Usikubali kuvuliwa Mavazi na Ibilisi

Biblia kwa kina No Comments

Usikubali kuvuliwa Mavazi na Ibilisi

Shalom mtu wa Mungu.. jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe sana. Karibu tuongeze ufahamu katika Elimu ya ufalme wa Mungu.

Maandiko yanasema katika..

Wakorintho 2: 9 ”Maana naliandika kwa sababu hii pia, ili nipate bayana kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote.

[11] Shetani asije akapata kutushinda; KWA MAANA HATUKOSI KUZIJUA FIKIRA ZAKE.

Ukikosa kuzijua fikira/hila za shetani..basi umekwenda na maji, biblia inatuonyesha kuwa shetani ni muongo na baba wa huo, hivyo hujigeuza na kuwa kama malaika wa nuru ili apate kuwanasa wale wenye hekima ya Mungu.

Moja ya ajenda ya shetani kwa sasa ni kuwavua watu mavazi yao na kuwaacha uchi, na hili amelifanikisha kwa kiasi kikubwa.. na hii alianza kidogo kidogo kwa kuingiza kitu kinachoitwa fashion.

Sasahivi unaweza ukatembea barabarani ukakutana na mtu anatembea uchi kabisa..halafu atakuambia ni fashion, wanawake na wanaume wanatembea na nguo za ndani..na wanasema ni fashion wapo kwenye dunia iliyoendelea. Sasa shetani hajaanza tu kuwavua nguo zote kwa wakati mmoja, alianza kwa kuvua sehemu moja ya mwili baada ya nyingine na hatimaye mwili wote ukabaki bila mavazi. Alianza miguuni akaleta fashion za gauni za mipasuko ya chini..na baadaye akapasua mpaka mwisho..halafu akaendeleza na mgongo wazi, na kisha akaanza juu tena..akaja na mabega wazi, kifua wazi, tumbo wazi na hatimaye mwili wote.

Ndivyo hatua za kuvuliwa Mavazi ilivyoanza namna hiyo, na kwasababu alianza kumvua yale ya rohoni..basi mtu huyo haoni tena kuwa yupo uchi. Ni hatari sana.

Hivyo, hata sasa katika kanisa ajenda kubwa ya shetani inayoendelea ni kuwavua wakristo mavazi yao, na ili afanikishe kama alivyofanya kwa ulimwengu ni kuwavua kidogo kidogo, ndivyo anavyofanya ndani ya kanisa. Yapo mavazi ya ukristo ambayo kila mkristo ni lazima awenazo, yapo mavazi ya nje na ndani ambayo zote zinatengeneza vazi kuu (UTAKATIFU) ambalo bila kuwa na hilo vazi kuona mbingu ni hadithi tu.

Mavazi ya nje ni mwonekano wako wote wa nje kwa ujumla,. jinsi unavyojistiri, na vitu unavyoweka kwenye mwili wako, na matendo unayoyatenda kupitia mwili wako.

Vilevile mavazi ya ndani, ni mambo yaliyo moyoni mwako, mambo ambayo kwa nje hayawezi kuonekana, kwa ujumla matendo yote ya rohoni yanayompendeza MUNGU ikiwemo kuomba, kutoa sadaka (Mathayo 6:4), kumwabudu Mungu katika roho, kujifunza na kutafakari Neno la Mungu, vile vile upendo, uvumilivu, utu wema, kiasi.

Wakolosai 3:12 “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa REHEMA, UTU WEMA, UNYENYEKEVU, UPOLE, UVUMILIVU,

13 mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

14 Zaidi ya hayo yote JIVIKENI UPENDO, ndio kifungo cha ukamilifu”.

Hapo Biblia inatumia neno “JIVIKENI” Ikiwa na maana kuwa mambo yafuatayo yanafananishwa na mavazi.. na anayataja pale kuwa ni moyo wa Rehema, Utu wema, Unyenyekevu, Upole, Uvumilivu na mwisho anamaliza na Upendo,

Kwahiyo hayo ndio mavazi tunayopaswa kuyavaa katika utu wetu wa ndani kila siku, na utaona pia yamerudiwa katika Wagalatia 5:22 kama matunda ya roho, na mengine baadhi kuongezeka.

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Kwahiyo shetani anachokifanya kwa mkristo wa kweli ambaye amevaa mavazi yote ya nje na ndani..ni kufanya kila juhudi ili aweze kumvua hayo mavazi yake na kisha ammalize kabisa. Na kama tulivyoona anaanza kumvua mtu kidogo kidogo..sio kwa wakati mmoja maana ni vigumu…ataanza kidogo kidogo pasipo huyo mtu kujua na hatimaye anajikuta yupo uchi bila hata kujua. Ndio maana hatukosi kuzijua hila zake.

Sasa, yapo mambo makuu matano ambayo ni kama vifungo/vishikilio au mkanda unaoshikilia mavazi mengine kwenye mwili ambao shetani akifanikisha tu kuviondoa hayo mambo..basi mavazi mengine ni lazima tu yadondoke zenyewe. Ni kama tu kuvaa shati lisilo na vifungo au vazi la kiunoni bila mkanda vazi lote litashuka tu. Na sio ajabu ndio maana Bwana Yesu alisema..

Luka 12:35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

Hivyo wewe kama mwamini..huna budi kuahikikisha unayashikilia haya mambo makuu matano pasipo kupunguza kuvifanya hata kidogo, maana ndio mkanda wako unaoushikilia vazi lako kuu la utakatifu..na adui anafanya kila mbinu akuvue.. Hivyo zingatia sana..

1 MAOMBI

Hii ndio kifungo kikuu ambayo shetani anawinda sana ili akuvue, hivyo hupaswi kabisa kufanya kosa la kupunguza kuomba…Ni heri ukapunguza muda wa kufanya mambo mengine ambayo unaona ni ya muhimu lakini usipunguze kuomba hata kidogo!..Kama tayari ulishaanza kuwa muombaji, halafu ukaanza kupunguza unamtengenezea adui nafasi ya kukuvua mavazi yote.

Ukiona umepunguza kuomba jua tayari mkanda umeanza kulegea, kumbuka shetani anaanza kidogo kidogo.

Maombi yanafananishwa na lile tukio la Nabii Musa, aliponyoosha mikono yake juu wakati wa vita…alipoionyoosha juu wana wa Israeli kule vitani walikuwa wanapata nguvu ya kuwapiga maadui zao na kuwashinda…lakini alipoishusha nguvu ziliwaondokea wana wa Israeli na kuhamia kwa adui zao na kuwashinda wana wa Israeli..Na sisi ni hivyo hivyo nguvu za Mungu zinashinda juu ya Maisha yetu dhidi ya nguvu za Adui endapo tu na sisi kila siku/kila wakati tutakuwa tumeinyanyua mikono na mioyo yetu juu kuomba.

Hivyo usiache wala usipunguze kuomba kabisa!..na kumbuka ndugu kuomba sio sala ile ya kuombea chakula!..au sio ile sala la “Baba yetu”…Hiyo haitoshi…kiwango cha chini kabisa biblia imetuambia angalau lisaa limoja kwa siku, ukienda masaa 3 au 4 ni vizuri Zaidi…na pia maombi sio kwenda kuombewa na mtumishi Fulani wa Mungu au ndugu yako!!..Maombi ni wewe kama wewe kusimama mwenyewe kuomba kwa bidii!.

Kumbuka, shetani anashida na wokovu wako, anafanya kila namna akuvue huo utakatifu ili usiende kumuona Mungu, wakati mwingine anatumia matatizo kadha wa kadha, watu mbali mbali na mapepo yake, atakuletea kazi nyingi ili ahakikishe kuwa hupati muda wa kuomba, hivyo kidogo kidogo ataanza kukuondolea hii kifungo kikuu na baadaye vifungo vingine vinakuwa rahisi kwake.

Hivyo ng’oa nanga leo anza safari ya maombi ya kina kila siku!..kama umerudi nyuma rudia desturi yako kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya.

2. KUSOMA NENO

Hichi ni kifungo kingine ambacho shetani akikiondoa, ni kama vile ametoka kuvua sehemu za miguuni anaendelea na sehemu nyingine ya juu.

3 MIFUNGO

Kuomba na kufunga kunapaswa kuwe ni desturi kwa mkristo, hupaswi kabisa kupunguza au kuacha kufunga, ukiacha kufunga na kuomba tayari umempa ibilisi nafasi kubwa.. hivyo hapa unapaswa kabisa kujikana nafsi.. maana wakati mwingine shetani atakuletea vyakula vingi vingi ili akutege, zipo faida nyingi sana katika maombi ya mifungo hasa yale ya masafa marefu…unapoingia kwenye maombi ya mifungo katika roho unaonekana umekaza mkanda wako..na hivyo huwezi kamwe kuvuliwa Mavazi yako.

4 USIACHE WALA USIPUNGUZE USHIRIKA

Maandiko yanasema..Waebrania 10:25 “WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Kukusanyika kunakozungumziwa hapo, ni kukusanyika na wapendwa wengine kanisani.

Mbinu ya kwanza shetani anayoitumia kuwavua wakristo mavazi yao na kuwaangusha ni kuwatoa katika kundi!..(kuwatenga na kundi), atanyanyua kisa tu , ambacho kitamfanya huyo mtu akereke na aache kwenda kanisani. Na yule mtu kwa kudhani kuwa “kujitenga na wenzake, ndio atakuwa salama, kumbe ndio kajimaliza”.

Unaweza kusema nikiwa peke yangu, ninaweza kusimama… lakini nataka nikuambia..mtu anayelala hajui dakika aliyoingia usingizini, vile vile mtu aliye pekee yake siku za kwanza atajiona nafuu lakini ndivyo anavyozidi kupoa kidogo kidogo na mwisho kupotea kabisa..

Hebu soma maneno haya…

Mhubiri 4:9 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.

10 KWA MAANA WAKIANGUKA, MMOJA WAO ATAMWINUA MWENZAKE; LAKINI OLE WAKE ALIYE PEKE YAKE AANGUKAPO, WALA HANA MWINGINE WA KUMWINUA!

11Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?

12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi”.

Hivyo usiache kamwe kukusanyika Pamoja na wengine, kwasababu kuna vitu ambavyo ukiwa peke yako inakuwa ni ngumu kuvipata, mfano wa vitu hivyo ni Faraja, ari, motisha, hamasa,.. Na vile vile kuna vitu ambavyo ukiwa peke yako ni ngumu kuvifanya kikamilifu.. Mfano wa vitu hivyo ni maombi!.. ukiwa mwenyewe nyumbani ni ngumu kukesha kuomba.. lakini ukiwa kwenye mkesha mahali ambapo watu wote wanaomba.. ukitazama kushoto Jirani anaomba, ukitazama kulia mwingine anaomba ni lazima na wewe utapata nguvu ya kuomba.. lakini nyumbani peke yako ni ngumu.

Hiyo ni hekima ya kiMungu, hivyo usijione unayo hekima kuliko Mungu..

Hivyo ndugu, usikubali kuvuliwa Mavazi yako na ibilisi, fahamu kuwa tumekaribia nyumbani kwa Baba, na pasipo kuwa na mavazi hayo hatuwezi kuingia kwake.. ndivyo biblia inavyotuambia..

Ufunuo wa Yohana 19:7-9 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

[8]Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.

[9]Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.

Usikubali kitu chochote kiwe ni sababu ya wewe kukosa mbingu, iwe ni kazi, elimu, marafiki, ndugu, mume/mke n.k tunaishi ukingoni kabisa mwa siku za mwisho na Bwana wetu yupo mlangoni. Na shetani analijua hilo hivyo anafanya kila namna atukoseshe mbingu.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *