WATU WALIOGANDA JUU YA SIRA ZAO NI WATU GANI? (Sefania 1:12)

Maswali ya Biblia No Comments

WATU WALIOGANDA JUU YA SIRA ZAO NI WATU GANI? (Sefania 1:12)

Swali: Ni watu gani hao walioganda juu ya sira zao ambao tunawasoma katika Sefani 1:12

Jibu: Tusome

Sefania 1:12 Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; NAMI NITAWAADHIBU WATU WALIOGANDA JUU YA SIRA ZAO; wasemao katika mioyo yao, BWANA hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.

Kabla hatuendelea mbele, tuangalie kwanza maana ya sira.

Sira ni nini?

Sira ni yale makapi yanayosalia baada ya pombe kuchachushwa, ni  mchanganyiko wa maganda ya mbegu na wadudu waliokuwa wanaichachusha pombe hiyo. Kwa kawaida pombe kama divai inapomalizika kuchachushwa, wanachofanya ni kuimimina kwenye vyombo vingine kwa ajili ya matumizi na kuiacha Sira chini.. kwasababu yenyewe inakuwa kama  topetope au urojo urojo fulani hivi.

Lakini makapi haya huwa yanathamani kubwa sana kwa wachachushaji, kwasababu pombe inayokaa muda mrefu juu ya Sira, huwa inaubora tofauti na ile ambayo, imekaa kwa muda mfupi. Kwa jinsi itakavyokaa sana juu ya sira basi ladha ya divai ndivyo inavyokuwa nzuri sana, vilevile mwonekano wake na harufu yake inakuja Zaidi, Lakini ile ambayo imechachushwa tu na saa hiyo hiyo au baada ya kipindi kifupi ikaondolewa na kupelekwa katika vyombo vingine huwa haina uzuri saa kama ile iliyodumu muda mrefu juu ya sira.

Wanaotengeneza divai, za ghali kama vile zinazoitwa champagne, huwa zinaachwa muda mrefu juu ya sira, hata miezi 4 na Zaidi, hivyo ubora wake unakuwa wa juu Zaidi kulinganisha na divai nyingine za kawaida. (Soma pia Isaya 25:6)

Sasa tukirudi kwenye swali letu, ni watu gani hao walioganda kwenye sira zao ambao Bwana alinena kwamba ataenda kuwaadhibu?

Ili tuelewe vizuri, tusome tena huo unabii wa Sefania.

Sefania 1:12 Kisha ITAKUWA WAKATI ULE, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, BWANA hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.

Hapo tunasoma..kuna wakati ambao Bwana aliandaa kuja kuwaadhibu watu hao walioganda kwenye sira zao. Sasa ni wakati gani huo? Na ni watu gani hao?

Huo sio wakati mwingine zaidi ya siku za mwisho, huu unabii ulikuja kutimia kwa sehemu mbili (kwa upande wa Wayahudi na Wakristo).

Watu walioganda kwenye sira zao, ni watu ambao walibaki kuvishikilia vitu vile (makapi) vinavyotumika kuchachusha divai,  kwa kuona kuwa yana thamani sawa na vile viungo vinavyotumika kutengeneza hiyo divai kabla ya kuwa sira (makapi).

Tuseme viungo hivyo mfano wake ni kama ngano, mahindi n.k ambavyo huwa vina thamani kubwa kabla ile divai haijaondolewa, ila ikishaondolewa vitu hivyo vinabaki kuwa makapi yasiyo na thamani yoyote.

Kwahiyo watu hawa walimchukiza Bwana kwasababu ya kuendeleza kuvishikilia hivi vitu visivyokuwa na faida tena (makapi)..hao watu walibaki kuganda hapo na kujiona kuwa wapo sawa na hawahitaji tena kitu kingine.

Sasa kwanini Bwana anasema ataichunguza Yerusalemu kwa taa, ni kwasababu ndipo palikuwapo na Hekalu lake.

Hivyo anaposema anaenda kuchunguza Yerusalemu ni kwamba anaenda kuchunguza watu wake (anaendelea kuchunguza kwa taa), ile TAA INAWAKILISHA NENO LA MUNGU. Kwahiyo atapeleka nuru itakayoenda kuichunguza Yerusalemu.

Na hii NURU ilikuwa ni NENO LA KRISTO, wakati ambapo Kristo alipotokea akaanza kuchunguza/kulihubiri hili Neno katikati ya Israeli, huko ndiko alikutana na wale watu ambao Bwana alikuwa ameshawatamikia kwamba atakuja kuwaadhibu kwasababu wameganda juu ya sira zao, na watu hao si wengine zaidi ya watu wa MADHEHEBU, ambao yalikuwepo madhehebu makubwa kama Mafarisayo, Masadukayo, Wahesenayo n.k.

Hivyo Neno la Mungu lilikuja kuwachunguza watu hawa kwa ukali, Kristo alipokuja akaanza kuwakemea na kuwaita kizazi cha nyoka, watu ambao walikuwa wanamkiri Mungu kwa midomo yao ila mioyo yao iko mbali na Mungu.

Hivyo Kristo alileta Neno lake katikati ya watu ambao walikuwa katikati ya madhehebu (katikati ya SIRA), walikuwa wameganda katika sira zao, tabia ambayo ilikuwa inamchukiza Mungu, watu ambao wanasema kwa mioyo yao Bwana hatatenda mema wala hatatenda mabaya.

Ndivyo watu wa madhehebu walivyo, wanasema ndani ya mioyo yao Bwana hatatenda mabaya, hataadhibu, ni watu ambao wanajiona katika macho yao wakamilifu sawa na ufunuo 3.

Ufunuo wa Yohana 3:14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; 

Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

[15]Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

[16]Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

[17]KWA KUWA WASEMA, MIMI NI TAJIRI, NIMEJITAJIRISHA, WALA SINA HAJA YA KITU; NAWE HUJUI YA KUWA WEWE U MNYONGE, NA MWENYE MASHAKA, NA MASIKINI, NA KIPOFU, NA UCHI.

Ni sawa na Mafarisayo na Waandishi ambao walikuwa wanajiona ni matajiri na hawahitaji kitu kingine, lakini Bwana aliwaonya kwamba atawaadhibu, wao hawakutazamia ghadhabu yoyote, hawakutazamia chochote kibaya ambayo Bwana atakuja kuwaadhibu nayo, kwasababu wanayo madhehebu makubwa, wao ni wa Masadukayo, Mafarisayo, Waalimu, wameketi mahali pa juu.

Lakini Bwana akawa anasema nitawaadhibu akitumia Mithali wasipate kuelewa, kwamba ni watu ambao wameganda juu ya sira zao, na ndio maana ilipokuja Neno la Kristo kwa watu hawa, unaweza ukaona jinsi ambavyo lilikuja kuwaadhibu, na hawakuweza kujua ni mambo gani walikuwa wamekosea kwasababu walikuwa wanajiona ni matajiri..wakamwendea Kristo kama matajiri na kumwuliza wewe ni nani? Unakosea kusema hivi na vile,

Na hata kizazi hiki, Bwana anakuja kuwaadhibu watu walioganda juu ya sira zao (madhehebu), ambao wanasema wao ni matajiri na wapo sahihi, hawahitaji kitu.. lakini tayari Bwana amesema atawatapika wasipotubu na kukubali kufuata Neno lake.

Vilevile watu wote ambao wamestarehe na kufanikiwa kwenye dhambi zao Bwana anawaonya watubu.

Yeremia 48:11 Moabu amestarehe tangu ujana wake, naye ametulia juu ya sira zake, wala hakumiminwa kutoka chombo kimoja kutiwa chombo kingine, wala hakwenda kufungwa; kwa hiyo ladha yake anakaa nayo, wala harufu yake haikubadilika.

[12]Basi, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo nitampelekea wamiminao, nao watammimina, nao watamwaga vyote vilivyomo vyomboni mwake, na kuzivunja chupa zake vipande vipande.

Je! Ni wewe ambaye umekaa na kustarehe kwenye maisha ya dhambi? Au ni wewe ambaye umeganda juu ya sira yako (dhehebu lako) na kujiona uko salama.

Basi leo Bwana anakupa shauri hili..

Ufunuo wa Yohana 3:18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

[19]Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

[20]Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

Tubu mgeukie Kristo kwa moyo wako wote, acha kujitumainia na ukubwa wa dhehebu lako maana madhehebu yote ni makapi, tena ni watoto wa yule kahaba mkuu. (Mama wa makahaba), usiendelee tena kushikilia hayo makapi, tafuta kumjua Mungu wa kweli, maana kila atafutaye atapata.

Na wewe ndugu ambaye unajiona salama kwenye maisha ya dhambi, leo hii unatenda dhambi lakini huoni chochote, unazini Bwana hakuadhibu kwa lolote, unafanya mambo yako machafu kwa muda mrefu sasa, unakwenda kwa waganga, hauumwi, kinyume chake unazidi kustawi, unaendelea kufanya anasa na ulevu, unasema mbona hakuna dhara lolote linalonipata, hujiulizi ni kwa nini? Unachodhani ni kuwa wewe ni spesheli sana kwake sio?  embu soma mstari huu tena ujifunze jambo..

Sefania 1:12 “Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami NITAWAADHIBU WATU WALIOGANDA JUU YA SIRA ZAO; wasemao katika mioyo yao, Bwana hatatenda mema, wala hatatenda mabaya”.

Umeona, Mungu utafika wakati atakuchunguza kwa taa, wewe ambaye umetulia juu ya Sira yako, huangaishwi angaishwi, unafanikiwa angali upo katika dhambi, unayesema, Mungu hawezi fanya jambo lolote hata nikiwa mwovu kiasi gani.

Jiangalie, hukumu ipo, utakufa ghafla, na moja kwa moja utajikuta upo jehanamu kama yule Tajiri wa Lazaro, ambaye hapa duniani alikuwa akijitumaisha katika Maisha yake ya anasa tu, hajali kama kuna kuzimu, au hukumu, hajali kama kuna kiama chake mbeleni.. Na wewe ndipo utakapojikuta huko kama hutatubu, ukilia na kuomboleza, ukisema laiti ningelijua, laiti ningelijua..

Wakati huo utakuwa umeshachelewa ndugu. Leo hii ukiona Mungu hafanyi chochote juu ya dhambi zako, sio kwamba anayafurahia hayo Maisha unayoishi, anakutazama tu, yamkini siku moja utatubu, lakini ikifikia wakati haoni badiliko lolote la wewe kumgeukia yeye, atakujia na kukuondoa duniani kama alivyofanya kwa Wamoabu na wengine.

Biblia inasema saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubali ni leo, usingojee siku Fulani ukasema hiyo ndio itakuwa siku yako ya wokovu, haitakaa ije kamwe. Mpe Yesu Kristo Maisha yako leo ayaokoe, Tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha tafuta mahali ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ili upate ondoleo la dhambi zako, na Kisha mwenyewe Mungu atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu ili akae na wewe siku zote za Maisha yako.

Hata kama ikitokea Maisha yako yamefikia ukingo leo, basi unaouhakika wa kuurithi uzima wa milele.

Ikiwa utapenda kuokoka, na unahitaji msaada huo basi unaweza, kutafuta kanisa la kiroho lililokaribu na wewe, wakusaidie au ukawasiliana na sisi kwa namba zetu hizi +255693036618 /+255789001312 kwa ajili ya Sala ya Toba na maagizo mengine.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe wengine ujumbe huu kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *