SISI NI SHAMBA LA BWANA

Biblia kwa kina No Comments

SISI NI SHAMBA LA BWANA.

Isaya 5:7 “Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza;..”

Ikiwa umemwani Yesu Kristo na ukaamua kutubu dhambi na kumfuata kwa gharama zote.. basi fahamu kuwa we ni shamba lake.

Na kama we ni shamba la Bwana, unapaswa kujitathimi kila mara ni matunda gani yanatoka kwako.

Kumbuka siku zote mtu asipowajibika mwenyewe kusafisha shamba lake, na kuhakikisha, anayatoa yale yasiyostahili, au analipalilia mara kwa mara, ajue kuwa ataangukia hasara, na mwisho wa siku kazi yake inakuwa bure. Sikuzote kazi nzito ya ukulima ipo katika kupalilia na kulitunza shamba, dhiki ya wavamizi, na magugu, na sio katika kupanda. Kwasababu kupanda kunaweza kuchukua siku moja au mbili basi. Lakini kulitunza shamba ni jambo lingine, linalomgharimu mkulima, kila siku awe anaamka asubuhi na mapema, na mara kwa mara kulitembelea shamba lake, kulitazama na kulipalilia.

Akiwa ni mkulima mvivu shamba lake litamea miiba na magugu na mwisho itakuwa ni hasara kwake.

Mithali 4:30-34 inasema..

30 “Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

31 KUMBE! LOTE PIA LIMEMEA MIIBA; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.

32 Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.

33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!

34 Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang’anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha”.

Ukishaokoka, tayari we ni shamba la Mungu. Hivyo kuanzia huo wakati huna budi kuanza kujisafisha ili uruhusu mbegu njema zimee ndani yako uweze kutoa mazao mengi kwa Kristo.

Hivyo tunajisafisha kwa kusali kila siku, kutafakari maneno ya uzima, kujitenga na uovu, kuomba na kufunga, na kujizuia sana na mambo ya kidunia. Tukizingatia haya kila siku. Basi mbegu halisi za Mungu zitamea ndani yetu. Na matokeo yake tutakuja kutoa mazao mengi kwa Mungu na tutapokea dhawabu kubwa tukifika kule juu.

Hivyo tusiwe watu, wa kukumbushwa kumbushwa habari za maisha yetu ya kiroho, tuamke usingizini, tuondoe uvivu, tukayatazame mashamba yetu kila siku. Anza sasa kuwajibika kupalilia shamba lako, usiruhusu mbegu za ibilisi zimee ndani yako kama mawazo mabaya, uchungu, hasira, wivu, matusi, kiburi, uzinzi n.k hizi zote unazizuia kwa kuwa mtu wa maombi, kusoma Neno, kujitenga na vyanzo vya mambo hayo mabaya.

1 Wakorintho 3:9;”Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu”.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *