thamini maisha ya kiroho ya mwanao tangu utotoni

Watoto No Comments

Bwana Yesu asifiwe milele yote, karibu tuyatafakari Maneno yake..

Usalama wa maisha ya mtoto yapo kwa Mungu lakini pia yapo kwa mzazi, ni jukumu la mzazi kuyajali na kuyathamini maisha ya mtoto hata kabla hajazaliwa mpaka anakuja kufikia hatua ya kuwa mtu mzima, jukumu la kumwangalia na kumjali lipo juu yako pia, na sio la Mungu peke yake tu,

Kipo kisa kimoja kwenye maandiko kinachoelezea habari husika tunayotamani kujifunza siku ya leo, habari yenyewe ni ile ya mitume kushindwa kumtoa yule Pepo kwa mtu, walihangaika kipindi kirefu, kwasababu hilo pepo lilikuwa tofauti na mapepo mengine waliyokutana nayo, mpaka Bwana Yesu alivyokuja kuliondoa na kulikemea hilo pepo na kuondoka,

Zaidi hatutaingia ndani kwa kuwa ni habari inayojulikana sana, ila kuna Mambo yanapatikana kwenye hiyo habari yenye msingi wa kukusaidia wewe mzazi au mlezi, na jukumu unalopaswa kulijua kwa watoto wako,

Embu tusome kwanza…

Marko 9:20 “Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.

21 Akamwuliza babaye, AMEPATWA NA HAYA TANGU LINI? Akasema, TANGU UTOTO.

22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia”.

Liweke jicho lako kwenye mstari wa 21, maandiko yanatuonyesha baada ya Bwana Yesu kuingilia kati kulitoa hilo pepo, akunyamaza kimya alitamani kujua historia kidogo ya mtoto, na ndo hapo anamuuliza baba wa mtoto, kwamba hii hali imempata tokea lini? na si kwasababu Bwana Yesu alikuwa hajui,alikuwa anajua kila kitu, kwa kuwa hakuna neno lililojificha mbele zake, ila alitaka kukuonyesha wewe mzazi ufahamu kwa kina kuwa yapo mambo mabaya,au mapepo yanayowakumba watoto wakiwa wangali wadogo..

Ni mapepo yanayojikita kwa ajili ya watoto tu, yanawaanza Katika hali yao ya udogo na kukaa nao hadi ukubwani huko, wanajiwekea msingi kuanzia chini kabisa ndio hapo yakija kukomaa ndani ya mtoto hali yake inakuwa mbaya kama habari tuliyoisoma lakini pia yanakuwa ni magumu Kutoka kwa ndani yake,

Mzazi jukumu la kumlea na kumjali mwanao lipo mikononi mwako mwenyewe, pengine unaweza kusema huyu ni mtoto tu, ni malaika kama wengi wasemavyo, lakini fahamu shetani alijui hilo, kazi yake kubwa ni kuharibu,kuiba na kuua,kama alimwingia mnyama ambaye ni nyoka,atashindwaje kwa Mwanadamu hata kama ni mtoto, hiyo ni kazi kubwa ya shetani, usiyaapuuzie Kabisa maisha ya rohoni ya Mtoto wako, yana thamani kubwa sana, shetani alijua umuhimu wa Yesu akiwa mtoto akataka kumuua akiwa mchanga, je wako si zaidi,

Unakuta mzazi yeye ndiye anakuwa mstari wa mbele kumfundisha mtoto wake mambo ya kidunia, anamwekea miziki ya kidunia yenye maudhui mabaya lakini anafurahia kuona mwanae anacheza na kukata mauno, huyo huyo mzazi anamtazamisha kuangalia katuni na masirizi ya tamthilia muda mwingi, unategemea vipi mapepo yasimvae mwanao?

Ila hujawahi kukaa chini na kumfundisha umuhimu wa Mungu kwenye Maisha yake, lakini hujawahi kufikiria jinsi gani anaweza kujifunza kumwimbia na kumsifu Mungu yeye mwenyewe kwa nyimbo za tenzi na sifa, yapo Mafundisho ya Sunday school kanisani, lakini hujawahi kumpeleka mwanao hata siku moja,akajifunza huko, wewe unachojali ni asome shule nzuri, awe na akili darasani, kila nguo mpya inayotoka unaumiza kichwa utaipataje, akili ya mzazi imejaa vitu vya mwilini ambavyo haviwezi kumsaidia rohoni, jiulize mara ya mwisho kumuombea mtoto wako ilikuwa ni lini? kama wewe mwenyewe hutajiangalia mwenyewe hutawezaje kumjali mwanao..

Lazima ufahamu adui shetani naye anaweka misingi yake kama usipojua jukumu lako wewe, mwisho wa hiyo habari tuliyoisoma ilikuwa shetani anakwenda kumuangamiza kabisa, mana mapepo yalikuwa yanamtupa kwenye moto, mara kwenye maji, lengo lake ni kumuua kabisa..na hilo pepo lilipata nguvu na haki ya kutenda hayo kwasababu lilishajiwekea msingi toka utotoni..

Ukiona mwanao ana tabia tofauti zilizo mbaya na ukachukizwa nazo, basi fahamu adui yupo kazini, mapepo yanatenda kazi yake, kwasababu sio Watoto walibadilika bali wazazi ndio sababu, ikiwa wewe mwenyewe huyajali maisha yako ya rohoni yeye Mtoto atawezaje kujisimamia mwenyewe,

Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”

FAHAMU JINSI YA KUYAZUIA MAPEPO YA UHARIBIFU

1) KWA KUTUMIA KIBOKO

Hii ni njia inayoonekana ngumu au isiyo na Upendo lakini nataka nikuambie ukiitumia kwa lengo zuri basi itakuletea matokeo mazuri sana, kwasababu hata biblia imesema ukimwamdhibu haumuui, zipo tabia kwa mtoto hazitoki kwa maneno tu au kumuombea bali kwa kushika kiboko, unapoona ana ujeuri ndani yake anza kuliondoa hilo pepo kwa kumuadhibu na kumfundisha ni kwa tabia gani unayomwadhibu nayo, hapo ataanza kukuelewa..

Mithali 23:13 “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.

14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu”.

2) KWA KUMFUNDISHA KANUNI ZA IMANI

Jambo la msingi pia analotakiwa kulifahamu mapema ni kuzijua kanuni za imani, yaani anaanza kuelewa umuhimu wa kuomba, unamfundisha, jinsi gani anatakiwa ajue namna ya kumwimbia Mungu na kumsifu, mfundishe kusoma biblia na kukariri vitabu vyake,hata kama hataelewa sasahivi, muonyeshe umuhimu pia wa kuhudhuria kwenye vipindi vya Sunday school,yeye mwenyewe lakini na wewe ukimuwekea msisitizo sana..

3) KWA KUMUOMBEA

Hakikisha ni desturi kila siku kuomba kwa kuwaombea wanao, Neema ya wokovu, ulinzi, Amani, mwenendo mzuri, na mengine mengi,liwe ni jukumu lako wewe mzazi..

4) MZUIE KUFANYA NA KUTAZAMA MAMBO YASIPOMPASA

Mwelekeze Katika mwenendo mwema unaoendana na jinsia yake, mzuie kuangalia magemu na tamthilia, mvishe mavazi yanayousitiri mwili wake, mavazi ya adabu yenye Heshima mbele za Mungu na jamii,

Yajali maisha ya mwanao kwa kuzingatia hayo, utaona mabadiliko makubwa sana, na mapepo hayatakuwa na nafasi kwa wanao, yajenge maisha ya ndugu zako, watoto wako, wadogo zako na wote walio wa nyumbani mwako..

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *