Nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.
Shalom; jina la Yesu Kristo libarikiwe.
Tunapomwamini Yesu Kristo na kuamua kumfuata kweli kweli tunafanyika kuwa watumwa wake, ndio maana tunamwita “Bwana”. Hivyo unapomwita kama Bwana, jiulize je umejiweka chini yake kama mtumwa?
Zifuatazo ni sifa za watumwa.
Wamejikana nafsi kweli kweli.Hakuna mtumwa yeyote anayekuwa na uhuru asilimia zote, muda wote utamkuta eneo la kazi..kitu kinachompa hofu kuliko yote ni kuipoteza kazi yake au kuiharibu, na kitu pekee kilichomuunganisha yeye na Bwana wake ni kazi yake hiyo aliyopewa, ya Injili. Huwezi kumkuta mtumwa aliye makini, muda wa kufanya kazi yupo anazurura!.. kadhalika watumwa wa Yesu, kwaajili ya Injili hawazururi zururi katika huu ulimwengu, shughuli shughuli na anasa za ulimwengu huu, zinawapita! Na wala hawazitamani.. macho yao ni kuifanya kazi ya Bwana na kuimaliza.. kuhubiri Injili kwao ni sharti! Sio ombi tena!
1Wakorintho 9:16 ” Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili.17 maana nikitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili”.
Watumwa wa Bwana waliojifunga nira ya Bwana, muda wote, masaa yote wapo katika mazingira ya kuifanya kazi ya Mungu. Mtume Paulo na wengine baadhi, walijitoa katika Injili kiasi kwamba hawakuwa na muda wa kutafuta wake, akili zao zote zilikuwa katika kuifanya kazi ya Mungu, mambo ya ulimwengu huu waliyaona kama mavi (Wafilipi 3:8).
Watu wengi wanadhani wakishaokoka tu kwa kumwamini Yesu imetosha! Hawajui kuwa mkristo aliyeokoka kweli kweli ni lazima afanye kazi ya Mungu (ahubiri Injili).
Bwana hajasema tu tuende kwake halafu tupumzishwe mizigo yetu baada ya hapo tusitarehe, hapana, alisema..
” Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 JITIENI NIRA YANGU, MJIFUNZE KWANGU, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 KWA MAANA NIRA YANGU NI LAINI, NA MZIGO WANGU NI MWEPESI”
Hapo hasemi kuwa tukishakwenda kwake ni kupumzishwa tu, basi na baada ya hapo hakuna kitakachoendelea..la! Hakusema hivyo, badala yake alisema “JITIENI NIRA YANGU” na tena anasema” mzigo wangu ni mwepesi “….Kumbe! Na yeye anayo nira!.. maana yake anatutoa kwenye utumwa mmoja na anataka kutuingiza kwenye utumwa mwingine!.. Tofauti ni kwamba nira yake yeye ni laini na pia mzigo wake ni mwepesi, na hili tunalidhibitisha pia kipindi kile wana wa Israeli walipomwasi Mungu na waliponyenyekea Bwana akawahurumia, lakini akawaambia..
2Mambo ya Nyakati 12:6 “Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israeli na mfalme; wakasema, BWANA ndiye mwenye haki.
[7]Naye BWANA alipoona ya kwamba wamejinyenyekeza, neno la BWANA likamjia Shemaya, kusema, Wamejinyenyekeza; sitawaharibu; lakini nitawapa wokovu punde, wala ghadhabu yangu haitamwagika juu ya Yerusalemu kwa mkono wa Shishaki.
[8] WALAKINI WATAMTUMIKIA; ILI WAPATE KUJUA UTUMWA WANGU, NA HUO UTUMWA WA FALME ZA NCHI.'”
Umeona hapo, maana ni hiyo hiyo ”nira ya Bwana ni laini, na mzigo wake ni mwepesi kuliko wa adui”.
Lakini pamoja na hayo hasemi kwamba ” yeye atatutia nira yake,baada ya kutufungua hiyo nira ya adui ” badala yake anasema ” JITIENI NIRA YANGU ” huo ni kama “Ushauri” na siyo “amri”. Ingekuwa ni amri angesema ” njooni kwangu nami nitawapa pumziko na kuwatia nira yangu “..hapo ingeweza kuwa amri, lakini mpaka anasema sisi ndiyo tujitie nira yake… huo ni uchaguzi!!.. maana yake ukipenda kuwa huru sawa, au ukipenda kuichukua NIRA mpya ya YESU KRISTO ni vizuri zaidi…
Sasa pengine unajiuliza nira ni nini,..nira ni kifungo Fulani ambacho mnyama kama ng’ombe anavikwa shingoni, kama nyenzo ya kuvuta mzigo ulio nyuma yake.. Tazama picha chini.

Kadhalika na Kristo naye anayo nira ambayo anawafunga watu wake wale ambao kwa mapenzi yao wameamua kujitia katika UTUMWA WAKE. Na wanapofungwa Nira hiyo, wanageuka kuwa WAFUNGWA. Maana yake wanakuwa ni wafungwa wa YESU kwa ajili ya Injili.
Swali ni Je wewe ni mfungwa wa Yesu?.. umejitia NIRA ya Bwana Yesu shingoni mwako?.. Au bado unayo nira ya adui shetani?..
Nira ya adui shetani ni ulevi unaoutumainia ambao unakufanya kuwa mtumwa wa pombe na singara!.. Nira ya shetani ni uzinzi na ukahaba unaoufanya ambao huwezi kuishi bila huo.. Nira ya adui shetani ni hizo mekaups, lipustiks, wanja, wigi, hereni, na nguo za aibu ambazo huwezi kutoka bila kujipodoa na kuvaa hizo nguo za utupu.
Nira ya adui shetani ni ushabiki wa mpira unaokufanya uwe mtumwa wa huo mpira.. Nira ya adui shetani ni tamaa zote za macho ambazo zimekufanya kuwa mtumwa..Nira hiyo huwezi kujivua mwenyewe, kwasababu aliyekufunga hukuwa na nia ya wewe kukuacha huru siku moja!
Hivyo huwezi kujifungua, unamhitaji Yesu azivunje!… ndipo uwe huru!… kwasababu kwa nguvu zako haiwezekani.. na baada ya kukufungua!, anakupa shauri la wewe kujitia nira yake!.. hapo siyo yeye anakufunga hiyo nira! Ni wewe ndio unayeamua kujifunga nira yake.. na kama ukitii na kukubali kumtumikia Yesu kwaajili ya Injili yake, na kuwa mfungwa wake.. yeye alisema maneno haya..
“..Amini,nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwaajili yangu,na kwaajili ya Injili, 30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, au ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Mathayo 10:28-30).
Kumbuka kama bado hujampokea Yesu, basi fahamu kuwa bado unayo nira ya adui shetani mwako, na upo kwenye utumwa wa dhambi hata kama hujijui, Hivyo mgeukie leo Kristo akuweke huru,Yeye mwenyewe alisema ” Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli ( Yohana 8:36)”,
Hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zako zote unazozitenda kwa siri na kwa wazi, na kisha tafuta ubatizo sahihi, ubatizwe kwaajili ya ondoleo la dhambi zako, ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu ( Matendo 2:38), Na baada ya hapo amua kujitia Nira ya Kristo, kwa kudhamiria kumtumikia yeye kwa gharama zozote zile, na Bwana mwenyewe atakufanya kuwa mtumwa wake.. na thawabu yako itakuwa kumbwa hapa duniani na utakapofika mbinguni.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.