Vitu vitano ambavyo hupaswi kupunguza kabisa katika safari ya imani

Uncategorized No Comments

Vitu vitano ambavyo hupaswi kupunguza kabisa katika safari ya imani.

Jina la Bwana Yesu Kristo libarkiwe milele na milele.

Ikiwa we ni mkristo wa kweli, vipo vitu vitano ambavyo hupaswi kabisa kupunguza katika safari yako ya wokovu.

Kwanza jambo ambalo unapaswa kufahamu ni kuwa wokovu ambao tumeupokea bure kwa neema ya Yesu Kristo Bwana wetu ni wa kushikililia sana kwa umakini kama vile mtu anayebeba mayai.

Kwanini, ni kwasababu Bwana aliingia gharama kubwa sana ili mimi na wewe tupate huu wokovu, ndio maana maandiko haya yanasema..

Waebrania 2:3 sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia;

Watu ambao wanaambiwa hayo maneno sio watu wa kidunia waliokataa wokovu, bali ni mimi na wewe ambaye tumeitwa tuwe watakatifu na tukatii wito.

Hivyo, wokovu ni jambo la kushikilia sana kwa umakini, ni jambo la kuitetemekea na kuogopa kama tulivyoambiwa katika..

Wafilipi 2:12 Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

Sasa, yapo mambo manne ambayo, mimi/wewe kama mkristo huna budi kuendeleanazo katika safari ya imani pasipo kupungusa hata kidogo.

Kumbuka, tunaposema mkristo, hatusemi tu mkristo ili mradi mkristo, hatulengi wakristo vuguvugu au wakristo jina, hatulengi wakristo wa madhehebu, hapana, hapa tunalenga mtu ambaye ameokoka kweli kweli, Mtu ambaye amesikia Injili na akatubu dhambi na kuacha kabisa kabisa na akabatizwa katika ubatizo sahihi, akapokea Roho Mtakatifu..huyu ndiye mkristo ambaye tunamlenga hapa.

Hivyo, ikiwa wewe ni mkristo wa kweli, zingatia yafuatayo ili ukristo wako uimarike, mambo haya ni lazima uvifanye kuwa desturi kwako.

1 MAOMBI

Katika safari ya imani usijaribu kabisa kufanya kosa la kupunguza maombi…Ni heri ukapunguza muda wa kufanya mambo mengine ambayo unaona ni ya muhimu lakini usipunguze kuomba hata kidogo!..Kama tayari ulishaanza kuwa muombaji, halafu ukaanza kupunguza unamtengenezea adui nafasi ya kufanya uharibifu mkubwa sana katika maisha yako na hatimaye kukurudisha nyuma.

Ukiona umepunguza kuomba jua tayari umeanza kurudi nyuma kiimani…hiyo ni dalili ya kwanza, dalili ya pili ni kupunguza kusoma neno.

Maombi yanafananishwa na lile tukio la Nabii Musa, aliponyoosha mikono yake juu wakati wa vita…alipoionyoosha juu wana wa Israeli kule vitani walikuwa wanapata nguvu ya kuwapiga maadui zao na kuwashinda…lakini alipoishusha nguvu ziliwaondokea wana wa Israeli na kuhamia kwa adui zao na kuwashinda wana wa Israeli..Na sisi ni hivyo hivyo nguvu za Mungu zinashinda juu ya Maisha yetu dhidi ya nguvu za Adui endapo tu na sisi kila siku/kila wakati tutakuwa tumeinyanyua mikono na mioyo yetu juu kuomba…Hizo ni faida chache tu za maombi zipo nyingi hatuwezi kuwa na muda wa kuzichambua zote hapa.

Hivyo usiache wala usipunguze kuomba kabisa!..na kumbuka ndugu kuomba sio sala ile ya kuombea chakula!..au sio ile sala la “Baba yetu”…Hiyo haitoshi…kiwango cha chini kabisa biblia imetuambia angalau lisaa limoja kwa siku, ukienda masaa 3 au 4 ni vizuri Zaidi…na pia maombi sio kwenda kuombewa na mtumishi Fulani wa Mungu au ndugu yako!!..Maombi ni wewe kama wewe kusimama mwenyewe kuomba kwa bidii!.

Kumbuka, shetani anashida na wokovu wako, ana shida na Maisha yako na sio hata kwa njia ya uchawi au kwa kuwatumia wachawi…anayo idadi kubwa ya mapepo kuliko wachawi..hivyo kazi zake nyingi anatumia mapepo yake kuzifanya hata zaidi ya wachawi….asilimia kubwa sana ya watu wanasumbuliwa na mapepo wakidhani ni wachawi!

Hivyo ng’oa nanga leo anza safari ya maombi ya kina kila siku!..kama umerudi nyuma rudia desturi yako kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya.

2 KUSOMA NENO

Kusoma Neno kunazidisha Ujazo wa Roho Mtakatifu Ndani Yetu..lakini pia ndio Chakula kikuu cha Roho zetu. Bila NENO ni sawa na mwili bila chakula, huawezi kuishi.

Mathayo 4:4 ”Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu”.

> Kusoma biblia ndiko kunakoweza kukukuza kiroho, (1Petro 2:2,),

> Pia ndipo unapoweza kufanywa upya ufahamu wako (Warumi 12:12).

> Lakini pia Ndani ya biblia kuna unabii wa maisha yako, kuna faraja, Kuna maonyo, kuna mashauri na miongozo (Zaburi 119:105).

Hivyo hakuna Namna mtu atayatenganisha maisha ya wokovu na usomaji Neno.

3 MIFUNGO

Kuomba na kufunga kunapaswa kuwe ni desturi kwa mkristo, hupaswi kabisa kupunguza au kuacha kufunga, zipo faida nyingi sana katika maombi ya mifungo hasa yale ya masafa marefu hatuwezi kuzitazama zote hapa,

Kwa jinsi unavyozidi kuenendelea kufunga kwa siku nyingi, ndivyo utakavyozidi kuwa mwepesi katika mambo ya rohoni.

Musa alifanikiwa kufunga siku 40 asiku na mchana bila kula, na sote tunajua ni nini alipata kule mlimani..Mungu alizungumza naye uso kwa uso, na kumpa zile Amri 10, Vivyo hivyo hata kwa Eliya naye alipofunga siku 40, Mungu alisema naye kwenye ule ule mlima wa Musa..

Halikadhalika na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, yeye pia alifunga siku 40 usiku na mchana bila kula chochote, mpaka ibilisi akatokea kumjaribu na kushindwa na aliposhuka kule mlimani alishuka na nguvu nyingi za Roho Mtakatifu ndipo akaanza kuhubiri injili na kuponya wangojwa katika Israeli yote.

Hivyo mifungo ya muda mrefu inafaa sana.

Faida nyingine ya kufunga inakusaidia kushusha chini matamanio ya mwili. Kwa kuwa chakula kinakuwa hakina sehemu kubwa katika mwili kwa wakati huo, hivyo hata kazi za uzalishaji wa homoni, zinapungua na hivyo inamfanya yule mfungaji awe katika hali ya utulivu Zaidi katika kumtafuta Mungu.

Biblia inatuambia pia, ukifunga, Mungu anakupa thawabu, Hiyo ni kuonyesha kuwa Mungu anathamini kujitesa kwetu kwa ajili yake.(Mathayo 6:16)

4 USIPUNGUZE KUSHUHUDIA

Agizo kuu ambalo Bwana alilotupatia ni kupeleka injili ulimwenguni kote.

Marko 16:15 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”.

Unaposhudia habari ya Kristo kwa wengine unazidi kuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu yako na hivyo unazidi kujengwa na kuimarika katika imani.

Kwasababu kila tunapofika mahali na kushuhudia tunafanyika vyombo vya Roho Mtakatifu, Hivyo Roho Mtakatifu hana budi kila wakati kuwa nasi kwasababu wakati wote tunatumika kama vyombo vyake, hakuna wakati uwepo wake utakaa mbali na sisi!..

Mathayo 10:18 “nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.

19 Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.

20 KWA KUWA SI NINYI MSEMAO, BALI NI ROHO WA BABA YENU ASEMAYE NDANI YENU”.

Kwahiyo kama wakati wote tutakuwa katika hayo mazingira ya kumshuhudia Kristo, maana yake wakati wote, kinywa kitakachokuwa kinasema ndani yetu ni kinywa cha Roho Mtakatifu, hivyo uwepo wake utakuwa nasi muda wote!, lakini kama hatutakuwa katika mazingira yoyote ya kumshuhudia Kristo ni ngumu Roho Mtakatifu kuwa na sisi, kuzungumza kupitia vinywa vyetu, au kusema nasi, hivyo usipunguze kabisa kushudia na kuhubiri Injili ya Bwana..kwa maana ndio sababu ya kuendelea kuishi duniani baada ya kuokoka.

5 USIACHE WALA USIPUNGUZE USHIRIKA

Maandiko yanasema..Waebrania 10:25 “WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Kukusanyika kunakozungumziwa hapo, ni kukusanyika na wapendwa wengine kanisani.

Mbinu ya kwanza shetani anayoitumia kuwaangusha watu, ni kuwatoa katika kundi!..(kuwatenga na kundi), atanyanyua kisa tu , ambacho kitamfanya huyo mtu akereke na aache kwenda kanisani. Na yule mtu kwa kudhani kuwa “kujitenga na wenzake, ndio atakuwa salama, kumbe ndio kajimaliza”.

Unaweza kusema nikiwa peke yangu, ninaweza kusimama… lakini nataka nikuambia..mtu anayelala hajui dakika aliyoingia usingizini, vile vile mtu aliye pekee yake siku za kwanza atajiona nafuu lakini ndivyo anavyozidi kupoa kidogo kidogo na mwisho kupotea kabisa..

Hebu soma maneno haya…

Mhubiri 4:9 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.

10 KWA MAANA WAKIANGUKA, MMOJA WAO ATAMWINUA MWENZAKE; LAKINI OLE WAKE ALIYE PEKE YAKE AANGUKAPO, WALA HANA MWINGINE WA KUMWINUA!

11Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?

12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi”.

Hivyo usiache kamwe kukusanyika Pamoja na wengine, kwasababu kuna vitu ambavyo ukiwa peke yako inakuwa ni ngumu kuvipata, mfano wa vitu hivyo ni Faraja, ari, motisha, hamasa,.. Na vile vile kuna vitu ambavyo ukiwa peke yako ni ngumu kuvifanya kikamilifu.. Mfano wa vitu hivyo ni maombi!.. ukiwa mwenyewe nyumbani ni ngumu kukesha kuomba.. lakini ukiwa kwenye mkesha mahali ambapo watu wote wanaomba.. ukitazama kushoto Jirani anaomba, ukitazama kulia mwingine anaomba ni lazima na wewe utapata nguvu ya kuomba.. lakini nyumbani peke yako ni ngumu.

Hiyo ni hekima ya kiMungu, hivyo usijione unayo hekima kuliko Mungu..

Kwa hayo mambo makuu matano (5) na mengine zaidi ya hayo tutaweza kuilinda imani yetu ambayo tumekabidhiwa mara moja.

Yuda 1:3 Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.

Je! Umempokea Yesu kweli kweli? Unahabari kuwa UNYAKUO wa kanisa umekaribia sana?

Kama bado haujaingia ndani ya Kristo unasubiri nini mpaka sasa? vipi kama leo ndio mwisho wa maisha yako na umesikia injili mara nyingi? Jiulize utaenda kuwa mgeni wa nani huko uendako?

Basi, Saa ya wokovu ni sasa, tubu dhambi zako kwa kumaniasha kuziacha kabisa na kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa jina la Yesu Kristo sawa sawa na Matendo 2:38..na baada ya hapo, anza kuzingatia hayo mambo matano kama tulivyojifunza na mengine zaidi ya hayo.

Bwana akubariki

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *