NAMI NIMEJUA YA KWAMBA KWA UKAMILIFU WA MOYO WAKO UMEFANYA HIVI

Dhambi No Comments

NAMI NIMEJUA YA KWAMBA KWA UKAMILIFU WA MOYO WAKO UMEFANYA HIVI.

Shalom Jina la Bwana Yesu libarikiwe.

Leo tutajifunza faida ya kuwa na moyo mkamilifu mbele za Mungu.

Ni kweli unaweza ukawa umeokoka, lakini unaweza pia ukawa na moyo usio mkamilifu kwa Mungu, na  hatimaye uhusiano wako na Mungu ukawa mbaya.

Moja ya faida ambayo unaipata pale moyo wako unapokuwa mkamilifu mbele za Mungu ni kuepuka makosa mengi/dhambi ambayo ungeweza kufanya pasipo hata wewe kuijua, ila kwasababu  moyo wako umekuwa mkamilifu, Mungu atakuzuilia mambo mengi ambayo ungeweza kutenda na kumkosea yeye.

Katika biblia tunamsoma mtu mmoja ambaye kutokana na ukamilifu wa moyo wake Mungu alimzuilia kutenda dhambi ambayo alikuwa anaenda kutenda pasipo hata yeye kujua, tusome..

Mwanzo 20:1 Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari.

[2]Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara.

[3]Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu.

[4]Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki?

[5]Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. KWA UKAMILIFU WA MOYO WANGU, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi.

[6]Mungu akamwambia katika ndoto, NAMI NIMEJUA YA KWAMBA KWA UKAMILIFU WA MOYO WAKO UMEFANYA HIVI, NDIPO NAMI NIKAKUZUIA USINITENDEE DHAMBI, kwa hiyo sikukuacha umguse.

[7]Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao.

Unaona hapo, huyu Abimeleki hakujua kuwa alimchukua mke wa mtu,  laiti angejua kuwa Sara ni mke wa Ibrahimu asingemchukua, lakini yeye alimchukua pasipo kujua, kwahiyo hakuwa na hatia kwa kuwa Ibrahimu hakumwambia kweli yote, kuwa pamoja na kwamba Sara ni ndugu yangu ila pia ni mke wangu.. hakumwambia hivyo, Kwahiyo yeye alijua yupo sahihi kumchua na kumfanya mkewe, na ndipo Mungu akamtokea kabla hajamkaribia, akamwambia huyo ni mke wa mtu..mrudishe kwa mwenyewe.

Hebu tengeneza picha huyo Abimeleki angefanya hayo kwa kukusudia, unadhani nini kingemtokea. Huenda Mungu angemwangamiza kabisa yeye na familia yake yote.

Hivyo ndugu, tujitahidi kuwa wakamilifu kwa Mungu wetu, hebu jitazame moyo wako ni mkamilifu kweli mbele za Mungu?

Moyo ulio mkamilifu ni ule usio na hatia, ni ule ambao unahofu na Mungu, unamcha na kumheshimu yeye.

Ukiona unaweza ukafanya chochoate kibaya bila hata kumhofu Mungu, fahamu kuwa unahitaji msaada wa kiMungu.

Leo hii unafahamu kabisa kuwa biblia imekataza wanawake kuvaa mavazi yawapasayo wanaume(suruali), na mavazi yote yasiyo na heshima lakini bado unayavaa pasipo hata kumwoogopa Mungu, basi tambua kuwa moyo wako uko mbali na Mungu na unamhitaji yeye akupe moyo wa hofu.

Ni kweli kuna vitu vingi unaweza kufanya ambavyo havimpendezi yeye pasipo hata kujua, lakini ukifanya hayo kwa ukamilifu wa moyo, bila kukusudia, Mungu hatakuacha ufanye, atakuzuia tu. Huenda ni kazi fulani, au chochote ambacho unaweza kutenda kwa mikono yako, au hata maneno ambayo ungeweza kunena, kwa vyovyote vile Mungu atakuzuilia tu usimtende dhambi.

Lakini ukitenda hayo huku unajua kabisa ni dhambi…hapo hakuna kuzuiliwa isipokuwa utavuna tu matokeo ya hiyo dhambi.

Waebrania 10:26 Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;

27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.

Unajua kabisa kusikililiza miziki ya kidunia, kunyoa stahili za kidunia, kutazama pornography, kucheza kamari/betting, kuzini, kujichua, kunywa pombe, kuvuta sigara, kusengenya, kusema uongo, kuvaa nguo za nusu uchi, ni dhambi na mambo mengine yote ambayo dhamiri yako inakushudia kabisa kuwa hayampendezi Mungu, halafu unakusudia kutenda… fahamu kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, yaani ziwa la moto…na usitegemee kwamba Mungu atakuzuia kutenda hayo wakati tayari unajua.. Mungu hafanyi hiyo kazi.

Ni wale tu ambao wangetenda kwa ukamilifu wa mioyo yao bila kujua, ndio Mungu anaweza kuwazuia kwa njia yake anayoijua yeye, aidha kupitia mahubiri kama haya, au njia nyingine kama ndoto n.k

Hivyo unaposoma leo huu ujumbe.. yamkini ni wewe ambaye Mungu anataka akuzuie usiende kufanya dhambi tena ambayo unapanga kwenda kufanya au umekuwa ukifanya pasipo kujua kuwa ni dhambi.

Basi, sikia maonyo ya Bwana na utii…tambua kuwa mwanamke kuvaa suruali ni machukizo mbele za Mungu (kumbu.22:5) hivyo usiendelee kuvaa..nenda kazichome na nguo zingine zote ambazo hazina utukufu mbele za Mungu na kwa jamii.

Vilevile fahamu kuwa mwanamke wa kikirsto hapaswi kujipamba kwa kusuka nywele, kuweka mapambo ya kidunia kwenye mwili wake kama hereni, vikukuu, bangili, cheni, vipini, lipustick, wanja, mekaup, rangi za kucha na kucha bandia, biblia inasema wanawake wa kikirsto wanapaswa wajipambe kwa mapambo ya rohoni somo 1Petro3:3 & 1Timotheo 2:9.

Leo hii Mungu anakujulisha haya kwasababu anakupenda na ameona kwamba unayafanya hayo kwa ukamilifu wa moyo (pasipo kukusudia) na ndio maana anataka akuzuie usiendelee kumchukiza… hivyo ni heri ukatii sauti hii.

Hapo ulipo tubu na ugeuke katika njia ambayo ulikuwa unaelekea, ulikuwa unampango wa kwenda kucheza kamari na magemu basi leo umesikia sauti ya Mungu kwamba hayo ni machukizo, geuka kabla Mungu hajakuacha maana alikuwa anakuvumilia tu kwa kuwa ulikuwa unatenda pasipo kujua.

Kumbukumbu la Torati 18:10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, WALA MWENYE KUBASHIRI, wala msihiri,

[13]Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako.

Ulikuwa unampango wa kwenda saluni kusuka na kupamba uso, geuka sasa maana unaenda kumchukiza Mungu.

Mwanzo 20:6 Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse.

[7]Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao.

Je! Umeokoka? Unafahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa siku za mwisho na unyakuo umekaribia!!

Ni heri ukampa Yesu Maisha yako leo ili akuepushe na hukumu inayokuja.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Ubarikiwe sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *