TABIA NYINGINE YA IBILISI UNAYOPASWA KUIFAHAMU.

  Siku za Mwisho, Uncategorized

ANACHANGANYA KWA PAMOJA UKWELI NA UONGO, AU ANASEMA UKWELI NA UONGO (KWA LENGO LA KUPOTOSHA)

Ipo tabia nyingine ya ibilisi ambayo wewe kama mtu unayejitoa sadaka kila siku ili kumtii Mungu (wewe unayajitahidi kumpendeza Mungu katika Kristo), unapaswa kuifahamu, kwa sababu maandiko yanasema kuwa, bilisi ameshatangaza vita na watu kama hao kuhakikisha anawaangusha (Ufunuo 12:17), hivyo basi, huna budi kuzijua tabia zake ili asipate nafasi ya kutushinda kama mtume Paulo alivyoandika katika.

2 Wakorinto 2:11 Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake. 

Na tabia hiyo ya ibilisi ambayo unayopaswa kuifahamu ni kuwa, ibilisi huwa anachanganya ukweli na uongo (anasema ukweli na uongo kwa pamoja kwa lengo la kupotosha). 

Wewe kama mkristo, unapaswa kutambua kuwa, si kila muda ibilisi atakuja kwako kwa vitisho, au si kila muda atakuja kwa kukutamanisha vitu vizuri kama fursa, kazi, utajiri, pesa, umaarufu, uongozi au nafasi mbali mbali na vyeo, hapana! Bali wakati mwengine atakuja na maneno ya kweli kabisa ya Mungu ili kusudi akunase katika mtego wake na kukufanya mateka wake, mfano mzuri ni pale alipomnasa Mwanamke wa kwanza Hawa, alimwendea na kumwambia maneno ya kweli kabisa ya Mungu (Mwanzo 3:1) na kuchanganya na uongo kwa lengo la kumpoteza.

Pengine ni pale alipokuwa akimjaribu Bwana kule jangwani, alipoona ameshindwa kumnasa kwenye mali na vyeo, alimjaribu tena kwa maneno ya maandiko matakatifu kabisa ya Mungu (lakini ni kwa lengo la kumpotosha).

Luka 4:9 Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini 

10 KWA MAANA IMEANDIKWAATAKUAGIZIA MALAIKA ZAKE WAKULINDE

11 NA YA KWAMBAMIKONONI MWAO WATAKUCHUKUAUSIJE UKAJIKWAA MGUU WAKO KATIKA JIWE

Na maandiko hayo ya Roho, ibilisi aliyatoa katika chuo cha Zaburi (soma Zaburi ya 91).

Hivyo ni tabia yake hiyo ibilisi pia kutumia maandiko na kuchanganya na uongo (kusema ukweli na uongo kwa lengo la kumpotosha mtu).

Sasa Inawezekana mimi na wewe tusipate nafasi ya kuhojiona na kujibizana na ibilisi moja kwa moja kama ilivyokuwa kwa Bwana au kwa Mwanamke wa kwanza kuumbwa (Hawa), lakini unapaswa kuifahamu tabia hii ya ibilisi ya kuzungumza ukweli na uongo pamoja kwa lengo la kupotosha watu, na ya kwamba, TABIA HII BADO ANAITUMIA HATA SASA KUWAPOTOSHWA WENGI nyakati hizi za sasa, kwa sababu maandiko yanasema

2 Wathesalonike 2:7 MAANA ILE SIRI YA KUASI HIVI SASA INATENDA KAZI; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. 

Sasa utauliza ni kivipi ibilisi anasema uongo na ukweli na wakati wewe binafsi hujawahi msikia na wala kuhojiana nae moja kwa moja Kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo?

Jibu ni kwamba, anaitumia tabia hii kupitia  watumishi wake wa uongo ambao ni wana wa kuasi kama yeye alivyo muasi.

Waefeso 2:2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule ATENDAYE KAZI KATIKA WANA WA KUASI

Ambao Watakuhubiria Roho Mtakatifu (ukweli), lakini watakwambia kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo sio lazima (uongo). Watakuhubiria uwe mtakatifu (ukweli), lakini kamwe hawatokwambia kuwa hivyo vimini vyako na visuruali vyako mwanamke unavyovaa si sawa mbele za Mungu (vitakupeleka Jehanam). 

Watakwambia Kristo anaponya na kuokoa, njoo kwa Yesu Kristo, mwamini Mwana wa Mungu, na huku watakwambia Mungu hawezi wahukumu wanadamu aliowaumba kwenye moto wa milele.

Watamtaja Kristo katika nyimbo zao za injili, kwamba Kristo anaweza, hakuna mwengine kama Yeye, lakini midundo wanayoitumia kumsifu Mungu katika nyimbo zao haina utofauti na ile ya kidunia. Watakwambia tunaishi katika siku za mwisho, Kristo yupo mlangoni (ukweli), lakini watakufundisha kukataa kushika maagizo yake kama vile wanawake kufunika vichwa vyao wakati wa ibada, kushiriki meza ya Bwana, kutawadhana miguu, n.k. 

Watakuhubiria amri ya upendo (ukweli), lakini watakwambia kuliinamia na kulisujudia sanamu la Mariamu, Yesu , au ng’ombe si dhambi. Watakuhubiria kuwasamehe wengine makosa yao (ukweli), lakini watakwambia kuwaomba watu waliokufa (wafu) sio dhambi. 

Ndugu mpendwa, unapoona tabia kama hiyo au Injili kama hiyo, kwa baadhi ya watu, basi tambua kuwa ni ibilisi anahubiri kupitia watumishi wake aliowadanganya (wawe wanafahamu au hawafahamu), hivyo kuwa makini na uchukue tahadhari, 

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.


Mada zinginezo:

Je! Ni kweli mshahara wa dhambi ni mauti na si moto wa milele?


KWANINI BIBLIA INAMFANANISHA IBILISI NA SIMBA ANGURUMAYE?


Je! Tunapaswa kumuombea Shetani na Malaika zake msamaha kwa Mungu wakiwa kama adui zetu namba moja?


Ni hukumu ipi ya Ibilisi inayozungumziwa katika Waraka wa (1 Timotheo 3:6?)


Kwanini Kuzimu kuongeze tamaa yake na kufunua kinywa chake bila kiasi? (Isaya 5:14).


Je! Ni dhambi kibiblia kuwaomba wafu (watakatifu)?

One Reply to “TABIA NYINGINE YA IBILISI UNAYOPASWA KUIFAHAMU.”

  • katika makanisa yetu ya mahali, akuna desturi hio ya kutafadhana miguu, je jambo hilo linaweza kumzuiya mtu kufika mbinguni?

LEAVE A COMMENT