Nini kinakutokea unapoenda kinyume na Nuru/Kweli.

Biblia kwa kina No Comments

Nini kinakutokea unapoenda kinyume na Nuru/Kweli.

Nakusalimu katika jina lipitalo majina yote, jina la Yesu Kristo wa Nazareth. Karibu tujifunze Neno la Mungu lililo taa na mwanga wa njia zetu.

Kama tunavyojua kazi mojawapo ya mwanga ni kutusaidia kuona hususani wakati wa usiku.

Lakini, je umewahi kutembea njiani ukakutana na mwanga mkali ukakumulika? Nini kilikutokea?

Bila shaka macho yako yaliumia, na ukashindwa kuona mbele, pengine ukamlalamikia huyo aliyekumulika, si ndiyo?

Hiyo ni kuonyesha kuwa mtu anapokwenda sambamba na nuru, anaona njia, lakini anapokwenda kinyume na ile nuru, ile nuru ikawa inamulika macho yake badala imulike huko anakokwenda..mtu huyo hataona tena njia, anakuwa kama kipofu.

Sasa, tukija katika roho, ni vivyo hivyo. Yesu Kristo ni nuru ya ulimwengu. Yeye mwenyewe alisema..

Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu”. (Yohana 9:5)

Hivyo basi, kama vile mwanga uwesavyo kutuonyesha njia..na pia uwesavyo kutupofusha pale tunapokwenda kinyume chake, ni vivyo hivyo, Kristo naye anatuonyesha njia ya uzima, lakini tukienda kinyume chake yaani kinyume na Neno lake..anatupofusha kwasababu yeye ni Nuru tena mkali. Unapoenda kinyume chake ni lazima tu upate upofu, ndicho kilichomtokea Paulo aliyeitwa Sauli kabla hajaokoka, alikuwa anaenda kinyume na kweli, alikuwa anawaua wakristo..na siku moja alipokuwa anaenda Dameski kuwauwa watakatifu, alikutana na mwanga mkali njiani ambayo ndiyo ile NURU HALISI akapofushwa macho, kwanini? Kwasababu alikuwa anaenda “opposite” kinyume na Nuru. Tunasoma..

Matendo ya Mitume 9:1 Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu,

[2]akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.

[3]Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.

[4]Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?

[5]Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.

[6]Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.

[7]Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.

[8]Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.

Umeona hapo, kinachomtokea mtu akienda kinyume na Nuru. Kristo alisema..

“…Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu”. (Yohana 9:39)

Wanaoona ni hao mfano wa Sauli ambaye alikuwa anaenda kinyume na kweli, na mwisho wake akawa kipofu na ndivyo alipoona baada ya kuwa kipofu, kwasababu wale wanaoona ni sharti wawe vipofu ndio waone.

Na hata leo, watu wanaoipinga injili ya kweli, watu wanaojiona wanajua sana na hawataki kusikia tena wala kubadilishwa na Neno, watu ambao wamebaki kushikilia udini na udhebebu. Hatima yao wanakuwa vipofu kwasababu wanaenda kinyume na Nuru, hivyo wasipokubali kujishusha na kuanguka chini (kutubu) kama alivyofanya Sauli watakuwa vipofu daima.

Matendo 22:7 Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?

[8]Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.

[9]Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami.

[10]NIKASEMA, NIFANYE NINI, BWANA? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.

Hebu na wewe leo, kubali kuweka ule Ufarisayo na udhebebu pembeni, na mwambie Bwana ”nifanye nini Bwana”. Bwana atakurudisha katika Neno lake alilolisema kwa kinywa cha Mtume Petro..

“..Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”. (Matendo 2:38).

Kwahiyo kama bado hujatubu kisawa sawa na hujabatizwa kwa usahihi, na hujapokea Roho Mtakatifu. Kanuni ni hiyo ”kutubu na kubatizwa kisha kupokea Roho Mtakatifu”

Na kutubu sio kuishia kumuomba Mungu msamaha! Hiyo inakuja baada ya toba ya kweli.

Kutubu ni kumaniasha kuacha dhambi na ulimwengu, maana yake unaamua kuacha dhambi zote kwa vitendo kabisa, kama ni uasherati unaacha kabisa kabisa..unafuta picha zote za ngono, unafuta makala yote ya uzinzi, unafuta namba za wazinzi wote yaani wanawake au wanaume ambao hamjafunganao ndoa ya halali, maboyfriends au magirlfriends wote futa namba zao au waambie umeamua kutubu na kuacha uasherati, na hivyo nao watubu. Unaacha mambo yote mabaya ..unaacha kamari, magemu, miziki ya kidunia zote unavuta kabisa, mapambo ya kidunia kama lipustick, mekaups, nywele bandia, kucha bandia, mahereni, n.k unatupia mbali kabisa, na mavazi yote ya kizinzi kama vile vimini zote, masuruali aina zote ikiwa we ni mwanamke, magauni yanayobana na nguo zote zinaonyesha maungo yako..unayachoma yote bila kuona aibu au kuonea huruma. Hiyo ndio maana ya kutubu na ndivyo watu walivyokuwa wanatubu walipokubali kupokea Nuru, Soma..

Matendo19:18 “Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.

[19]Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga WAKAKUSANYA VITABU VYAO, WAKAVICHOMA MOTO MBELE yai WATU WOTE; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu”.

Unaona hapo, watu walivichoma vitabu vyao vya uganga pasipo kujalisha ghrama waliyoingia. Leo hii Unaona ni gharama kubwa kuchoma hayo mawigi ulizonunua kwa bei ghali, hizo hereni na fashions za kidunia unaogopa kuvichoma, ni kwasababu bado unaenda kinyume na Nuru, bado hutaki kutubu. Nataka nikuambie leo usipokubali kutubu na kumpokea Yesu Kristo aliye nuru ya ulimwengu, tegemea kuwa kipofu, na siku zote kipofu akitembea gizani mwisho wake atatumbukia shimoni (kuzimu). Lakini leo ukinyenyekea..ukakubali kuanguka chini kama Sauli, yaani ukatubu kwa kumaanisha kuacha ulimwengu kabisa, basi Bwana atayaponya macho yako, nawe utageuzwa kuwa mtumishi na kupewa jina jipya kule mbinguni kama ilivyo kuwa kwa Paulo na sisi.

Hivyo usiendelee kuushikilia udini wala udhebebu.. ukasema dhehebu letu haliamini katika hayo, au ukasema imani yetu inaamini kuwa Mungu anaangalia roho, haangalii mwili, au tumekombolewa katika sheria na tunaishi katika neema, nataka nikuambie utakuwa umepotea sana ndugu yangu, Mungu anaangalia roho,nafsi na mwili, na tena neema ya Kristo inatufundisha kuukataa ubaya na udunia, Soma Tito 2:11-12.

Hivyo kubali kubadilika . usiendelee kwenda kinyume na kweli/Nuru maana utakuwa kipofu na mwisho utaishia jehanum ya moto usipotubu.

Tubu sasa, na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa jina la Yesu Kristo ili upokee Roho Mtakatifu atakayekusaidia kuishi maisha yanayompendezayo Mungu (utakatifu).

Kumbuka tunaishi ukingoni mwa nyakati na moja ya siku hizi Kristo anarudi kulichukua kanisa lake, je utakuwa wapi siku hiyo?

Bwana atusaidie tufanye maamuzi sahihi kabla hutujachelewa.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *