
USINIPUNGUZIE MWENDO.
Tukiwa bado tupo mwanzo wa mwaka, ni wakati wa kushika sana vile tulivyo navyo na kuendelea mbele, wala si wakati wa kurudi nyuma kabisa au kupunguza mwendo uliokuwa nayo.
Ulikuwa upo mbali na anasa mwaka jana, basi huu mwaka unapasawa kwenda mbali zaidi, ulikuwa umejitenga na mambo ya kiulimwengu mwaka jana, mwaka huu usipunguze huo mwendo kabisa…zidi kujitakasa na kukaa mbali na ulimwengu.
Ulikuwa umekaa mbali na vichocheo vyote vya dhambi kama usinzi, uasherati, ulevi, mizahaa n.k basi huu mwaka huna budi kupiga mbio zaidi na kusema..
“… Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia.” (2Wafalme4:24)
Usikubali mtu au kitu chochote kikupunguzie mwendo wa kumtafuta Mungu.
Usikubali rafiki, mchumba, mke/mume, mzazi au ndugu, usikubali kazi, shule, n.k
Paulo akijua kuwa anakaribia ukingoni kabisa mwa safari yake, hakujali taarifa yoyote mbaya iliyoletwa mbele yake, utaona yeye mwenyewe anasema, mji kwa mji Roho Mtakatifu alimshuhudia kuwa vifungo na dhiki nyingi vinamngojea kule Yerusalemu alipokusudia kwenda, lakini bado alisema, siachi kupiga mbio nimalize mwendo wangu.
Matendo20:23 “isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.
24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama KUUMALIZA MWENDO wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu”.
Paulo alikuwa ni mtu mwenye malengo, ni mtu aliyekuwa anatazama vya mbali sana, alijua kupiga mbio huko kuna tuzo Fulani kubwa mbeleni, hivyo ni sharti aishindanie kwa nguvu ili asiikose.
1Wakorintho 9:24 “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? PIGENI MBIO NAMNA HIYO, ILI MPATE.
25 Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.
26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.
26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;
27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”
Unaona alijua sikuzote mkimbiaji ambaye anajua lengo la kukimbia kwake ni nini huwa hakimbii kwa kuubembeleza mwili, bali anakimbia huku mawazo yake yakuwa kweney tuzo iliyowekwa mbele yake, hilo ndilo linalomfanya asitembee tembee njiani, asikubali kuusikiliza mwili, kwamba umechoka, hivyo apunguze mwendo.
Hali kadhalika mkimbiaji mzuri kwa namna ya kawaida, anapokaribia mzunguko wake wa mwisho ndio huwa anaongeza mwendo Zaidi, na ndicho alichokifanya Paulo.
Embu tumtazame mtu mwingine wa mwisho ambaye safari yake sikuzote ilikuwa ni ya mwendo tu, mtu ambaye yeye hakujali kikwazo chochote alipokuwa anamalizia mwendo wake hapa duniani. Na huyo si mwingine Zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Biblia inatuambia wakati wa kupaa kwake ulipokaribia, “ALIUKAZA” uso wake kwenda Yerusalemu.
Luka 9:51 “Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;
52 akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.
53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu”.
Kuukaza uso maana yake, ni kutokuwa tayari kuambiwa chochote, au kushauriwa chochote au kukwamishwa na chochote mpaka utimize malengo yako uliyoyakusudia mbele yako. Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu, wakati ambapo anajua amebakiwa na kipindi kifupi sana, amalize mwendo wake pale Yerusalemu, huku akijua moyoni mwake kuwa Mateso makali anakwenda kukumbana nayo, kusulibiwa, yeye hakujali chochote, Zaidi ndio alilazimisha kwenda huko huko.
Na sisi kipindi hichi cha kufunga majira, hatuna budi kuendelea kupiga mbio, huu sio wakati wa kupunguza mwendo wa Imani, usipunze mwendo wa maombi, usipunze mifungo, mikesha, kushudia, kusoma biblia.
Hizi ndizo nyakati za kuzidisha mwendo, kutojali vitisho vyovyote vya kiimani, vitisho vya ndugu, au rafiki, au majirani, kwasababu kama unyakuo hautatukuta, basi pia siku zetu za kuishi duniani zinapungua siku baada ya siku, mwaka baada ya mwaka.
Hivyo tupige mbio tukijua kuwa zipo tuzo mbele yetu zinatungojea, lakini tukiwa walegevu hatutazipata.
2Timotheo 2:5 “Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali”.
Shalom.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.