
USIKUBALI KUTUMAINISHWA KWENYE DHAMBI
Jina la Bwana libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia..
Hatari kubwa iliyopo katika siku hizi za mwisho ni Kunyanyuka kwa jopo kubwa la Manabii wa Uongo ambao kazi yao ni kuwatumainisha watu waendelee kuishi katika dhambi na mwisho wa siku wakose mbingu…
Sasa biblia inapotaja uwepo wa manabii wa uongo, haimaanishi tu manabii bali hata waalimu, wainjilisti, mitume, wachungaji, maaskofu, mashemasi(2Petro 2:1) n.k…Yaani kwa ufupi kila karama ina waongo wake…Sasa watumishi wote hao wa uongo biblia imewapa jina moja la ujumla ambalo ndio hilo MANABII WA UONGO.
Kwahiyo akitokea mwalimu anafundisha uongo huyo ni Nabii wa Uongo wa siku za mwisho, kadhalika akitokea mchungaji anafundisha uongo huyo pia ni Nabii wa uongo kulingana na Biblia.
Sasa katika siku hizi za mwisho wameongezeka sana…Ni sababu gani imewafanya waongezeke kwa kasi kiasi hicho?? NI KWASABABU HIZI NI SIKU ZA MWISHO! HILO TU!..Hawajataka wenyewe kunyanyuka kwa nguvu zao hapana! bali kuna nguvu ya siku hizi za mwisho ndio zinazowanyanyua.
Na kazi yao kubwa ni kukuzuia USIURITHI UZIMA WA MILELE!!!!. Hilo tu!!
Ndio hapo watakutumainisha na mafundisho yao ya faraja uendelee kwenda kanisani na bado dhambi ipo ndani yako, hawakuambii ukweli wote ila watakuambia ukweli nusu.
Siku moja nilisikia bwana mmoja ambaye ni mchungaji wa kanisa fulani kubwa tu, nilikuwa nafuatilia mafundisho yake kwenye redio, nikasikia akifundisha somo fulani ambalo lilikuwa linawafuta usikivu wa watu wasilikilize kwa umakini sana.
Lakini nilipoendelea kumsikiliza, nikajikuta napata huzuni moyoni kwa kitu nilichosikia akisema, nikazima redio hapo hapo.
Na papo hapo Bwana akanipa hili andiko..
2 Petro 2:19 wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.
Kwahiyo hawa wanawahidia watu uhuru, kumbe nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu.
Watakuambia Mungu haangalii mwili anatazama roho, kwahiyo we vaa tu utakavyo, jipambe kwa kila aina ya pambo umpendeze mumewe.
Watakazana kufundisha na kuhubiri namna ya kupata pesa!. Namna yakufunguliwa kiuchumi, namna ya kutoka kimaisha..Lakini kamwe hawatafundisha namna ya kutoka kwenye dhambi!!. Wana macho ya kuona kesho utaolewa, lakini hawana macho ya kuona kesho utakwenda jehanamu kama usipotubu. Wanaona maono ya wewe Kesho yako itakuwa ni ya kicheko, lakini hawaona maono kuwa Kesho yako itakuwa ni kilio na kusaga meno kama utaendelea kuishi na huyo mke ambaye si wa kwako, na huyo mume ambaye si wa kwako, na huo ulevi ambao unaufanya sasa, na hizo biashara haramu ambazo unazifanya sasa.
Yeremia 23:16 “Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.
17 Daima huwaambia wao wanaonidharau, Bwana amesema, MTAKUWA NA AMANI; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.
21 Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri”.
Epuka kusikiliza injili hizi za manabii wa uongo, wanaokufariji katika dhambi, lakini hawakuambii ukweli kuwa, ukiendelea na Maisha ya dhambi unayoishi utakwenda kuzimu. Manabii hao ni asili yao ni kuzimu, na siku ile watu wengi sana watashangaa kuwaona Jehanamu.
Huu si wakati wa kuziamini kila roho zinazokutabiria mafanikio tu, na wala hazijali hatma ya maisha yako baada ya kifo, zichunguze sana, leo zitakutabiria utajifungua mapacha, kesho zitakutabiria utajenga nyumba, mwezi ujao zitakutabiria faraja za ajabu, lakini hazitakutabiria madhara ya dhambi baada ya kifo, hazitakutabiria madhara ya sanamu ndani ya moyo wako,hazitakutabiria Neno la Yesu linalosema “ukiwa vuguvugu nitakutapika”
Biblia inasema mbingu na nchi zitapita lakini maneno ya Mungu hayatapita kamwe, Bwana alisema dunia itaangamizwa, ni kweli itaangamizwa, alisema ufalme wa mbinguni umekaribia ni kweli umekaribia, alisema kutakuwa na dhiki kuu, ni kweli dhiki kuu lazima ije, alisema yupo mlangoni kurudi, ni kweli yupo mlangoni, alisema tujiepushe na hichi kizazi cha ukaidi kilichopotoka, na alisema pia “hakuna mtu atakayemuona yeye asipokuwa mtakatifu” Waebrania 12:14.
Je! wewe leo umejiwekaje?. Ni matumaini yangu utaanza kuufanya wito wako na uteule wako imara kuanzia sasa, na kuacha kujitumainisha na mafundisho ya faraja ya hao wanabii wa uongo ambao wapo wengi duniani. Na kuanza pia kutazama siku za vilio ambazo nazo zinakuja mbeleni.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.