Tunza moto wa madhabahu

Maswali ya Biblia No Comments

 

Nakusalimu katika jina tukufu, Jina la Bwana wetu YESU KRISTO. Mkuu wa uzima.
Karibu tujifunze Neno la Mungu..

Katika agano la kale, Mungu alimwagiza Musa ajenge Hema iwe mahali pa Mungu kushuka na kusema na wana wa Israeli(Kutoka 25:1-9) hema hiyo ambayo iliitwa hema la kukutania ilikuwa ni ya kuhama hama kulingana na safari ya wana wa Israeli jangwani..

Hivyo haikuwa ya kudumu sehemu moja. Ila baadaye baada ya wana wa Israeli kufika nchi yao ya ahadi (Kanaani) alikuja kutokea Mfalme Daudi na akaazimia moyoni mwake kukarabati ile hema na kufanya iwe nyumba ya Bwana, Hivyo alikusudia kumjengea Mungu nyumba na nyumba hiyo ilikuja kujengwa na mwanaye Sulemani na ikaitwa Hekalu la Sulemani.

Sasa moja ya jambo ambalo lilikuwepo ndani ya hiyo nyumba ya Mungu ni madhabahu ambayo juu yake kulikuwa na moto uliokuwa ukiwaka daima usiku na mchana. Na moto huo ulitumika kwa ajili ya kuteketeza Sadaka mbali mbali ambazo zilikuwa zinaletwa na wana wa Israeli,(Sadaka ya kuteketezwa) pamoja na shughuli zingine ndani ya nyumba ya Bwana..na kazi zote zinazohusiana na hiyo madhabahu na nyumba ya Mungu kwa ujumla ilifanywa na makuhani tu ambao walikuwa ni Walawi.

Mambo ya Walawi 6:8-13

8 “BWANA akanena na Musa na kumwambia,

9 Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.

10 Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani, atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.

11 Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi.

12 NA HUO MOTO ULIO MADHABAHUNI ATAUTUNZA UWAKE DAIMA JUU YAKE, USIZIMIKE; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.

MOTO UTATUNZWA UWAKE JUU YA MADHABAHU DAIMA; USIZIMIKE.”

Sasa katika agano jipya.. maandiko yanasema nyumba ya Mungu (Hekalu) ni miili yetu..

1Petro 2:5 “Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, MMEJENGWA MWE NYUMBA YA ROHO, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.”

Pia tunalithibitisha hili katika..

1Wakorintho 3:16-17 16″Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.”

Soma pia 1Wakorintho 6:19

Umeona? Mwili wako ni nyumba ya Mungu!.
Sasa ni vizuri tufahamu kuwa agano la kale ni kivuli cha agano jipya (Waebrania 10:1), kama tulivyosoma katika agano la kale kulikuwepo na madhabahu ndani ya ile nyumba ya Mungu ambayo juu yake ilikuwa na MOTO iliyokuwa ikiwaka wakati wote bila kuzimika, makuhani walikuwa wanachochea kwa kuni kila siku.

Vivyo hivyo na sisi tuliomwamini Bwana Yesu na kutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha kabisa na kubatizwa ubatizo sahihi, ndani yetu tunakuwa na MOTO ambayo ni Roho Mtakatifu..na moto huu unapaswa kutuzwa daima usizimike, kwani maandiko yanasema “Mzimzimishe Roho” (1Wathesalonike 5:19),

UTAUTUNZAJE MOTO WA ROHO MTAKATIFU..

1 DUMU KATIKA UTAKATIFU.

Tukirudi katika agano la kale.. kulikuwepo na sheria kadha wa kadha ya usafi kwa makuhani wanaohudumu madhabahuni pa Mungu, kuhani alitakiwa kuzingatia usafi wa hali ya juu sana, la, sivyo kukionekana uchafu wowote adhabu yake ilikuwa ni kifo, tena ule moto ulikuwa unatumika tu kwa shughuli za madhabahuni basi. Na si vinginevyo, haukuruhusiwa kutoa huo moto na kupeleka nje kufanyia shughuli zingine au kuleta moto mwingine kutoka nje na kuingiza madhabahuni bila Bwana kuagiza, kufanya hivyo ni kujitafutia kifo..
Utakumbuka wale wana wawili wa Haruni (Nadabu na Abihu) walileta moto mwingine kutoka nje (labda kutoka huko kwenye marago yao) na kuingiza madhabahuni pa Mungu na kilichowatokea ni Kifo..

Walawi 10:1 “Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza.

2 Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA.”

Vile vile na wewe uliyeokoka na ukapokea moto (Roho Mtakatifu) huna budi kuishi katika hali ya utakatifu kama kuhani wa Mungu, ili moto uendelee kuwaka ndani yako ni lazima udumu katika hali ya usafi kiroho, Kumbuka Roho Mtakatifu kama jina lake lilivyo ni mtakatifu..

hakai mahali pachafu, unapokuwa mchafu unapelekea huo moto kufifia ama kuzimika kabisa, unapoingiza moto mwingine (roho nyingine) ndani ya nyumba ya Mungu ambayo ndiyo mwili wako..unapelekea hasira ya Mungu kuwaka juu yako na mwicho usipogeuka, Mungu ataizima ile nuru iliyokuwa ikiwaka ndani yako(Roho Mtakatifu atakuacha) na hapo utakuwa umekufa kiroho,

Utakuwa hauna tofauti na yule ambaye hajaokoka..na itakuwa vigumu tena uokoke, haijalishi utahubiriwaje! hakutakuwepo tena na nguvu ya kukuvuta uokoke, wala hautasikia tena kuhukumiwa na dhambi, kwa ufupi utakuwa umeandikiwa tu ziwa la moto!. na hiyo ndiyo hasara ya kuachwa na Roho Mtakatifu,

Waebrania 6:4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno nzuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.”
Soma pia..

1Petro 2:20 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.

21 Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.”

Umeona hapo!. Kuna hatari sana ya kuachwa na Roho Mtakatifu pale ambapo umempokea na ukaja kukengeuka kwa kuacha utakatifu na kugeukia ulimwengu, hivyo ikiwa umemzimisha moto wa Roho Mtakatifu ndani yako kwa kuacha utakatifu uliokuanao hapo kwanza, tubu sasa na uendelee kuishi katika utakatifu kabla huo moto haujazima kabisa maana ikizima ndio utakuwa mwisho wako,

Ufunuo 2:5 “Basi, Kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

Jihadhari na moto wa kigeni ndani ya nyumba ya Mungu (mwili wako), kumbuka unapoingiza moto wa kigeni (roho nyingine chafu) ndani ya hekalu la Mungu unafanya hasira ya Mungu iwake juu yako!!
fahamu kuwa chochote cha kidunia ambacho unaweka kwenye mwili wako kama urembo ama fashion elewa kuwa kupitia vitu hivyo unaingiza roho nyingine chafu ndani yako pasipo wewe kujua na mwisho utapelekea ule moto wa Mungu kufifia na hatimaye kufa ndani yako!!, hizo vipodozi, pafyumu, lipstick, vihereni, bangili, cheni, hizo rangi unazopaka kwenye kucha, kichwani, hizo wanja, wigi, na kila aina ya mapambo yatokanayo na dunia hii..zote zina roho chafu nyuma yake, hizo picha za ngono na filamu,na miziki za kidunia unazozitama zote zina roho chafu nyuma yake, hayo magemu, na hizo movies unazofuatilia yana maroho nyuma yake na mwisho utajikuta unafungua milango ya kila aina ya pepo ndani yako,..na Kumbuka mwili wako sio nyumba ya kuhifadhi mapepo bali ni nyumba ya Roho (1Petro 2:5…Mmejengwa mwe nyumba ya Roho) Hivyo ili moto wa Roho Mtakatifu uendelee kuwaka ndani yako huna budi kuishi katika hali ya usafi kwa kujitenga na ulimwengu,

Jitenge na mapambo ya kidunia, jitenge na makundi ya kidunia, jitenge na filamu za kidunia,.unatazamiaje moto wa Roho Mtakatifu uendelee kuwaka ndani yako ikiwa kila wakati wewe ni kukesha kutazama movies, mipira, miziki za kidunia,kukaa vijiweni na kufuatilia mambo yasiyo na maana, unatazamije Roho Mtakatifu adumu ndani yako ikiwa nyumba yake ambayo ni mwili wako umeigeuza kuwa nyumba ya makahaba, kumbuka maandiko yanasema Hekalu la Mungu ni takatifu ambalo ndilo ninyi (1Wakorintho3:17), itunze nyumba ya Mungu, isitiri kwa mavazi ya heshima na adabu, si kwa kutembeza uchi kwa kuvalia vimini, suruali kwa mwanamke,

si kwa kuweka uchafu wowote wa kidunia ambayo unadhani ni urembo kumbe unaingiza roho chafu ndani ya nyumba ya Mungu,.. maandiko yanasema wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani.”
(1Timotheo2:9) soma pia 1Petro 3:3,
Kwa kufanya hivyo.. kuishi maisha matakatifu utazidi kufanya moto wa Roho Mtakatifu uzidi kuwaka ndani yako!.

2 MAOMBI

Jambo la pili la kufanya ili moto wa Roho Mtakatifu uzidi kuwaka ndani yako ni kudumu kwenye maombi.. Maombi ni kama kuni ya kuwasha moto ndani yako, na neno la Mungu linasema moto hufa kwa kukosa kuni (Mithali 26:20).. Hivyo ili moto wako uendelee kuwaka daima huna budi kuchochea kwa kuni za maana ni si kwa mabua,

Walawi 6:12 “Na huo moto ulio madhabahuni utautunza uwake daima juu yake, usizimike; NAYE KUHANI ATATEKETEZA KUNI katika moto huo kila siku asubuhi;…)”

Fanya moto uzidi kuwaka kila siku kwa kuomba na kusali kila wakati…walau kila siku saa limoja usiache kuomba, siri ya kujazwa Roho Mtakatifu ni kudumu kuomba kila wakati..

Luka 11:13 “Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?”

Hapo anasema “HATAZIDI SANA” maana yake ni jambo endelevu.. kadri unapoomba ndivyo unavyozidi kujazwa, ndivyo moto unavyozidi kuwashwa ndani yako.
Hivyo we kama mtu uliyemwamini Bwana YESU na kupokea Roho wake Mtakatifu..usiwe mlegevu kwenye eneo la maombi, kumbuka unapodumu kuomba ndivyo wokovu wako unavyozidi kuimarika..kwani adui hawezi kukusogelea, nani awezaye kusogelea kwenye moto unaowaka? Kwanini leo unashindwa na tamaa za mwili, mawazo mabaya, n.k ni kwasababu yawezekana umepoa kimaombi,

3 KUSOMA NENO LA MUNGU NA KUSHUHUDIA/ KUHUBIRI

Hii ni jambo lingine ambalo unapaswa kufanya ili moto wa Roho Mtakatifu uendelee kuwaka ndani yako!!
Ukiwa msomaji wa Neno la Mungu mara kwa mara na kushudia/ kuwahubiria wengine waokoke kama wewe,

unazidi kumpa Roho Mtakatifu nafasi ndani yako ya kuzidi kukusogelea na kukufundisha na hatimaye utazidi kuongezeka viwango vya kumtumikia Mungu.. kumbuka Neno la Mungu ni TAA hivyo huna budi kuweka ndani yako kwa wingi ili uzidi kutoa mwanga mkali.. ambao unatosha kukumulikia njia na pia kuwamulikia wengine.

Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”

Weka Neno la Mungu ndani yako kwa wingi ili uzidi kuangaza kote, hata walio gizani waone njia,

Wakolosai 3:16 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”

Zingatia hayo mambo manne ili moto wa Roho Mtakatifu uzidi kuwaka ndani yako!!, Kumbuka tunaishi katika siku za mwisho, na Bwana Yesu alisema..

Luka 12:35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na TAA zenu ziwe zinawaka.”

Tunza moto wa Roho Mtakatifu maana Bwana Yesu yupo karibu.. kumbuka akija akakukuta upo gizani na taa yako imefifia hautaenda kwenye unyakuo.. maana atakuja saa usiyoijua, utakuwa kama wale wanawali watano wapumbavu (Mathayo 25)

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *