Tukio hili litatokea hivi karibuni na kuishangaza dunia.

Siku za Mwisho No Comments

Tukio hili litatokea hivi karibuni na kuishangaza dunia.

Je! Unafahamu tukio kubwa na la kushangaza ambalo lipo mbioni kutokea?

Kama hulifahamu, basi kuna hatari kubwa iko mbele yako…kwa maana itakujia ghafla kama vile mtego unasavyo.

Siku zote gari ambalo linakimbia kwa spidi kubwa kwenye barabara ya vumbi, huwa kuna vumbi ambayo inaonekana kwa mbali ambayo kwa wewe uliye mbali ukiona utajua tu kuna kitu kinachokuja kwa spidi… hivyo utachukua tahadhari mapema ili isije ikakupitia ukapata madhara.

Ndivyo ilivyo kwa tukio la kurudi kwa Yesu kuja kunyakua watakatifu yaani tukio la UNYAKUO, wale ambao wameshajiweka tayari… tayari wameshaona lile fumbi kwa mbali, mwanzoni tulikuwa tunahisi tu harufu ya unyakuo ndio zile dalili kadha wa kadha ambazo zimetajwa ndani ya biblia mfano matetemeko, tetesi za vita, tauni kama korona, manabii wa uongo, Israeli kuwa taifa huru, n.k, sasa hizo zilikuwa ni harufu tu, unajua hata kipindi kifupi kabla ya mvua kunyenya huwa wanyama wanaanza kuhisi harufu..na utaona wanaelekeza pua zao huko juu. Na halikadhalika wateule wameanza kuhisi harufu ya unyakuo toka mbali na ndio maana wameelekeza mawazo yao juu, Bwana alisema..

Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia”. (Luka 21:28).

Kwa sasa sio harufu tu bali tunaona wazi wazi lile fumbi linakuja kwa kasi, na harufu inazidi kuwa kali siku kwa siku..ndio maana watu wengi wameanza kukisia kuwa ni siku fulani, mwezi fulani…na wengine wanasema wameonyeshwa kwenye maono, ndoto, hiyo ni lile fumbi kabla tukio lenyewe halijafika, au tuseme ni kama vile wanavyoandaa njia wakati mtu mkubwa tuseme labda Raisi yupo njiani kuja, utaona askari wanatangulia kuweka mazingira sawa katika hilo eneo…ndivyo ilivyo kwa tukio hili ambalo linaenda kutokea hivi karibuni. MFALME ANAKUJA.

Mwanzoni ilikuwa ni vigumu kumtambua mpinga-kristo ni nani, lakini katika siku za karibuni kila mkristo halisi ameshamjua mpinga-kristo na makao yake, zamani kidogo tuseme miaka 10 kurudi nyuma kuna mambo ambayo ni kama ilikuwa ni vigumu kufanyika… lakini sasa hivi kulingana na teknolojia kukua kwa kasi..ni kama kila kitu kinawezekana… yaani maarifa yameongezeka kwa kasi sana ndani ya hichi kipindi, na mambo maovu pia yameongezeka kwa kasi sana, utaona mambo kama ushoga, wanawake kutembea uchi, wanaume na wanawake kubadili maumbile yao, ngono hadharani, teknolojia imerahisisha.

Sasa hivi kuna akili bandia (AI), watu bandia(maroboti), na vitu kadha wa kadha ambazo zimewekwa tayari kwa utawala wa mpinga-kristo ambaye ataenda kutambuliwa na dunia hivi karibuni baada ya UNYAKUO WA WATAKATIFU, Unaona jinsi muda unavyokwenda kasi!, Hayo mambo sio ya miaka elfu 10 ijayo ni mambo ambayo mimi na wewe tutaenda kushuhudia ndani ya kizazi chetu hivi karibuni.

Usiposhuhudia tukio la unyakuo basi utashudia tukio la mpinga-kristo kuanzisha mfumo mpya duniani na bila shaka utapokea chapa yake.

Injili tayari imefika kila taifa, sasa ni nini tunachosubiri kama sio unyakuo tu. Ni kweli hakuna ajuaye siku wala saa hata malaika hawajui, lakini tumepewa majira na nyakati kwamba tukiona hayo tujue Mwana wa Adamu yupo mlangoni.

Kwa kawaida hakuna mtu ajuaye siku ambayo mvua itanyesha hata wale wanaotabiri nao wanakisia tu kupitia vipimo vyao, lakini hawana uhakika asilimia zote, lakini tumepewa kutambua majira ya mvua, kwamba tukiona mawimbi meusi yakitanda juu tunajua kabisa saa yoyote au siku yoyote mvua itanyesha na ndivyo ilivyo.

Sasa kama tunafahamu hayo yote, kwanini hatufahamu nyakati na majira haya kuwa muda wowote Yesu anarudi! Huoni huo ni unafiki? N’gombe wanajua mvua ipo karibu kwa kunusa tu, je! sisi wanadamu ambao tuna akili zetu si zaidi sana kutambua kuwa siku zimeisha na hukumu imekaribia.

Luka 12:54 Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

[55]Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

[56]Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?

Sasa ni nini tunapaswa kufanya katika hichi kipindi cha kumngojea Bwana?

Je! tuuze vitu vyetu tukae kusubiria unyakuo? au tuache kufanya shughuli zetu za kila siku, La hasha!. Tukifanya hivyo tutakuwa hatupo miongoni mwa wateule, vilevile tukiwa na hofu ya kuogopa unyakuo ni ishara ya wazi kuwa hatujatiwa muhuri wa Roho, hivyo unyakuo hautatuhusu haijalishi tunasema kwa vinywa vyetu kuwa tumeokoka.

Ni kama tu habari ya kufa, ukiona kuwa unaogopa kufa kwamba ikitokea ukaambiwa leo ndio mwisho wako tumbo linakuuma au unazimia kabisa, basi fahamu kuwa unahitaji kumpokea Yesu wa kweli, kwamaana waliokoka kweli kweli mauti haina nguvu juu yao, biblia inasema hatukuipokea roho ya utumwa iletayo hofu (Warumi 8:15), bali tulimpokea Roho Mtakatifu ambaye anashudia na roho zetu wakisema njoo Bwana.

Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.

[20]Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. AMINA; NA UJE, BWANA YESU.

Hivyo hofu yoyote ile iwe ya mauti, iwe ya wachawi, iwe ya majini/mashetani, au hata ya maisha unaogopa kesho utaishije, hiyo ni ishara kuwa bado hujapokea Roho Mtakatifu na hivyo hata ukifa au unyakuo ukitokea leo utakuwa hatarini ndio maana roho yako inakataa kukubaliana na hayo matukio ni kwasababu hiyo.. haujawa tayari/haujaokoka.

Hivyo kwa wewe ambaye upo tayari kwa ajili ya unyakuo na roho yako inakushudia, unachopasawa kufanya katika kipindi hichi ni kuongeza kiwango chako cha utakatifu. Biblia inasema…

Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

[11]Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na kufanya haki; NA MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA”.

Umeona hapo, tunachopaswa kufanya ni kujitakasa kila siku, na tunatakasika kwa kusoma Neno la Mungu, kuomba kwa bidii, kuzidi kumtafuta Mungu kwa bidii na kujihadhari na ulimwengu…huku tukifanya kazi ya Mungu/kuhubiri Injili ya utakatifu. (kwa ujumla ni kukesha katika roho)

Na vilevile tunapaswa kuendelea kukutanika pamoja na kuwa na ushirika mtakatifu yaani kujengana kiimani..ndivyo biblia inatuhasa tufanye katika kipindi hichi cha kumngoja Bwana.

Waebrania 10:25 wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.

Lakini kama bado upo nje ya wokovu na umekuwa unasikia injili kila siku hutaki kutubu na kuacha dhambi, hutaki kuacha ulimwengu, umebaki kushikilia hiyo dini yako na hilo dhehebu lako ambalo haliamini katika utakatifu, umehubiriwa vya kutosha kuwa wanawake kuvaa mavazi ya wanaume ni machukizo kwa Mungu, kujipamba kama Yezebeli ni hatari kwa roho yako, lakini bado unaendelea kutia mawanja, mawigi, mahereni, na kuvalia mavazi ya aibu..huku ukijidanganya kuwa unaishi katika zama mpya, na kwamba wale wanaojistiri wanaishi katika zama za kale..leo nakuambia wala sio mimi ila Neno la Mungu linakuambia ”mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu”.

Hivyo ni heri uache huo uvuguvugu. Ubaki kuwa baridi kabisa kwa maana ikiwa unavaa nguo fupi inayoaonyesha mapaja yako au inayochora mwili wako hauna tofauti na anayetembea uchi kabisa, ikiwa unajichua, unatazama pornography, unasikiliza miziki, movies zenye maudhui hayo ya zinaa, hauna tofauti kabisa na wale wanaofanya, ikiwa unauza sigara, pombe, hauna tofauti na wanaotumia, ikiwa unawauzia wanawake suruali, vipodozi za kubadilisha mionekano yao hauna tofauti na wanaofanya huo uasi, na mambo yote ni vivyo hivyo, kwahiyo ni heri uamue kimoja, ulimwengu au kwa Yesu.

Ukichagua kwa Yesu basi kuwa tayari kuingia hiyo gharama ya kuacha vyote lakini kama hutaki kuacha… basi usijaribu kidogo kuacha nusu nusu, ni heri ubaki huko huko mazima kwenye ulimwengu.

Lakini ikiwa upo tayari kuacha vyote na kuyasalimisha maisha yako kwa Yesu leo na hujui pa kuanzia. basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya somo hili.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *