Watajua ni Neno la Nani Litakalosimama, Neno Langu, au Neno Lao.
Yeremia 44: 28 “Nao watakaoukimbia upanga, watatoka katika nchi ya Misri, na kuiingia nchi ya Yuda, watu wachache sana; na wote wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili kukaa huko, WATAJUA NI NENO LA NANI LITAKALOSIMAMA, NENO LANGU, AU NENO LAO.”
Je! U miongoni mwa wanaoshindana na Muumba wao?
Maandiko yanasema…
Isaya 45:9 “Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?
Kama we ni msomaji wa biblia, utakumbuka Israeli na Yuda waliwahi kupelekwa utumwani huko Babeli na Ashuru kwasababu ya makosa yao. Mwanzoni kabisa mfalme wa Ashuru alienda huko Samaria akawachukua Israeli mpaka Ashuru, wakasalia upande wa Yuda ambao nao baadaye walikuja kuchukuliwa na mfalme wa Babeli.(kumbuka Israeli zamani ilikuwa imegawanyika)
Sasa kipindi mfalme wa Babeli (Nebukadreza) anakuja kuwachukua Yuda… alikuja kwa awamu tatu, awamu ya kwanza alikuja kipindi cha utawala wa Yehoyakimu, ambapo katika kundi hili ndipo walikuwepo akina Danieli na wale wenzake…Awamu ya pili ni kipindi cha utawala wa Yekonia mwana wa Yehoyakimu, katika kundi hili ndipo alikuwepo Nabii Ezekieli, na awamu ya tatu ilikuwa chini ya utawala wa Sedekia, awamu hii ilikuwa mbaya zaidi kwani watu wengi waliuliwa kikatili na wengi walikufa kwa njaa na tauni baada ya kuzungukwa kwa muda mrefu na jeshi la Wakaldayo(Babeli) ilikuwa hakuna kutoka nje ya mji. Ndicho kipindi ambacho nyumba ya Mungu (Ile Hekalu la Sulemani) ilibomolewa, ikateketezwa kabisa na vyombo vyote vilichukuliwa, na watu wengi kuuliwa.
Sasa baada ya watu wengi kuuliwa kama kuku na wengine kuchukulia mateka, kulikuwa na kundi ndogo la watu walio dhaifu, ambalo lilibakizwa kwa ajili ya kutunza ardhi isibaki ukiwa.
Hayo yote yalitokea kwa sababu ya makosa yao wenyewe.. ijapokuwa Mungu aliwavumilia sana kwa muda mrefu huku akiwatuma watumishi wake kuwaonya waachane na ibada za miungu na uchafu waliokuwa wakifanya ila hawakutaka kusikia, waliwaua wale watumishi wa Mungu kama akina Isaya..walizidi kufanya machukizo mengi, Hata kusiwepo na nafasi ya kuponywa tena. (2Mambo ya Nyakati 36)
Sasa lile kundi dogo lililobaki..lilimfuata Yeremia Nabii na kumwambia…
Yeremia 42:1-19 “Ndipo maakida wote wa majeshi, na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hoshaya, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, wakakaribia,
2 “wakamwambia Yeremia, nabii, Twakusihi, maombi yetu yakubaliwe mbele yako, ukatuombee kwa BWANA, Mungu wako, yaani, watu hawa wote waliosalia; maana tumesalia wachache tu katika watu wengi, kama macho yako yatuonavyo;
3 ili kwamba BWANA, Mungu wako, atuonyeshe njia ambayo yatupasa tuiendee, na jambo litupasalo tulitende.
4 Ndipo Yeremia, nabii, akawaambia, Nimewasikia; tazama, nitamwomba BWANA, Mungu wenu, sawasawa na maneno yenu; tena itakuwa, neno lo lote ambalo BWANA atawajibu, nitawaambia; sitawazuilia neno liwalo lote.
5 Wakamwambia Yeremia, BWANA na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo BWANA, Mungu wako, atakutuma utuletee.
6 Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya BWANA, Mungu wetu.
7 Ikawa, baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia.
8 Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa,
9 akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi;
10 Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang’oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda.
11 Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema BWANA; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake.
12 Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.
13 Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya BWANA, Mungu wenu;
14 mkisema, La! Lakini tutakwenda nchi ya Misri, ambayo hatutaona vita, wala kuisikia sauti ya tarumbeta, wala kuona njaa kwa kukosa chakula; nasi tutakaa huko;
15 basi, lisikieni neno la BWANA, enyi mabaki ya Yuda; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mwakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko;
16 basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko.
17 Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao.
18 Maana BWANA wa majeshi Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama hasira yangu, na ghadhabu yangu, ilivyomwagwa juu ya hao wakaao Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu, mtakapoingia Misri; nanyi mtakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu; wala hamtapaona mahali hapa tena.
19 BWANA asema katika habari zenu, enyi mabaki ya Yuda, Msiingie Misri; jueni sana ya kuwa nimewashuhudia hivi leo.
Hayo ndiyo maneno waliyomwambia Yeremia aseme na Mungu, na Mungu akawajibu namna hiyo, akiwaonya sana WASIENDE MISRI. Ila tunasoma baadaye walikuja kwenda kinyume na ahadi walizoziweka wenyewe kwamba tutatii kila neno la Mungu wetu tunayekutuma kwake, ikiwa ni jema au baya.
Pamoja na Mungu kuwahakikishia ulinzi katika hiyo nchi, kwamba wasimwogope mfalme wa Babeli wanayemwogopa, maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake,..tena Bwana akawaambia…
Yeremia 42:10 “Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang’oa; kwa maana najutia mabaya niliyowatenda.”
Ila hawakutii sauti ya Mungu aliyowaambia kaeni katika nchi yenu maana mimi ni pamoja nanyi, walinyanyuka na kuelekea Misri wakidhani huko watapata usalama, huko kuna kula chakula kizuri, huko kuna amani tele, ila haya ndiyo maneno ya BWANA kwa watu hao…
Yeremia 42:15 basi, lisikieni neno la BWANA, enyi mabaki ya Yuda; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mwakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko;
16 basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko.
Pamoja na maonyo mengi kwamba wasiende Misri, ila walishupaza shingo zao wakaenda, na zaidi ya yote walienda kuabudu miungu ya Misri na kuvukiza malkia wa mbinguni uvumba, na kuendelea kumkasirisha BWANA.
Ndipo Neno la Mungu lilivyomjia Yeremia Nabii ikisema…
Yeremia 44:1 Neno lililomjia Yeremia, katika habari za Wayahudi wote waliokaa katika nchi ya Misri, waliokaa Migdoli, na Tahpanesi, na Nofu, na katika nchi ya Pathrosi, kusema,
2 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ninyi mmeona mabaya yote niliyoleta juu ya Yerusalemu, na juu ya miji yote ya Yuda; na, tazama, ni ukiwa leo, wala hapana mtu akaaye ndani yake;
3 Kwasababu ya uovu wao, waliotenda ili kunikasirisha, kwa kuwa walikwenda kufukiza uvumba, na kuwatumikia miungu mingine, ambao hawakuwajua, wao, wala ninyi, wala baba zenu.
4 Tena nalituma kwenu watumishi wangu wote, manabii, nikiamka mapema na kuwatuma, nikisema, Basi ninyi; msilifanye chukizo hili linichukizalo.
5 Lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, ili wageuke na kuacha uovu wao, wasifukizie uvumba miungu mingine.
6 Kwa sababu hiyo ghadhabu ya yangu, na hasira yangu, zilimwagika, nazo ziliwaka katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, na miji hiyo imeachwa ukiwa, na kuharibika, kama ilivyo leo.
7 Basi, sasa, BWANA, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa nini mnafanya uovu huu mkubwa juu ya nafsi zenu wenyewe, kujikatilia mbali mwanamume na mwanamke, mtoto mchanga na anyonyaye, mtoke kati ya Yuda, msijiachie mtu abakiye;
8 kwa kuwa mnanikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, mkifukizia uvumba miungu mingine katika nchi ya Misri, mlikokwenda kukaa ugenini; mpate kukatiliwa mbali, na kuwa laana, na aibu, katika mataifa yote ya dunia?
9 Je! Mmesahau uovu wa baba zenu, na uovu wa wafalme wa Yuda, na uovu wa wake zao, na uovu wenu wenyewe, na uovu wa wake zenu, walioutenda katika nchi ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu.
11 Basi, kwa sababu hiyo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaelekeza uso wangu juu yenu, ili niwaletee mabaya, hata kukatilia mbali Yuda yote.
12 Nami nitawatwaa mabaki ya Yuda, waliolekeza nyuso zao kuingia nchi ya Misri, wakae huko, nao wataangamia wote pia; wataanguka katika nchi ya Misri; wataangamia kwa upanga, na kwa njaa; watakufa, tangu wadogo hata wakubwa, kwa upanga, na kwa njaa; nao watakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu.
Hayo ndiyo maneno ya Bwana kwa watu hao walioshupaza shingo zao kwenda huko Misri na kuabudu miungu, ijapokuwa walishuhudia kilichowakuta ndugu zao ila hawakujali. Walitaka kushindana na Muumba wao.
Sikia maneno wanayomjibu Yeremia mtumishi wa Mungu…
Yeremia 44:15 Ndipo watu wote waliojua ya kuwa wake zao waliwafukizia uvumba miungu mingine, na wanawake wote waliosimama karibu, mkutano mkubwa, yaani, watu wote waliokaa katika nchi ya Misri, katika Pathrosi, wakamjibu Yeremia, wakisema,
16 Neno lile ulilotuambia kwa jina la BWANA, SISI HATUTAKUSIKILIZA.
17 LAKINI BILA SHAKA TUTALITIMIZA KILA NENO LILILOTOKA KATIKA VINYWA VYETU, kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kumiminia sadaka za kinywaji, kama tulivyotenda sisi, na wakuu wetu, katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu; maana wakati huo tulikuwa na chakula tele, na kufanikiwa, wala hatukuona mabaya.
18 Lakini tulipoacha kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kumiminia sadaka za kinywaji, tumepungukiwa na vitu vyote; na kuangamizwa kwa upanga, na kwa njaa.
20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake, yaani, watu wote waliompa jibu lile, akisema,
21 Uvumba mliofukiza katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ninyi, na baba zenu, wafalme wenu, na wakuu wenu, na watu wa nchi, je! BWANA hakuwakumbuka watu hao? Je! Jambo hili halikuingia moyoni mwake?
22 Hata BWANA asiweze kuvumilia tena, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu, na kwa sababu ya machukizo mliyoyafanya; kwa sababu hiyo nchi yenu imekuwa ukiwa, na ajabu, na laana, isikaliwe na mtu kama ilivyo leo.
23 kwa sababu mmefukiza uvumba, na kwa sababu mmetenda dhambi juu ya BWANA, wala hamkuitii sauti ya BWANA, wala hamkwenda katika torati yake, wala katika amri zake, wala katika shuhuda yake; ndiyo maana mabaya haya yamewapata kama ilivyo leo.
24 Tena Yeremia akawaambia watu wote, na wanawake wote, Lisikieni neno hili la BWANA, ninyi nyote wa Yuda, mliopo hapa katika nchi ya Misri;
25 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ninyi na wake zenu mmenena kwa vinywa vyenu, na kutimiza kwa mikono yenu, mkisema, Bila shaka tutatimiza nadhiri zetu tulizoziweka, na kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kumiminia sadaka za kinywaji; basi, zithibitisheni nadhiri zenu.
26 Basi, kwa sababu hiyo lisikieni neno la BWANA, ninyi nyote wa Yuda, mnaokaa katika nchi ya Misri, Tazama, nimeapa kwa jina langu kuu, asema BWANA, ya kwamba jina langu halitatajwa tena katika kinywa cha mtu awaye yote wa Yuda, katika nchi yote ya Misri, akisema, Kama Bwana MUNGU aishivyo!
27 Tazama, nawaangalia niwaletee mabaya, wala si mema; nao watu wote wa Yuda, waliopo hapa katika nchi ya Misri, wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa, hata wakomeshwe kabisa.
28 Nao watakaoukimbia upanga, watatoka katika nchi ya Yuda, watu wachache sana; na wote wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili kukaa huko, WATAJUA NI NENO LA NANI LITAKALOSIMAMA, NENO LANGU, AU NENO LAO.
29 Na hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu, asema BWANA, kwamba mimi nitawaadhibu ninyi mahali hapa, mpate kujua ya kuwa maneno yangu yatasimama juu yenu, kuwaletea mabaya bila shaka;”
Yamkini huu ujumbe unakukuhusu wewe unayesoma ….ambaye Bwana amekukutanisha na madhabahu hii, basi, fahamu kuwa Bwana anasema na wewe ili uache kushindana na Neno lake…maana siku zote Neno la Bwana ndilo linaloshinda na kusimama daima, ila maneno yetu tunayoyatumainia hayatufikishi popote.
Leo hii unawapuuzia watumishi wa Mungu wanaokuletea injili, na kuwaona kuwa waongo, unawadharau kwa sababu ya kiburi chako kama walivyomdharau Yeremia na kumuona kuwa ni muongo (Yeremia 45:1-4), na wewe vivyo hivyo unawakejeli na kuwadharau watumishi wa Mungu na kuona huko Misri ulipo kuna usalama, huko kwenye anasa na starehe za kila namna ya dunia hii, ukadhani kuwa hii dunia itaendelea tu kukupa raha na amani sikuzote..usijue siku zake za kuangamizwa zimekaribia.
Nataka nikuambie wale watu kwasababu ya kiburi chao kama hicho ulichonacho walimuona Yeremia mtumishi wa Mungu kuwa ni muongo na anayoyasema amejitungia tu mwenyewe kama tu na wewe yamkini unasema ndani ya moyo wako hivyo, pale unapoambiwa uache huo uvaaji mbovu wa vimini na masuruali na hayo mapambo ya kidunia uliyoweka kwenye mwili wako ili upate kushindana na Muumba wako aliyekuumba ukiwa mkamilifu.. unasema ni uongo kwasababu ya kiburi cha uzima, leo hii umebadilisha nywele, kucha, na muonekano wako ambao Bwana alikuumbia nayo akaona kila kitu ni chema.
Huko kote ni kushindana na Mungu…ndio maana Bwana anasema ninyi mnapindua Mambo.
Isaya 29:16 “Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa, kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?”
Isaya 45: 8 “Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia!…”
BWANA leo anakuita utoke huko Misri (kwenye udunia), toka huko kwenye anasa na starehe za ulimwengu huu maana hakuna usalama bali ni ghadhabu ya Mungu tu.
Vile vile yamkini umeokoka mwanzoni, Bwana akukutoa Misri kwenye utumwa wa dhambi, ila sasa unatamani kurudi huko tena, leo Mungu anakusihii usitamani kurudi tena huko, usitamani kurudi kwenye uasherati, ulevi, kwenye mapambo ya kidunia. Baki ndani ya Neno la Mungu maana ndiko usalama wako ulipo, vumilia njaa, na dhiki mbali mbali maana ni za kitambo kidogo tu, utaingia kwenye raha ya milele.
Wewe binti usishindane na Muumba wako!! ridhika na vile alivyokuumba, wala usitake kubadilisha mwonekano wako, huko ni sawa unashinda naye, unapobadilisha rangi za kucha zako, na ngozi yako, nywele zako na kuweka za bandia, na kutoboa masikio yako, na pua yako kwasababu ya kutafuta urembo zaidi ya aliyokuumbia Mwenyezi, basi, hapo unashindana na kusudi lake. Ni heri uonekane mshamba ili umpendeze Mungu wako kuliko kuonekana wa kisasa na kuwapendeza walimwengu na mwisho kuishia Jehanumu ya moto.
Bwana anakuambia ”usiwe na miungu mingine ila Mungu wako tu aliyekuumba” hizo vitu bandia ulizoweka kwenye mwili wako ni miungu ya kigeni, ni roho ya Yezebeli, hizo hereni, wanja, lipustick, wigi, rangi za kucha zimebeba maroho nyuma yake ambazo ndizo zinakutumikisha kwenye utumwa wa dhambi… hivyo usiendelee kuwa mtumwa, amua kuviondoa vyote na kuvichoma moto.
Usiende Misri mwana wa Mungu. Usiende Misri!! Na kama upo huko toka haraka..Njoo kwa Yesu. (Toka kwenye udunia), uepukane na ghadhabu ya Mungu inayokuja.
Amua kumpa Yesu maisha yako kwa kudhamiria kabisa kutubu dhambi kweli kweli na kuacha ulimwengu… ili uokoe nafsi yako. (Kumbuka ziwa la moto lipo na vile vile tunaishi siku za mwisho kabisa). Jiulize leo ukifa au unyakuo ukitokea utakuwa mgeni wa nani sasa usipokubali kumpa Yesu maisha ingali bado unayo nafasi, tubu sasa kisha tafuta kanisa la kweli ukabatizwe ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na Kwa Jina la Yesu Kristo Sawa sawa na Matendo 2:38..na utapokea Roho Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kweli yote…huku we mwenyewe ukitia bidii kuzidi kumsogelea Mungu.
Bwana akubariki sana.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.