Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Katika kitabu cha Yona sura kwanza kabisa tunaona neno la Mungu linamjia Yona na kumwambia aende Ninawi akauhubirie mji ule uache uovu wake yaani watu wa mji ule watubu wamrudie Mungu. Lakini Yona hakufanya hivyo. Matokeo yake akakimbilia kwenda tarshihi na asiende Ninawi.
Yona 1
2 Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.
3 Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana.
Hivyo Yona hakuwa Tayari kumsikiliza Bwana katika kile alichomwambia.. akafata akili zake na matamanio yake ni yapi akaona ni Heri akimbilie Tarshishi sehemu ambayo ulikuwa ni mji wa kibiashara zamani zile wa watu wanaitwa Wafoinike. ili akakae huko aendelee na mambo yake lakini haikufanikiwa kwani kama tunavyoona katika mistari inayoendelea hapo Mungu akatuma upepo mkali na merikebu aliokuwa amepanda ikawa karibu kuvunjika.
Hivyo habari nzima tunaifahamu ikiwa huifahamu basi ni vizuri zaidi.. Bwana akitupa neema tutakichambua kitabu cha Yona na kujifunza yalimo humo.
Sasa maandiko yanaposema “akakimbilia Tarshishi apate kujiepusha na uso wa Mungu”
Maana yake Yona hakuhitaji tena kuendelea kumtumikia Bwana. Yaani hakutaka tena kuwa ni nabii wa Mungu wala hakutaka tena kuendelea kuwa ni mtumishi wa Mungu. Bali aliona ni heri akafanye mambo yake kivyake huko asimtumikie Mungu tena.
Ni kitu gani tunajifunza katika habari hii fupi?.
Hiyo inatufundisha pia sisi tuliookoka na kumwamini Yesu Kristo tusijiepushe na uso wake.. hapa ni kwa watumishi wote pamoja na wote tuliomwamini Yesu Kristo.
Hapa tunaona baada ya Yona kukimbilia Tarshishi dhoruba na tufani vilimpata ikawa karibu hata wapoteze maisha yao wote waliokuwa kwenye merikebu ile.
Unapofikilia kuacha kumtumikia Mungu (yaani kurudi duniani na kuacha wokovu) ndugu Shetani yupo na amekuandalia boti inakusubilia. Utakwenda katika boti hiyo utapanda ambapo mwanzo utakuwa ni mzuri kabisa utaona kumtumikia kule ulikuwa unapoteza Muda kukaa kwenye wokovu mara maombi nk utaona ulikuwa unafanya kazi bure.
Utaona chaguo ulilolifanya ni sahihi na utajikuta unalala kabisa usingizi mzuri katika boti hiyo lakini muda sio mrefu utaanza kuona madhara yake tufani zitakukuta na Shetani atakutumikisha na kukuharibu vya kutosha maana upo katika mikono yake.
Hii inatuonyesha/kutufundisha kuwa hakuna mtu yeyote ambae anatoka mbele za uso wa Bwana na akapata kuwa salama au kuwa na Amani. Bali ni amani na furaha ya kitambo kudogo sana kisha baada ya hapo ni mateso makubwa mno.
Ndugu ikiwa unaanza kuona wokovu ni mzito unaona wokovu huo unakuzuia kupokea rushwa,kuzini,kukosa mambo mazuri ya ulimwengu huu na ukaona utoke katika wokovu ufanye hayo yote.. ndugu itakuchukua muda kidogo sana utaona hayo ndio maisha lakini utayaona madhara yake muda si mrefu siku zote ulimwengu unavutia ukiwa mbali lakini ukiingia hauvutii unatisha mno.
Tulia kwa Mungu muamini Mungu katika nyakati zote na majira yote tulia na Mungu. Umekosa,umepata isikufanye uende mbali na Mungu. Kwa Mungu ndio kuna usalama wa maisha yako huko kwingine wamejaa wadanganyifu na wauwaji(Shetani na jeshi lake).
Wala hutaweza kuwashinda kwa nguvu zako mwenyewe.
Shetani siku zote anaonekana kama rafiki kwako anakuja kwa namna ambayo huwezi ukaona kama anaweza kukuangamiza kabisa.
1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”
Unaona hapo? Shetani anatafuta mtu wa kummeza yaani kuondosha uhai kabisa. Na huyo ni mtu anaekimbilia Tarshishi.
Ndugu usifadhaike na kuwaza sana kuwa muda unakwenda huna hiki na hiki hujakamilisha mambo fulani kuwa mtulivu tembea na Mungu wakati na majira vitakapofika atakukamilishia yote maana unastahili.
Atakupa vyote. Usijaribu kutafuta furaha na amani nje ya Yesu Kristo. Nakuhakikishia kamwe hutaipata utateseka sana huko nje mwisho utapotea kabisa. Kuwa na kiasi katika mambo yote.
Huko nje iko furaha ya kitambo sana ambayo haina muda mrefu itageuka na kuwa matatizo makubwa kwako na utaishia kuangamia. Usifikiri kuacha au kupumzika kidogo katika safari yako ya wokovu unapoishiwa nguvu Bwana atakutia nguvu.
Utaendelea mbele zaidi maana yeye ndio alioianzisha safari anajua namna ya kuikamilisha sisi ni kuwa tayari tu kutembea nae.
Je umemwamini Yesu Kristo? Furaha yako na tumaini lako ni nini? Je ni hiyo kazi yako uliyonayo? Au mke ulienae au Mume na watoto ulionao? Ndugu haya yote hayana muda mrefu na hayawezi kukupa furaha na amani na hakikisho la maisha ya baadae ila awezae kukupa haya ni Yesu Kristo.
Amua leo kumpa Yesu Kristo maisha yako. Usipuuze kabisa injili kwani wakati mbaya unakaribia ambao hutaweza tena kuchukua maamuzi na utakakuwa umechelewa muda ni sasa geuka uache njia yako kama watu wa Ninawi walivyotubu na kumrudia Mungu akawarehemu na Mungu pia atakurehemu yeye ni mwingi wa Rehema na fadhili. Hakika anakupenda sana.
Yesu yuko Karibu kurudi je unauhakika wa kwenda nae.?
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.