Mungu amewekeza kitu kwako je! Unakitumiaje?.
Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Kila mmoja mmoja wetu pale tu anapookoka Mungu anawekeza kitu ndani yako ambacho Mwisho wa siku anatarajia kiongezeke zaidi ya vile alivyokiweka kwa mara ya kwanza. Na ni jukumu lako kuhakikisha kinaongezeka.
Kama vile muwekezaji yeyote yule hawekezi ili kile kitu alichokiwekeza kibaki vile vile bali anatarajia kitu hicho kiongezeke zaidi siku baada ya siku na kikiwa hakiongezeki kinabaki vile vile ni rahisi sana muwekezaji huyo kusitisha kuendelea kuwekeza.
Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu wetu kuna vitu anaviwekeza kwetu na matarajio yake ni kuona vinaongezeka.
Sasa kama wewe ni Msomaji wa Biblia mzuri katika Mathayo sura ya 25 yote inazungumzia sana hasa ufalme wa mbinguni kwa kuufananisha na mifano dhahiri ili watu aliokuwa akizungumza nao wakati ule hata sasa tuweze kumuelewa.
Katika habari hii tunaona Mtu mmoja aliekuwa anataka kusafiri aliwaita watumwa wake(wafanyakazi) yaani watu aliokuwa nao karibu anawaamini(watu waliookoka) akawapa kila mmoja taranta na kisha akaondoka. Hebu tusome habari hii lipo jambo tutajifunza hapa..
Mathayo 25″14 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.”
15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.
Ukisoma kwa makini hapo utona kama Kuna upendeleo fulani kwa nini huyu apewe tano mwingine mbili na Mwingine moja? Kwa namna ya kawaida tunaweza kuona mwenye kupewa moja alionewa au alikuwa haaminiki.. la haikuwa hivyo.
Turudi mstari wa 15b hapo anasema. “…..KILA MTU KWA KADIRI YA UWEZO WAKE;akasafiri”
Kumbe kila mmoja alipewa taranta kwa kadiri ya uwezo wake yeye mwenyewe.. hivyo mtu huyu alikuwa anajua uwezo wa watumwa wake vyema.
“Mungu siku zote hakupi kitu kilicho nje ya uwezo wako ambacho utashindwa kukimudu” hii ni siri kubwa sana na ni lazima tufahamu hili..
Hivyo Mungu anapokupa kitu anategemea kwamba unaweza kukimudu na anatarajia kama unaweza kukimudu basi ukizalishe zaidi.
Sasa je! hicho kitu ulichopewa unakitumiaje? Je! Unakizalisha au umekichimbia chini ya ardhi (jibu unalo wewe).
Kumbuka atakapokuja atakuja kutaka kujua umefikia wapi atataka hesabu yake umefanyia nini na umezalisha nini?
Kama mtu huyu alivyorudi aliketi na watumwa wake wote na kutaka hesabu kutoka kwao tusome…
Mathayo 25 “16 Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.”
17 Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.
18 Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
19 Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
20 Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako
.22 Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.
23 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
24 Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;
25 basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.
26 Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.28 Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
29 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.
30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Unaona hapo kwenye mstari wa 19 Baada ya siku nyingi mtu huyo alitaka hesabu nao watumwa wake.
Ukweli ni kwamba kila mtu anakitu cha kipekee kwa ajili ya kanisa(mwili wa Kristo) kuujenga na kwa ulimwengu pia.
Kanisa linahitaji hicho kitu kilichowekwa ndani yako ili liweze kusaidika na ulimwengu unahitaji vivyo hivyo ili uweze kusaidika kumbuka wewe ni kiungo muhimu katika mwili wa Kristo na ni nuru na chumvi ya ulimwengu.
Fahamu hili vyema kuanzia leo “ haupo kwa bahati mbaya hapa duniani upo kwa kusudi maalumu na inakupasa ulitimilize wala hakuna anaweza kulitimiza ila wewe mwenyewe “
Hivyo unaposhindwa kanisa halitasaidika katika sehemu fulani na ulimwengu vivyo hivyo(anza kuishi kwa kuitambua thamani yako katika Kristo Yesu). Unapokuwa mlegevu utakuwa kama mzingo katika pande zote katika kanisa na ktika ulimwengu.
Yaani utakuwa huna faida yoyote katika kanisa na kwa ulimwengu pia.
Ni nini tunahitaji kufahamu zaidi juu ya habari hii na inatupasa tufanye nini?
1.Mungu anachotaka kuona kwetu tunazaa na kuongezeka.
Mungu anatamani kuona kile alichokiweka ndani yetu kinafanyika msaada kwa wengine lakini na sisi pia tunapiga hatua hatubaki vile vile kama tusipozaa na kuongezeka ipo hatari kubwa sana kunyang’anywa kile tulichopewa.
Mathayo 25:29”Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”
Lakini maandiko yanaendelea kusema..
Mathayo 7:19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
Hivyo kuzaa matunda mazuri(kuhubiri injili na matunda ya haki kama vile wema,saburi upendo nk).
2.Pasipo kuchukua hatua hatuwezi kuzalisha chochote katika ufalme wa Mungu.
Tukiwa ni watu wa kusubiri subiri majira yafike hakika majira hayo hayatafika.. na katika roho utaonekana ni mtu mlegevu.
Mathayo 25:26 “Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;”
3.Kuwa mwaminifu katika kile ulichokipokea(karama/neema).
Kumbuka tumeaminiwa na kupendwa sana na Yesu Kristo na tunapokea neema ya uwezesho wa ajabu mno. Ili vitu vidharike kwetu tunahitaji sana kuwa ni waaminifu..
“Mazingira yatatwambia tunapoteza muda na hakuna tunachokifanya” lakini uhalisia hatupotezi muda. Hivyo tunapokuwa waaminifu katika vidogo ndio tunazidi kupandishwa taraja na kuwekwa katika mambo makubwa.
4.ulichopewa kiko ndani ya uwezo wako.
Kumbuka Mungu siku zote anawekeza karama mbali mbali ndani ya kila mmoja mmoja ambavyo vyote kwa pamoja tunaweza kuvimudu kabisa. Kitu pekee ambacho tunatakiwa sisi ni kukifanyia kazi tu.
Na ukweli ni kwamba kila mmoja wetu kapewa kiwango cha neema cha kuweza kutimiliza uwekezaji wa Mungu uwe na matunda ndani yetu. Acha kuwa mlegevu hubiri,Soma neno, taka sana karama za rohoni, jifunze unyenyekevu,upole,kiasi hivi vyote tumepewa ndani yetu ili vidhirike tunahitaji sana kufanyia kazi.
Maandiko yanaposema tutakula kwa jasho mara nyingi sana Tafsiri inayokuja ni katika mambo ya mwilini ukweli ni kwamba Mungu hakuwa anazungumzia mambo ya mwilini ila rohoni na kukawa na madhirisho katika mwili.. Mungu hakuwa busy na kulaani ardhi sivyo. Hii ni siri kubwa ambayo utaifahamu kwa sehemu na kadiri Mungu atakavyozidi kutupa neema tutajifunza juu ya hili katika somo lake..
Lakini nachotaka ufahamu hapa ni kwamba Mungu alikuwa anamaanisha hasa kwa mambo ya Rohoni hebu tutafakari kwa ufupi sana jambo hili naimani utanielewa vizuri..
Kipindi Adamu na Hawa hawajaasi utaona Mungu mwenyewe alikuwa akiwafuata pale bustanini kuwafundisha yaani walikuwa wanapata chakula cha rohoni bure kabisa kabisa. Hawakuwa wanasumbuka na kuomba,kufunga,nk lakini baada ya kuasi mambo yalibadilika ikabidi sisi sasa tuanze kuchukua hatua ya kumtafuta Mungu kwa njia mbali mbali. Utaona hata uzao wa Adamu baada ya Habili yaani Sethi walianza kutafuta ni kwa namna gani Mungu watamuona??
Wakaanza kubuni mambo kama ibada nk hivyo mambo ya rohoni kwa sasa yanapatikana kwa nguvu na ndio maana Bwana Yesu mwenyewe anasema..
Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.“
Hivyo ukiwa ni mlegevu katika mambo ya rohoni hakika hutaupata ufalme wa mbinguni!! Na ufalme wa mbinguni ni nini hasa? Ni wewe kumuelewa Yesu Kristo na kufahamu haki uliyonayo katika Kristo Yesu na mamlaka uliyonayo na nguvu ulizonazo na kuwa na uhakika wewe kuingia katika umilele baada ya maisha haya.
Hivyo kusudia kuanza mwaka huu na nguvu nyingi kwa kujikana kweli kweli ili kile alichokiweka Mungu ndani yako kizae matunda.
Ubarikiwe sana.
Mawasiliano: 0613079530.
@Nuru ya upendo.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.