
UKITII, YESU ATAKUOKOA.
Ni Kwanini watakaotangulia kwenda mbinguni wawe ni watu wanaoonekana kuwa mbali na Mungu, kuliko watu wa kidini?
Mathayo 21:31 “….Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.”
Mpaka kupelekea Bwana Yesu kuzungumza maneno hayo, ni kutokana na mfano aliousema juu yake kidogo, uliowahusu watoto wawili wa baba mmoja. Ambapo Baba yao alipowaita na kuwatuma shambani mwake wakafanye kazi, biblia inatuambia yule wa kwanza bila kusita aliitikia wito na kumuhakikishia baba yake kuwa atakwenda shambani, lakini baadaye hakwenda..Na yule wa pili alipotumwa yeye aligoma pale pale mbale ya baba yake, hakwenda popote. Lakini baadaye akajutia uamuzi wake, kuwa amekosea sana, hivyo akatubu na muda huo huo akaenda shambani kwa baba yake, kufanya kazi.
Ndipo Yesu akawauliza kati ya hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya Baba yake?. Wakasema ni yule wa pili,
Yesu akawaambia sasa..
Mathayo 21:31b “…Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.
[32]Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.”
Hii ikiwa na maana kuwa, wapo watu wengi leo hii ambao tunawaona ni wakaidi mbele za Mungu, Lakini wakiwa tayari kutubu, na kutii. Yesu Kristo atawasamehe mara moja, na kuwapa kipaumbele kikubwa sana katika ufalme wa mbinguni, kuliko hata watu wanaojiona ni wa kidini, ambao wanaijua haki yote, na huku matendo yao yanaenda kinyume na makusudi ya Mungu.
Pengine wewe ni mmojawapo wa mwana mkaidi mbele za Mungu. Na pengine hata leo bado unaendelea na ukaidi wako. Naamini ipo sababu kwanini leo umekutana na ujumbe huu, Yesu anakupenda na anataka akuokoe na kukupa tumaini jipya la Maisha katika kipindi hichi cha siku za mwisho. Pengine unaweza ukajiona una dhambi nyingi zisizosameheka, ukadhani kuwa Mungu ameshakuchukia hakupendi tena, Lakini nataka nikuambie, Mungu anakupenda, na ndio maana bado alikuwa radhi kuketi ili kula na kunywa pamoja na watu wenye dhambi.
Marko 2:16 “Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?
[17]Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi”.
Umeona? Ni wewe tu leo kufungua moyo wako, akubadilishe, yeye yupo tayari kukupokea na kukusamehe na kukupa raha nafsini mwako sawasawa na (Mathayo 11:28). Kwasababu hukumu yake ipo karibu na hapendi upotee katika ziwa la la moto, ukifa katika hali hiyo.
Hivyo ikiwa utapenda kupata msaada wa kuokoka au kubatizwa, basi wasiliana nasi kwa namba zetu, unazoziona chini ya makala hii nasi tutakusaidia kwa jambo hilo bure kabisa ndugu yetu.
Bwana akubariki sana.
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618