Shalom, tunamshukuru Bwana kwa siku nyingine tena aliyotupa..
Wengi wetu tumekuwa tukiomba sana , wengine wameenda mbali zaidi wakiisindikiza maombi yao kwa mifungo ya siku hata mwezi, jambo ambalo ni jema sana na lapendeza sana mbele za Mungu, kwasababu maandiko yametutaka tuombe bila kukata tamaa, (luka 18:1)
Lakini leo natamani tujifunze Jambo lingine ambalo Katika hilo litakuongezea wigo mpana kwenye maombi yako au wakati wa kuomba, kwa kuomba kila mmoja anaomba lakini shida inakuja pale ambapo unaomba huoni matokeo ya kile unachokiomba au huoni mwitikio wowote..
Lakini kabla ya kuendelea mbele zaidi lazima ufahamu nini maana ya maombi, maana yake kama usipoweza kujua maana ya maombi unaweza usielewe umuhimu wa maombi,
Maombi ni mawasiliano kati ya Mungu na mwanadamu/ mwamini kwa njia ya imani, AU ni sehemu maalumu ya utulivu ya kufanya ushirika ulio bora na imara kati ya mwamini na Mungu..
Kama ni sehemu ya mawasiliano basi kumbe yakupasa uhakikishe mtandao hausumbui sumbui,au haukwami kwami ili kukufanya usiisikie sauti ya yule unayewasiliana naye, kwa neema za Bwana tutaangalia aina za maombi,na kwa kujifunza hilo tutapiga hatua zaidi katika kuomba kwetu..
Maombi yameganyika Katika sehemu mbili
1) MAOMBI YASIYO NA MATOKEO
Haya yanakuwa ni maombi lakini mwisho wake unakuwa hakuna matokeo yoyote, unaomba kweli, na sio kwamba Mungu hayasikii maombi unayoomba, anasikia, kwasababu hakuna neno la mwamini linalopita bure mbele zake, lakini zipo zipo sababu zinazopelekea maombi yako kukosa Nguvu,au kutokuwa na hoja za msingi kwa Mungu zinazofanya maombi kutokuwa na matokeo..
Na leo tutaangalia sababu zinazofanya maombi kutokuwa na matokeo..
• Kukosekana utulivu kwenye fahamu/fikra zetu
Hili ni jambo la msingi sana wewe kama mwamini unalopaswa kulizingatia unapokuwa kwenye Maombi/kuomba, wengi wamekuwa kwenye maombi lakini kiuhalisia fahamu zao hazipo hapo, yupo kimwili anaomba,ananena kwa lugha,analia na kuomboleza lakini fikra zake ziko nyumbani kwao huko iringa anafikiria mashamba yake aliyoyaacha, sasa kwa namna kama hii usidhani utaona uwepo wowote wa kimaombi, asilimia kubwa ya fikra au ufahamu upo kwa mwanadamu mwenyewe ni asili yake ndani yake, wala sio shetani ijapokuwa anashinikiza pale ambapo amepata nafasi,
Asilimia kubwa ya maombi yenye matokeo yanahitaji utulivu wa kifikra na ufahamu wako kiujumla, lazima akili yako ikubaliane na kile unachokiomba, lazima uelekeze ufahamu wote Katika maombi, lakini ukiona upo kwenye maombi ila ufahamu,upo jikoni,mana umeenda sokoni,mara ufahamu unaanza kukumbusha mambo yaliyopita, jua kabisa hayo ni maombi yasiyo na matokeo,utaomba adi asubuhi lakini hutaona chochote..
1 Wakorintho 14:14
[14]Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.
• Kuomba kwa tamaa ili vitumike kwa anasa
Maandiko yanasema,
Yakobo 4:3
[3]Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.
Sababu nyingine itakayofanya maombi yako yasiwe na matokeo hi hiyo, unaomba lakini kuomba kwako ni ili uvitumie kwa mapenzi yako mwenyewe, lengo la Mungu ni kuona nia yako Katika hicho unachotamani ukipate unakitumiaje,
wengi wanaomba wafanikishwe kwenye kazi zao za mikono lakini wanashangaa hawaoni mabadiliko kwa miaka mingi lakini kumbe uhalisia unatamani ufanikishwe ili ukatumie wewe mwenyewe na nafsi yako,mana yake unaiona nafsi yako ni bora zaidi inahitaji kushibishwa mema kuliko ya mwingine, nia ya Mungu unapomuomba baraka anatamani kuona ndani yako unatamani kuwabariki na wengine kupitia baraka hizo hizo unazomuomba,
Na maombi kama hayo huwa hayaleti matokea yoyote,na hutaona chochote kikibalika ijapokuwa Mungu hatakunyima rizki ila kuongezewa itakuchukua muda pasipo kuijua kanuni..
Wafilipi 2:3-4
[3]Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.
[4]Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.
• Kutokuwa na uvumilivu wa kumngoja Bwana
Tunda la uvumilivu linahitaji sana sio tu kimwili hata kiroho, uvumilivu wa kumngoja Bwana unahitaji sana kwa mwamini yeyote anayemwomba Bwana, zaidi uwapo kwenye maombi kuna wakati unafika huoni uwepo wowote wa kimaombi ndani yako,au hujisikii hali yoyote ya maombi sasa sio wakati wa kuhairisha maombi na kusema Bwana hayupo na mimi wakati huu, Hapana,bali hapo hapo unaendelea kumngoja Bwana, maana yake usipoonyesha uvumilivu fahamu kabisa mwisho wake utakuwa umeomba kidogo lakini umeomba maombi yasiyokuletea majibu yoyote,
Habari ya Elia tunaisoma,ijapokuwa hakuona dalili zozote za mvua kunyesha lakini aliendelea kumngoja Bwana kwa kuendelea kuomba Mpaka akaona matokeo ya alichokuwa anakiombea..
1 Wafalme 18:41,43-44
[41]Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.
[43]Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.
[44]Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.
2) MAOMBI YENYE MATOKEO
Ili uyafurahie Maombi yako ni pale utakapoona yanakuletea matokeo au majibu zaidi hata ya vile ulivyoomba, Maana yake ili uone matokeo basi vigeuze hivyo Vipengele viwe tofauti,kama ni mtu wa maombi basi hakikisha akili yako, fahamu zako na fikra zinakuwa kwenye kuomba,zilazimishe zikutii, kwasababu tuna nguvu za kutiisha kila fikra ikutii wewe, hakikisha unaomba lakini unatamani na wengine wabarikiwe kupitia wewe,usiijali nafsi yako tu,jali na za wengine,na cha mwisho kuwa mtu wa kumngoja Bwana uwapo kwenye maombi,tunda la uvumilivu liwe ndani yako upelekapo maombi mbele za Bwana Yesu..
Kwa kufanya Hayo,utayafurahia maombi yako na utazidi kumfarahia Mungu kwa jinsi anavyozidi kutenda sawa sawa na umuombayo..
Mathayo 6:32
[32]Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.