kuchekwa, na kudharauliwa, na kudhihakiwa, alijiona hawezi kuzalisha kile alichopewa, hana uzoefu na biashara..hakutaka kujitosa kama wale wenzake…ambao wao pia waliijua hatari ya biashara kwamba kuna kupata na kupoteza, lakini hawakutaka kuzipa kipaumbele… lakini yeye akasema sitaki kupata magonjwa ya moyo..wacha niihifadhi tu..kwani nini! , maadamu sijamtapeli..akirudi nitamrudishia kilicho chake. Ndivyo hali ya watu wengi wanajihita wakristo ilivyo.

Na kama upo miongoni mwa watu hao, leo umesoma ujumbe huu kwasababu Bwana anakupenda hataki uende kutupwa katika giza la nje ambapo huko kuna kilio na kusaga meno.

Hivyo amua leo kuzama katika wokovu, acha kusita-sita maana muda uliobakia ni mfupi sana, Bwana yupo karibu kuliko watu wanavyodhania. Ni siku yoyote, saa yoyote parapanda ya mwisho italia, jiulize utakuwa wapi? Na hata kama Bwana hatarudi leo, au mwezi ujao, je wewe usipofika kesho? Jiulize utaenda kuwa mgeni wa nani na umesikia injili vya kutosha.

Hebu amua kumpa Yesu maisha sasa kikamilifu kabla hujachelewa, acha dhambi zote, acha ulimwengu, acha uvuguvugu, amua kuchoma kabisa mavazi ya kiulimwengu kama hizo vimini, vitop, masuruali, na hayo mawigi, mahereni, mabangili, mekaups, ondoa na hiyo rangi mdomoni na kwenye kucha zako maana ni machukizo kwa Mungu, futa picha zote na filamu za ngono kwenye simu yako, futa miziki ya kidunia zote, futa makala yote ya kizinzi,  makundi yote ya kihuni yafute yote, kamari na magemu yote ya kishetani futa usiache hata moja, mali za watu ulizotapeli rudisha mara moja, mke/mume wa mtu rudisha na uombe rehema, na mambo yote mabaya unaacha pasipo kusita-sita, na baada ya hapo unaenda kubatizwa.

Na kumbuka sio ubatizo tu ilimradi, unapaswa kubatizwa ule ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na Kwa jina la Bwana Yesu Kristo sawa na maandiko. Baada ya hapo unaendelea kuishi maisha masafi na kujitenga na ulimwengu, huku ukifanya kazi ya Mungu (kuhubiri Injili), na kushirikiana na watakatifu wenzako.

Bwana akubariki sana kwa maamuzi sahihi uliyoamua leo kuchukua… hakika hautawahi kujutia milele.

Shalom

Washirikishena wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *