USIKUBALI KUPOTEZEWA MUDA
Kati ya jambo ambalo unapaswa kuzingatia sana katika safari yako ya wokovu na hata katika maisha haya ni kitu kinachoitwa MUDA, ukweli ni kwamba muda ni kitu pekee ambacho kina thamani zaidi ya kila kitu..hapa duniani.
Hakuna mtu aliyewahi kununua muda hata sekunde moja, haijalishi atakusanya fedha kutoka kwenye mabengi yote duniani, huwezi kuongeza wala kupunguza muda.
Mungu ametupa masaa 24 kwa siku..hakuna mtu atakayeza kujiongezea zaidi au kupunguza.. Ndio maana kila mtu anapaswa awajibike kutumia muda wake vizuri pasipo kuruhusu mtu mwingine au kitu chochote kuchezea muda wake…kwa maana ukipoteza muda huwezi kwenda kupata tena kama huo..na hata ule ambao unasema unafidia huo ni muda mwingine ambao ungepaswa ufanye jambo lingine… hivyo yakupasa ungalie sana jinsi unavyotumia muda uliopewa chini ya jua.
Jambo ambalo shetani aligundua mapema ili awapeleke watu mbali na Mungu ni kuwapotezea muda..kwa mfano biblia inavyosema..
“Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.” (Mhubiri 12:1)Shetani kwa kulifahamu hilo, alijua kuwa kumbe muda ambao tunapaswa kumkumbuka muumba wetu na kumtafuta ni wakati wa ujana na sio wakati wa uzee, hivyo alichokifanya shetani ni kubuni vitu ambavyo vitawapotezea vijana muda ili wasimtafute Mungu wakati wa ujana wao.. Kwahiyo akavileta vitu kama kamari, magemu, mipira, na burudani burudani ambayo kwa nje yanaonekana kuwa na lengo la kujifurahisha, kumbe! moja ya ajenda ya kishetani iliyobuniwa kuzimu ni kuwapotezea vijana muda ili wasimtafute Mungu mapema. Ndio maana unaona hizo vitu sasahivi vipo kila kona hata sehemu za porini.. lazima ukute sehemu wanachezea hiyo kamari na hayo magemu na sana sana vijana ndio utawakuta.
Na sehemu nyingine inayowapotezea watu wengi muda wa kumtafuta Mungu ni hizi simu, tv, na mitandao kwa ujumla..utamkuta mtu usiku kucha anakesha kuangalia simu au tv, halafu kitu anachokitazama utakuta labda ni movie, au yupo anachati, au anangalia vichekesho n.k vitu ambavyo havimfaidii chochote kwenye roho yake zaidi sana vinampotezea tu muda na kumjaza kila aina ya roho chafu.
Halikadhalika utafutaji wa fedha..ni moja ya sehemu ambayo adui hutumia kuwapotezea watu muda wasimtafute Mungu, ukweli ni kwamba fedha ni nzuri ikitumiwa vizuri..ila pale zinapogeuzwa kuwa ndio kila kitu kiasi kwamba kama hauna huwezi kuishi.. fedha hizo zinakuwa ni miungu, Na ndio hapo unakuta misemo mbali mbali watu wakizitumia kwasababu ya kutafuta fedha, kwa mfano msemo maarufu kwa sasa ni ”ngoja nijitafute kwanza” “tafuta pesa” hizo ni misemo ambao zinabuniwa kuzimu kwa ajili ya kuwafanya watu wazame sana kutafuta fedha kuliko Mungu. Na ukweli ni kwamba hakuna mtu aliyewahi kufikia mwisho wa kutafuta fedha…kadri mtu anapozidi kutafuta ndio anajiona bado anauhitaji mpaka anaenda shimoni. Na ndicho adui shetani anachotaka.
Hivyo ikiwa umeokoka kweli kweli.. angalia jinsi unavyotumia muda wako katika siku, angalia ni vitu gani vinakupotezea muda wa kumwabudu Mungu, je! ni watu gani wanakupotezea muda wako wa kukaa uweponi mwa Mungu.
Katika biblia tunasoma habari ya mtu mmoja ambaye alikuwa amepanga safari yake yeye na mkewe, lakini ikawa kila alipotaka kusafiri mkwewe alimzuia zui.. mpaka baadaye baada ya siku kadha kupita aliamua kwenda, na huko njiani alikutana na tukio baya sana.. lakini tatizo lilianzia kwa kupotezewa muda wa kutoka huko alikokuwa.
Waamuzi 19:1 Ikawa katika siku hizo, hapo kulipokuwa hapana mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa hali ya ugeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda.
[2]Kisha huyo suria yake akaandama ukahaba kinyume chake, kumwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa kuko muda wa miezi minne.
[3]Kisha mumewe akainuka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda wawili; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye.
[4]Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, AKAMZUIA; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala kuko.
[5]Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu.
[6]Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi.
[7]Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe AKAMSIHI-SIHI, naye akalala kuko tena.
[8]Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili.
[9]Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu.
[10]Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye.”
Halikadhalika tunamsoma pia mama mmoja katika biblia ambaye alikuwa akimhudumia Elisha mtu wa Mungu, na Elisha kwa kupenda ukarimu wake alimwambia aombe neno lolote..mama huyo kwasababu hakuwa na mtoto aliomba apate mtoto, na kweli baadaye alikuja kupata mtoto wa kiume kama Elisha alivyomtamkia kwa Neno la Bwana, sasa mtoto huyo siku moja aliumwa kichwa na akafa, na kilichotokea ni kwamba huyo mwanamke alimwambia mumuwe amtaharishie punda na mtumishi mmoja, ili kumwendea Elisha mtu wa Mungu.. lakini mumewe alitaka kumpotezea muda kwa kumwambia maneno ya kumkawisha kawaisha kama yule Mlawi alivyofanywa, akaanza kumwambia kuwa leo haifai uende, leo ni sabato? leo ni mwezi mpya, kwanini usiende kesho? tunasoma biblia huyo mama hakutaka kupotezewa muda.. alipanda punda na mtoto wake.. akamwambia huyo mwendesha punda..mwendeshe tena kwa haraka na usinipunguzie mwendo nisipokuambia, Tusome…
2 Wafalme 4:8 Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.
[9]Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.
[10]Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.
[11]Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala.
[12]Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake.
[13]Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe.
[14]Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee.
[15]Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni.
[16]Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo.
[17]Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.
[18]Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao.
[19]Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake.
[20]Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa.
[21]Mamaye akapanda juu, akamlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, akamfungia mlango, akatoka.
[22]Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja, ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, nikarudi tena.
[23]Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno.
[24]AKATANDIKA PUNDA, AKAMWAMBIA MTUMISHI WAKE, MWENDESHE, TWENDELEE MBELE. USINIPUNGUZIE MWENDO, NISIPOKUAMBIA.
Na wewe kwanini leo hii unakubali kupotezewa muda wako wa kwenda kumwabudu Mungu wako aliyekuumba? Kwanini unaruhusu hiyo kazi ikupotezee muda? Kwanini unaruhusu hicho kitu unachokifanya ikupotezee muda wa kukaa uweponi mwa Baba. Angalia masaa 24 unafanya kazi lakini hata saa moja ya Mungu hupati! siku 7 unafanya kazi lakini hata siku moja ya Mungu hupati? Unaweza kukesha usiku kufanya mambo yako lakini hata masaa mawili huwezi kukesha kumwabudu Mungu!
Kuwa makini sana na muda? Kuwa makini na watu unaoishi nao iwe ni shuleni, kazini n.k angalia wasikipotezee muda, huo muda ambao unakaa na kupiga nao soga ungepaswa ukaombe, au ukasome Neno, kumbuka adui anatafuta kukupotezea muda ili ukae mbali na Mungu halafu akunase.
Usikubali kitu chochote kikupotezee muda wa kumwabudu Mungu maana tumeumbwa kwa kusudi hilo, hivyo weka mipaka kwa kila kitu ufanyacho, usikubali kazi iwe ni sababu ya wewe kukaa mbali na Mungu, wakati mwingine adui hutumia hiyo kukupotezea muda. Hivyo ukiona hiyo kazi haikupi muda wa kumtafuta Mungu ipasavyo kila siku, ukiona hupati hata lisaa limoja kukaa uweponi mwa Mungu.. kusoma Neno lake na kuomba au kwenda ibadani..hebu angalia hiyo kazi kwa jicho lingine, jiulize je! ni mapenzi ya Mungu kweli wewe kukosa muda wa kumwabudu Mungu wako?
Na ikiwa hujaokoka bado, fahamu kuwa shetani anakupotezea muda kwa hicho unachokitafuta kwanza na kusema nitaokoka baadaye, kwani biblia inasema saa ya wokovu ni sasa na sio baadaye!
2 Wakorintho 6:2(Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)
Saa ya wokovu ni sasa unaposoma ujumbe huu..leo chukua maamuzi sahihi ya kumpokea Yesu kweli kweli kabla mlango wa wokovu haujafungwa kwako, maana wakati huo utakuja kutafuta kwa vilio na usiupate. Wokovu sasa unapatikana bure..unachopaswa kufanya ni kudhamiria tu kuacha dhambi kabisa na kuacha ulimwengu kisha unaenda kubatizwa kwa ubatizo sahihi na baada hapo unaendelee na safari ya kwenda mbinguni kwa kuukomboa wakati.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.