TU UZAO WA IBRAHIMU

Biblia kwa kina No Comments

TU UZAO WA IBRAHIMU

Yohana 8:33 “Wakamjibu, Sisi TU UZAO WAKE IBRAHIMU, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?.”

Je! we ni mzao wa Ibrahimu?

Uzao wa Ibrahimu ni upi?

Uzao wa Ibrahimu ni uzao wa YESU KRISTO, kulingana na kuwa Yesu Kristo ndiye aliyebeba ahadi za Mungu kwa Ibrahimu. ambazo Mungu alimuahidi Ibrahimu kuwa katika uzao wako nitakubariki. (Mwanzo 17:1-7)

Sasa tunalithibitishaje hili, kuwa uzao wa Ibrahimu ni uzao wa Yesu Kristo? Tunathibitisha kwa kusoma kama ilivyo andikwa katika biblia. Tunasoma

Wagalatia 3:16 “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo”.

Unaona hapo, wengine wote, akina Isaka na Yakobo,(yaani Israeli katika mwili). walibeba sehemu za baraka hizo lakini si zote.

Hivyo ili mtu ahesahiwe kuwa ni mmoja wa uzao wa Ibrahimu yaani uzao wa YESU KRISTO ni lazima azaliwe mara ya pili katika uzao wake. Na kuzaliwa mara ya pili si katika mwili bali ni katika roho. Tutakuja kuona baadaye kidogo mtu anapaswa afanye nini ili azaliwe mara ya pili. Lakini sasa tutaangalia tabia chache zinazotambulisha uzao wa Ibrahimu.

Ili kuweza kujua tabia za huu uzao wa Ibrahimu, kwanza tufahamu tabia za Ibrahimu mwenyewe na ni kwanini amebarikiwa namna hii.

Sifa aliyokuwanayo Ibrahimu mpaka akaahidiwa baraka hizo zote sio nyingine zaidi ya IMANI.

Ibrahimu tunamwita ni Baba wa Imani, kutokana na Imani tunayoiona aliyokuwa nayo kwa Mungu wake licha ya kukaa kwa muda mrefu bila kupata mwana Mungu aliyekuwa amemuahidia akizingatia na huku umri umeshakwenda yeye na mke wake, hakukata tamaa kumwamini Mungu badala yake aliendelea kusubiria mpaka Mungu alipotimiza alichomuahidia na hata alipopata mwana, zaidi ya yote tunasoma katika uzee ule Mungu alimjaribu tena amtoe mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa, Nalo hilo Ibrahimu halikumtikisa bali alidhubutu kumtoa kwasababu aliamini Mungu anaweza hata akamfufua kutoka katika wafu(Waebrania11:17-19). Ndipo Mungu akavutiwa sana na Imani ya Ibrahimu..

Lakini hilo pekee tu pekee lingetosha Mungu kumfanya Ibrahimu kuwa baba wa imani na mtu wa kuigwa kwa vizazi vyote? Watu watakaokuja kumwamini yeye baadaye?..Lipo jambo lingine la ndani zaidi tunapaswa tulijue ambalo ndilo tutaligusia kwa siku ya leo.

Tukisoma kitabu cha Waebrania tunapata kuona tabia nyingine tofauti ambayo Ibrahimu aliionyesha kwa Mungu wake. Tunasoma:

Waebrani 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. 

9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10 Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”.

Sasa ukiyachunguza hayo maandiko kwa makini utaona kuwa Ibrahimu alikuwa na jicho lingine la mbele zaidi hata ya lile alilokuwa ameahidiwa na Mungu katika mwili..Na ndio maana siku zake zote maisha yake yote hakusumbuliwa na mambo yanayopita, hukusumbuliwa na kukawia kwake kupata mtoto,hakusumbuliwa na hata kutoa mwanawe Isaka kuwa sadaka kwa Mungu wake…

Embu Soma tena hapo anasema. 9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE,..

Kumbuka Mungu alimtoa Ibrahimu nchi ya mbali sana huko Uru ya Ulkadayo na kumleta Kaanani, mahali ambapo Mungu alimwahidia kumpa kila kitu ambacho ni chema, alimwahidia kuwa atamfanya kuwa taifa kubwa sana, atamfanya kuwa uzao hodari, uzao ambao utamiliki malango yote ya adui zake wote..Atamfanya kuwa taifa tajiri, na lenye nguvu sana..

Sasa embu jaribu kutengeneza picha ingekuwa hiyo nafasi umepewa wewe, Mungu anakuambia utakuwa na uzao hodari katika nchi fulani na kwa kupitia wewe mataifa yote duniani yatabarikiwa, hivi utajisikiaje?…Ni wazi kuwa utajiona kuwa ni mtu wa kipekee mbele za Mungu kuliko wengine wote, utatanua mbawa kidogo, utajiona kuwa wewe ni mtu muhimu sana mbele za Mungu kuliko wengine..Hata ukifika katika hiyo nchi Mungu aliyokuahidia utaimiliki pengine kwa kiburi fulani, utaishi kama mfalme fulani au chifu fulani hivi kwani Mungu tayari ameshakuridhia na kukupa wewe..hata watu wote wa huo mji wakitaka kupigana na wewe hutaogopa, kwasababu Mungu alishakupa wewe milki hiyo.

Lakini kwa Ibrahimu haikuwa hivyo, alikuwa na jicho la mbali zaidi, hakutazama Baraka hizo Mungu alizomwahidia za kitambo tu, hakutazama wingi wa uzao atakaokuwa nao duniani, hakutazama ukuu wa taifa atakalolizaa duniani, hakutazama utajiri wa kimwilini, kwa hili jicho la kimwilini, bali aliyatafakari maisha yake kwa utulivu sana, akiangalia jinsi Mungu alivyomtoa Nchi ya Ulkadayo na kumleta pale Kaanani, na jinsi Mungu alivyomwepusha katika taabu zote zile, za kungojea nchi ambayo Mungu amemwahidia, akajiuliza kama Mungu anao uwezo wa kunifanya taifa kubwa ndani ya dakika moja, kwanini anakawia hivi kunipa mwana? Sababu nini?..Ibrahimu alitaka kujua kusudi la maisha, nyuma ya haya yote kuna nini?.. Na ndipo akafahamu kuwa maisha yake ni picha ya mambo yatarajiwayo mbeleni yajayo baada ya ulimwengu huu kupita. Alifahamu kuwa maisha yake ni somo, maisha yake ni sauti Mungu anayozungumza naye juu ya mambo ya mbeleni sana..ng’ambo ya pazia..

Na ndio maana tunasoma Ibrahimu licha ya kupewa utajiri wote ule wa kimwilini, bado aliendelea kuishi katika nchi ile ambayo ni kweli ilikuwa ni haki yake kustarehe na kujifurahisha lakini biblia inatuambia aliishi mule kama vile siyo nchi yake, aliishi katika milki yake kama vile sio milki yake, kama vile mgeni nyumbani kwake mwenyewe..aliishi na mke wake Sara kwenye mahema, fikiria Ibrahimu alikuwa ni mtu tajiri sana mwenye mali nyingi alizopewa na Mungu lakini hakuishi kwenye makasri,..hiyo inafunua nini?..Inaonyesha ni jinsi alivyoishi kama mpitaji hapa duniani?.

Unadhani alikuwa hajipendi?. Hapana..Biblia inatuambia ni kwasababu alikuwa anautazama mji ulio bora, alikuwa anautazamia mji wenye misingi, sio ule wa Kaanani aliopewa ambao Mungu kweli alimpa kuwa milki yake, lakini huo ingempasa aweke misingi yeye iliyodhaifu, ingempasa aubuni yeye..Lakini badala yake Ibrahimu hakufanya hivyo bali aliutazamia mji wenye misingi ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu mwenyewe.. Na mji huo si mwingine zaidi ya YERUSALEMU MPYA ya mbinguni HALELUYA!!.

Jambo hilo ndilo lililomfanya Mungu apendezwe na Ibrahimu na kumfanya awe kielelezo cha kuigwa kwa watu wote, ikiwemo mimi na wewe.

Na kama kweli wewe ni mzao wa Ibrahimu lazima tu utakuwa na tabia kama hii, utakuwa na imani hii.. kwasababu mtoto wa nyoka ni nyoka tu, vivyo hivyo mtoto wa Ibrahimu ni Ibrahimu.Ndio maana waliozaliwa mara ya pili katika uzao huu wa kifalme yaani uzao wa YESU KRISTO wanaitwa wa-Kristo, tunafanana na Yesu Kristo katika mwenendo na tabia zote.

Kumbuka YESU KRISTO Bwana wetu alikuwa ni uzao wa Ibrahimu yaani alitokea katika ukoo wa Ibrahimu na ndiye aliyebeba zile ahadi za Mungu kwa Ibrahimu.

Hivyo japokuwa alipewa na Mungu utajiri wote na mamlaka yote ya kutawala kila kitu hapa duniani lakini tunaona yeye hakutaka kuishi kama Mfalme hapa duniani, hakuishi kwenye makasri makubwa, aliishi milimani na kwenye mahema kama Ibrahimu baba yake, sehemu nyingine alisema..

“… Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.’ (Mathayo 8:20).

Hii ni kuonyesha kuwa alikuwa anaishi kama mpitaji hapa duniani akijua maisha halisi hayapo hapa, kama vile Ibrahimu aliishi katika nchi yake mwenyewe kama mgeni kwasababu alikuwa akiutazamia mji wenye haki na wa kudumu milele.

Vivyo hivyo na katika UZAO wa YESU KRISTO. Wote wanaozaliwa humo, kuna roho na tabia zinazofuatana nao katika maisha yao yote. Hivyo wanajikuta zile tabia YESU alizokuwa nazo kama Baba wa ukoo wanazirithi nao pia wanakuwa nazo. Wataishi kama wapitaji na wasafiri hapa duniani, hawatapagawa na maisha ambayo watu wengine wa dunia hii wanaangaikia usiku na mchana, kwasababu wanajua hayo siyo maisha halisi.

Hata kama watakuwa wamebarikiwa kuwa na mali na vitu vya mwilini hawataweka mioyo yao huko, wataishi kama vile hawana. Kwasababu akili zao na mioyo yao wanatazamia ule mji wenye misingi ambao mwenye kuujenga ni Mungu mwenyewe, hawataona shida kujitoa kwa kila kitu kuwekeza katika maisha yajayo.

Hawa ndio wana wa Ibrahimu.

Je! umefanyika mzao wa Ibrahimu? Kama huna hiyo sifa aliyokuanayo Ibrahimu fahamu kuwa bado hujawa mzao wake haijalishi utakiri mara ngapi! Kama bado unaupenda ulimwengu na huku unasema ni M-Kristo mzao wa Ibrahimu hapo utakuwa unajidanganya mwenyewe. Wayahudi walijua wao ni uzao wa Ibrahimu lakini kwasababu hawakuwa kama Ibrahimu, Yesu aliwaambia dhahiri kuwa ninyi ni wa baba yenu ibilisi.

Yohana 8:39 Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu.

[40]Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo.

[44]Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.

Hivyo unachopaswa kufanya kama bado hujaingia katika huu uzao wa kifalme na unahitaji leo kuingia na kushiriki baraka za Mungu ambazo ni pamoja na uzima wa milele.. unapaswa kuzaliwa katika ukoo huu wa Ibrahimu kupitia kumwamini Yesu Kristo mwana wa ahadi.

Na unazaliwa katika uzao huu kwa wewe kudhamiria kwanza kutubu dhambi zako zote na kumaanisha kuziacha kabisa kwa vitendo, na halikadhalika kuacha ulimwengu na tamaa, mitindo na namna zake zote. Baada ya hapo unaenda kubatizwa kwa kuzamishwa katika maji mengi na Kwa jina la ukoo huu yaani jina la YESU KRISTO, hapo utapokea Roho wa Mungu (Roho Mtakatifu) ambaye atakutia muhuri kuwa wewe sasa ni mzao wa Ibrahimu, mrithi wa ahadi za Mungu. Hapo hata ukifa leo moja kwa moja unapokelewa kifuani mwa Ibrahimu.

Hebu chukua leo uamuzi wa kumwamini Yesu na kumgeukia ili uokoke na hukumu iliyo mbele yako..na kama umekwisha kumwamini basi leo funguka anza kuelekeza moyo wako kule juu kwa maana hapa hatuna mji udumuo. (Kuwa mzao wa Ibrahimu kweli kweli).

Waebrania 13:14 Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *