Usikimbilie kutafuta msaada kwa miungu.

Uncategorized No Comments

Usikimbilie kutafuta msaada kwa miungu.

Jambo linalomchukiza Mungu sana ni pale watoto wake wanapokimbilia kutafuta msaada kwa miungu wakati yeye yupo na hashindwi na jambo lolote.

Na miungu siyo tu kwenda kwa waganga wa kienyeji, au kwa manabii wa uongo.. bali hata kwa watu wa kawaida…ukiwategemea sana wanakuwa miungu yako na mwisho wa siku Mungu atakulaani mwenyewe, kwani biblia inasema..

Yeremia 17:5 “BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, Na moyoni mwake amemwacha BWANA.”

Angalia unapokutana na tatizo lolote iwe ni ugojwa au changamoto yoyote, wakwanza kumkimbilia ni nani? Je! ni mganga mashuhuri unayemjua? Je ni Daktari, Je ni mchungaji au Nabii fulani. Ukiwafanya hao wote kuwa wakwanza na ukawategemea Zaidi ya Mungu, wanakuwa miungu kwako…na badala ya kupokea uponyaji unapokea kifo. Ndicho kilichomtokea Ahazia Mfalme wa Israeli, alipougua ugonjwa wake..alikimbilia kuuliza kwa mungu wa mataifa wakati Mungu wa Israeli yupo na hajashindwa na wala hajawahi kushindwa, na balala apokee uponyaji akapokea kifo kwasababu alitegemea miungu mingine atatuliwe tatizo lake.

Tunasoma..

2Wafalme 1:1-4,17 Ikawa, baada ya kufa kwake Ahabu, Moabu wakawaasi Israeli.

[2]Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu.

[3]Lakini malaika wa BWANA akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, JE! NI KWA SABABU HAPANA MUNGU KATIKA ISRAELI, HATA MNAKWENDA KUULIZA KWA BAALI-ZEBUBU, mungu wa Ekroni?

[4]Basi sasa, BWANA asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.

[17]Basi akafa, sawasawa na neno la BWANA alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.

Ukikutana na changamoto ya ugojwa au tatizo lolote, kabla hujakimbilia kwa madaktari, au watu fulani, hebu piga magoti muulize Mungu juu ya ugonjwa wako au tatizo lako, kabla hujatafuta msaada wa maombezi, au matibabu, hebu ingia kwenye maombi, ongea kwanza wewe na Mungu, Mungu yupo karibu na wewe zaidi hata kule unakokimbilia.

Ukimfanya Mungu awe tegemeo lako kwa kila kitu, yeye atakupa suluhisho la matatizo yako yote, kama ni ugojwa anaweza akakuponya hapo hapo kitandani pasipo mtu yoyote kuhusika, au akakuleta mtu, au akakupa amani ya kwenda kwa Daktari..vyovyote vile yeye ana njia nyingi za kumponya mtoto wake.

Lakini ukikimbilia kwa waganga, au kwa watu fulani, ukahangaika huku na kule na huku umemwacha Mungu moyoni mwako, fahamu kuwa unajitafutia kifo badala ya uponyaji.

Halikadhalika ukiwa mwana wa Mungu huna haja ya kutafuta msaada kwingineko ili ushindane na maadui zako, yaani watu wanaotumiwa na ibilisi kukudhuru, unachopaswa kufanya ni kuwaombea tu ili wapate neema ya wokovu, kemea roho chafu zinazowatumikisha… yamkini ni roho za wivu, usengenyaji, hasira, matusi, kiburi, n.k vunja hizo roho kwa jina la Yesu Kristo, wala usipigane moja kwa moja na watu, kumbuka vita vyetu si vya damu na nyama bali ni juu ya falme za giza.

Na kama kweli umeokoka kabisa kabisa yaani umefanyika mwana wa Mungu, basi fahamu kuwa Mungu ni Baba yako, na hakuna mzazi asiyewajibika kumlinda mwanae. Hivyo tayari unao ulinzi wa kutosha, hakuna chochote kitakugusa, hivyo huna haja ya kuogopa vitisho vya watu na mashetani…ukiona una hofu ya wachawi, majini, au watu fulani au chochote kile, basi fahamu kuwa hiyo ni ishara kuwa huwenda Bado hujafanyika mwana wa Mungu.

Mfalme mmoja wa Yuda alikuwa anamtegemea Mungu kwa kila kitu, na hata maadui zake walipokuja kupigana naye..yeye hakutumia nguvu yoyote kupigana bali BWANA alimpigania kinyume na maadui zake, lakini siku moja alipotishiwa na adui zake, alimuacha Mungu wake aliyempigania siku zote akaenda kutafuta msaada kwingineko, hivyo akapoteza ile nafasi ya ulinzi kwa Mungu na hatima yake ikawa mbaya.

2Mambo ya Nyakati 16:1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa kutawala kwake Asa, Baasha mfalme wa Israeli akapanda juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.

[2]Ndipo Asa akatoa fedha na dhahabu katika hazina za nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, akampelekea Ben-hadadi mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,

[3]Kwangu na kwako na liwe agano kama lilivyokuwa kwa baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea fedha na dhahabu; basi, uvunje agano lako na Baasha, mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.

[4]Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawapeleka maakida wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli; wakapiga Iyoni, na Dani, na Abel-maimu, na miji ya hazina yote ya Naftali.

[5]Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo, akaacha kuujenga Rama, akaikomesha kazi yake.

[6]Ndipo mfalme Asa akawatwaa Yuda wote; nao wakayachukua mawe ya Rama, na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye akajenga kwa vitu hivyo Geba na Mispa.

[7] WAKATI ULE HANANI MWONAJI AKAMWENDEA ASA MFALME WA YUDA, AKAMWAMBIA, KWA KUWA UMEMTEGEMEA MFALME WA SHAMU, WALA HUKUMTEGEMEA BWANA, MUNGU WAKO, KWA HIYO LIMEOKOKA JESHI LA MFALME WA SHAMU MKONONI MWAKO.

[8]JE! HAO WAKUSHI NA WALUBI HAWAKUWA JESHI KUBWA MNO, WENYE MAGARI NA WAPANDA FARASI WENGI SANA? LAKINI, KWA KUWA ULIMTEGEMEA BWANA, ALIWATIA MKONONI MWAKO.

[9]Kwa maana macho ya BWANA hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. KWA HAYO UMETENDA UPUMBAVU; kwani tangu sasa utakuwa na vita.

Leo hii ndugu yangu biblia inatufundisha na sisi tuwe na mioyo iliyomwelekea Mungu. Kwasababu macho ya Mungu yanakimbia-kimbia duniani kote, ikiwa na maana Mungu anaangalia anarudi tena anaangalia, anarudi tena anaangalia aone mtu atakayekuwa na moyo mkamilifu utakaomwelekea yeye kwa kila kitu ili azionyeshe nguvu zake.

Kama ilivyokuwa kwa mfalme Asa. Tuweke tegemeo letu lote kwa Mungu, tumtwike yeye fadhaa zetu zote, tusiwe wepesi kuwakimbilia wanadamu, bali mioyo yetu siku zote tuielekeze kwa Mungu muumba wa mbingu na nchi, kwasababu yeye anawaangalia watu kama hao waliokamilika mioyo aonyeshe nguvu zake zote. Tuvumilie na kumtegemea Mungu hatari inapojitokeza mbele yetu..Tusiwapendelee wanadamu hata kama ni ndugu zetu, mabosi wetu, bali sisi tuweke tegemeo letu lote kwa Bwana YESU basi.

Lakini ikiwa haujampa Yesu maisha yako, fahamu kuwa hakuna msaada utapata kwa Mungu, na huko unakotegemea hakuna matumaini..hivyo ni heri leo ukampa Bwana maisha yako maana mlango wa neema bado upo wazi kwa ajili yako, damu ya thamani ya Yesu Kristo bado inafanya kazi hata sasa hivi.. lakini imebaki kipindi kifupi sana isimame kufanya kazi yake. Usisubiri kipindi Fulani kifike , hicho hakitafika ndugu yangu, hiyo ni injili ya shetani anayokuhubiria moyoni mwako.. muda wa wokovu ni sasa biblia inasema hivyo.

Hivyo chukua uamuzi sasa wa kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana Yesu kikamilifu, na utakapofanya hivyo kwa kudhamiria kabisa kutoka ndani ya moyo wako, kutubu kwa kuacha dhambi na maisha yako ya kale, basi yeye mwenye atakupa uwezo wa kuzishinda dhambi. Na haraka mara baada ya kuamini kwako unapaswa ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako. Kisha Roho wa Mungu ataachiliwa juu yako kukulinda na kukuongoza katika kweli yote. Na baada ya hapo utakavyozidi kuuelekeza moyo wako kwa Mungu na kumtegemea yeye siku zote ndivyo utakavyouona mkono wake katika maisha yako, Na Mungu atakutumia wewe kuonyesha nguvu zake kwa wengine.

Ni matumaini yangu utafanya hivyo. Na Bwana akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *