Fahamu siri iliyopo katika Neno la Mungu.

Biblia kwa kina No Comments

 

Fahamu siri iliyopo katika Neno la Mungu.

Sehemu 01

Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Tunakuwa ni wazito wa kusoma maandiko ni kwa sababu hatujui uweza au nguvu iliyoko katika maandiko/Neno la Mungu. Wengi wetu tunasoma tu kama sehemu ya Ukristo wetu na tunajikuta hakuna kitu kikubwa sana tunachokipata zaidi ya kuwa na mistari mingi vichwani mwetu.

Si vibaya kuwa nayo na si kwamba haitakiwi uwe navyo la unatakiwa uwenavyo vingi sana na viweke kwa kadili umezavyo kwa msaada wa Roho wa Yesu.

Lakini kama tukitambua kwa kina hili neno la Mungu ni nini? Au limebeba nini katika ule uhalisia wa ndani kabisa basi tutakuwa ni watu wa kusoma biblia kila siku katika ufahamu mpana zaidi.

Kila Neno/Andiko ni ufunguo unaokusaidia wewe kuingia sehemu nyingine katika ulimwengu wa roho

2 Timotheo 3

16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;

17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

Sasa Neno la Mungu limebeba nini au kuna siri gani iliyopo?

Kuna siri nyingi zipo tutaangalia chache kwa undani kidogo.

1.Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe.

Wengi tunajua ni neno la Mungu lakini hatujui kuwa ndio Mungu mwenyewe yaani wazo la Mungu au mpango mkamilifu wa Mungu yaani kwa uhalisia Mungu hatumfahamu anafananaje/yaani sura yake nk.

Lakini Mungu kajiweka katika urahisi sana wa sisi kumfahamu na tukitaka kumjua yeye ni nani tabia yake ikoje amejifunua kupitia maandiko hivyo kama tukisoma Neno lake tunamsoma yeye.

Yohana 1:1
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”

Unaona hapo? Neno linatajwa mara tatu likielezewa uhalisia wa hilo Neno ni nini. Linatajwa “Neno” mwandishi anataka kutuonyesha huyo Neno ni nani? Anasema huyo Neno alikuwa ni “MUNGU” Sasa kivipi Neno alikuwa ni Mungu? Mwandishi anaelezea tena..

Yohana 1:14
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

Unaona hapo? Neno huyo alifanyika kuwa mwili akakaa kwetu, nani huyo? Yesu Kristo yaani Mungu mwenyewe/Wazo la Mungu (Mungu mwenyewe alivaa mwili).

Mwandishi huyu katika waraka wake anaelezea vizuri tena..

1 Yohana 1:1
“Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima ;”

Hivyo Kristo ndio Neno la Mungu na ndio Mungu mwenyewe unaposoma maneno ya Bwana Yesu na Biblia nzima maana yake unamsoma Mungumwenyewe na kumuelewa tofauti na wanasanyansi ili wag undue mambo yanayoendelea hata nje ya dunia itawagharimu kufanya uchunguzi kwa gharama kubwa na muda mwingi na bado wanafanikiwa kwa sehemu ndogo sana lakini sisi Kristo kajifunua kwetu si tumuelewe tu bali tuwe kama yeye.

Hivyo unaposoma Neno la Mungu basi tambua unasoma Mungu mwenyewe asiyeonekana kwa macho ya damu na nyama Haleluya.

2 .Neno ndio lililofanya kila kitu kinachoonekana na kisichoonekana.

Hii ni siri nyingine iliyoko katika Neno la Mungu ndio lililofanya kila kitu unachokiona hapa duniani.

Sasa na sisi tukitaka kufanya kitu kisichoonekana kuwa dhahiri ni lazima tuwe na Neno la Mungu maana ndio chanzo cha kila kitu.

Yohana 1:3
“Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”

Sasa unaposoma Neno na likakaa ndani yako basi unaweza kuumba jambo lolote kupitia hilo.. maana hilo Neno la Mungu ndio lilifanya vyote. Chochote unachokitaka kipo ndani yake, iwe kazi,Mume,Familia,Mke,nk ukiwa na hili unaweza kuumba vikatokea vyote. Hiyo ndio nguvu ya Neno la Mungu. Vitu vingi haviumbiki na tunatamani ni kwa sababu hatusomi Neno na kuliweka moyoni. Na kulifanyia kazi.

Waebrania 1:2
“mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.”

Anasema tena..

Wakolosai 1:16
“Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.”

Hivyo tunafanya miujiza nk kwa sababu Neno lenyewe ndio linalotuwezesha.

3.Neno la Mungu ni uhai na tena ni uzima.

Neno la Mungu ni hai linapoingia ndani ya mtu linaleta mabadiliko kwa sababu ile ni pumzi ya Mungu.

Neno ni uzima tena usioharibika. Tunapolisoma linazidi kutuhuisha kila siku na kutufanya kuwa ni watu wengine kabisa.

Yohana 1

4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.

5 Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.

Unaona hapo? Ndani yake maana yake nje hakuna uzima na ukitaka kuuona uzima kweli kweli ndani yako Soma Neno.

Waebrania 4:12
“Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.”

Neno la Mungu ni hai, linanguvu ya kubadilisha mambo yasiyowezekana yakawezekana(Huyu ni Mungu mwenyewe awezae kufanya yasiyowezekana yakawezekana) utangundua watu wote katika maandiko walikuwa wanapokea ahadi iliyotamkwa kwa Neno tu.

Mungu alitamka tu Neno kwa Ibrahimu kuwa mwakani unaokuja atakuwa na mtoto Sarah akacheka lakini ikatokea.

Mtu mwingine anaitwa Simon aliambiwa Hatakufa mpaka atakapomuona mkombozi ni kweli ilikuwa hivyo. Hakutokewa na Mungu lakini ilikuwa ni sauti ya Mungu iliyosema nae yaani Mungu alisema Neno juu yake.

Mwandishi anasema li hai,lina nguvu na lina ukali hizi ni sifa Neno hilo(Biblia yako/Mungu) na ni jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo maana yake Neno la Mungu linaufahamu wa juu sana usioelezeka.

Katika Sehemu ya pili tutajifunza namna ya kutenda ili Neno hili lifanyike halisi katika maisha yako tutajifunza kanuni. (Kila kitu kinaongozwa na kanuni iwe duniani ama mbinguni na usipofata kanuni ni ngumu kupata unachokitarajia)

Maranatha.
Ubarikiwe sana.
Mawasiliano 0613079530.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *