Shukuruni kwa kila jambo.

Biblia kwa kina No Comments

Shukuruni kwa kila jambo

Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.!

Umewahi kufikiri kwa ni nini Maandiko yanatutaka tushukuru kwa kila jambo? Ni jambo ambalo si jepesi haswa pale unapopitia katika magumu si rahisi kushukuru kwa ajili ya hayo magumu.

Ni rahisi kumshukuru Mungu katika mazuri tu lakini katika magumu si rahisi inahitaji ufahamu na ukomavu kiroho kufanya hivyo.

Sasa kuna siri gani katika kushukuru kwa kila jambo? Tutatazama kwa kina kuna siri ipi na kama tukifahamu basi itakuwa ni rahisi kumtukuza Mungu hata katika magumu tunayoyapitia..

1 Wathesalonike 5:18
“shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”

Sasa ili kupata ufahamu zaidi wa mstari huu tusome kwenye Biblia ya kiingereza anasema….

1 Thessalonians 5:18
[18]Thank [God] in everything [no matter what the circumstances may be, be thankful and give thanks], for this is the will of God for you [who are] in Christ Jesus [the Revealer and Mediator of that will].

Maana yake..

1 Wathesalonike 5:18
[18]Mshukuruni [Mungu] kwa kila jambo [ hata hali ziweje, shukuruni na mushukuru] , kwa maana hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwenu [mlio] katika Kristo Yesu [Mfunuaji na Mpatanishi wa mapenzi hayo].

Unaona hapo!, kwamba hata hali iweje haijalishi ni mbaya kiasi gani,huoni mwisho,wakati mwingine unaelekea kupoteza tumaini kabisa lakini maandiko yanakwambia shukuru katika yote sasa ni kwa nini?.

Kwanza ni Muhimu kutambua hakuna jambo lolote liwe baya au zuri linalokupa ambalo Mungu hana taarifa nalo.

Kila jambo linalokupata aidha liwe zuri au baya maadamu unatembea katika mapenzi ya Mungu basi yeye anafahamu na si kufahamu tu anajua mpaka jinsi unavyojisikia anaelewa zaidi ya wewe unayeipitia hiyo hali.

Mathayo 10

29 Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu;

30 lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

31 Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

Hawa ni jamii ya ndege wadogo na ni wengi sana lakini Bwana Yesu anasema ndege hata mmoja kati ya hao akifa Mungu anafahamu ndege mmoja kama na kwa sababu gani! Hivyo anasema “ Msiogope; basi bora ninyi kuliko mashomoro wengi”

Maana yake Mungu anafahamu katika hali zote unazopitia na anataka umshukuru katika hizo..

Tutafakari mfano huu! Mzazi anaemuathibu mtoto wake pale anapokosea na kumuonya, na mtoto yule anapoathibiwa kimsingi anatakiwa amshukuru mzazi wake kwa kumuathibu lakini kwa sababu ya akili yake haijakomaa vyema ataona kama anaonewa na anachukiwa, na ukimwambia ashukuru kwa sababu ya adhabu hiyo ni wazi hatakuelewa atakuona kama kichaa na unamuonea na wewe ni katili.

Hata Wakati tunasoma pindi tulipokuwa tunafeli tulikuwa tunapigwa viboko nakumbuka tuliwahi kupigwa karibia na staff nzima kwa sababu tu tumefeli na tuliona kama ni uonevu na ukatili wa hali ya juu sana(hela tunatoa n bado tunapigwa nk). Lakini kumbe ilitupasa kuwashuru waalimu wale badala ya kuwafikiria vibaya.

Nakumbuka wakati fulani nikiwa day Primary nilikuwa nazuiliwa sana kuangalia TV wala kwenda kwenye mabanda umiza kwenda kuangalia mpira,  wakati fulani nilikuwa natoroka usiku saa4 naenda kuangalia mpira narudi saa 7 mpaka saa 8 siku moja nikapigwa sana nyumbani niliona nimefanyiwa ukatili sana.

Lakini kumbe ilinibidi nishukuru kwa sababu walikuwa wananiwazia mema na kunitengeneza niwe mtu bora siku zijazo na walikuwa wananiokoa na janga kubwa mno.

Vivyo hivyo unapoona unapita katika hali huielewi mshukuru Mungu,  kwani katika kushukuru utaugusa moyo wa Mungu na utafanikiwa kupata funzo litakalokusaidia katika nyakati zinazokuja.

Usianze kunung’unika Mungu kakuacha au hakuoni au ndio Mungu kakuchoka usifikili hivyo ukafanana na wana wa Israeli kumbuka Mungu anakuwazia mawazo yaliyo mema(kukosa moyo wa shukrani kunaleta manung’uniko nk)..

Yeremia 29:11
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Ukilifahamu hili kuwa Mungu anakuwazia Mema hutapata muda wa kunung’unika badala yake utamshukuru.

Na ukweli ni kwamba Shukuruni zinaweza kukutia nguvu isiyokuwa ya kawaida hasa pale unapopita katika magumu.  Shukuruni ni kitu kinachoweza kukupa amani ya kutosha katika moyo wako katika nyakati mbaya.  Shukuruni ni kitu kinachoweza kukupa tumaini mahali ambapo unaona tumaini hakuna. Na unapomshukuru Mungu unavuta uwepo wake karibu sana na msaada wake pia.

Ni kitu kinachokupa tumaini la hakika kwamba Mungu yupo pamoja na wewe siku zote na nyakati zote.

Ukianza kunung’unika lazima utaona Mungu yuko mbali na wewe na hakuoni kabisa nk.

Maandiko yanasema..

1 Wathesalonike 5:16
“Furahini siku zote;”

Utawezaje kufurahi siku zote ikiwa si mtu wa kushukuru kwa kila jambo? Andiko hili linatimia kwako ikiwa utaanza kujifunza kumshukuru Mungu.

Unapokuwa katika hali ambayo si nzuri Mshukuru Bwana kwani hakutesi bali anakuimalisha na kukufundisha jambo ambalo ni kwa faida yako na wengine pia.

Warumi 12:12
“kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki , mkisubiri; katika kusali, mkidumu;”

Unaona hapo? Kwa tumaini mkifurahi katik dhiki, kumbe inatupasa kufurahi na kushangilia katika dhiki maana kazi ya dhiki huleta saburi.

Huwezi kufurahia katika dhiki ikiwa si mtu wa Shukrani lazima utalalamika tu.

Warumi 5

3 Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;4 na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;”Dhiki kwa Mkristo wa kweli ni kitu kinachomsogeza karibu na Mungu na ni faida kwa Mkristo “

Yapo maandiko mengi sana ambayo yanatupa sababu za kushukuru kwa kila jambo. Maadamu tunatembea katika mapenzi ya Mungu mambo mengi mabaya yatakuja ikwa kweli umesimama imara na dhabiti lakini katika hayo Mshukuru Mungu mandiko yanasema heri(amebarikiwa/kubarikiwa)

2 Timotheo 3:12  Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.

Lakini maandiko yanasema tena.

1 Petro 4:14  Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.

Hivyo hupiti katika dhiki kwa Bahati mbaya bali ni mapenzi ya Mungu wewe upite katika hayo na Mshukuru Mungu na endelea mbele..

Omba maombi haya kwa imani.…!

Eee Mungu ninaomba unipe moyo wa kukushukuru katika nyakati zote mbaya na nzuri,uniondolee manung’uniko, nipe moyo wa kukushukuru na kinywa cha kukutukuza katika majira yote na nyakati zote, nipe moyo unaobubujika shukrani muda wote, Asante Baba kwa kuwa unanisikia,Asante Baba kwa kuwa unanipenda,Asante Baba kwa kuwa unanijali na kuniwazia mema ni katika Jina la Yesu Kristo Amen .”

Ubarikiwe sana.

Mawasiliano 0613079530.

@Nuru ya upendo.

 

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *