Je! Umevunjiwa Kongwa lako?
Mambo ya Walawi 26:13 Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ILI MSIWE WATUMWA WAO; NAMI NIMEIVUNJA MITI YA KONGWA LENU, nikawaendesha mwende sawasawa.
Kongwa nini?
Kongwa ni nira au kifungo cha shingoni ambacho kinatengenezwa kwa kutumia mti uliogawanyika sehemu mbili au mti uliochongwa unaoshikamanisha au kuunganisha vitu viwili katika sehemu moja.
Tazama picha juu.
Mtu yoyote ambaye yupo nje ya wokovu, yupo chini ya kongwa la ibilisi, yaani ni mtumwa wa ibilisi kwa kujua au kutokujua.
Wana wa Israeli walipokuwa Misri walikuwa chini ya kongwa/utumwa wa Farao mpaka ilipofika wakati Bwana Mungu akaja kuvunja hilo kongwa kwa kuwatoa utumwani na kuwaleta katika nchi yao ya ahadi ambapo aliwafunga kongwa lake (Sheria zake).
Hata na sisi tulipokuwa katika vifungo vya giza, tulipokuwa tukitumikishwa kwenye dhambi, tulikuwa tumefungiwa kongwa zito ambalo lilitulemea kwa muda mrefu mpaka ilipofika wakati, Mungu akamtuma mwanae mpendwa Yesu Kristo ambaye alikuja kuvunja lile kongwa ambalo tulifungiwa na shetani, akatufunga kongwa/nira yake ambayo ni laini..na hivi sasa tupo huru mbali na dhambi na vifungo vyote vya ibilisi.
Je! Wewe umevunjiwa Kongwa lako? Je! Umewekwa huru au bado upo utumwani?
Ikiwa leo dhambi ina nguvu juu yako, ujue bado upo chini ya kongwa la ibilisi, hata kama utasema umeokoka na unampenda Yesu.
Ikiwa tamaa zinakushinda, ikiwa uzinzi, usengenyaji, uongo, uchungu, vinyongo, wivu, n.k vina kushinda, basi tambua bado umefungwa nira na ibilisi.
Lakini Yesu Mwokozi wa ulimwengu, leo anakuambia..
Mathayo 11:28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
[29]Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
[30]kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Umeona, leo hii unapoamua kumgeukia Yesu na kutubu dhambi zako zote, Kristo yupo tayari kukupokea na kukupumzisha/kukuondolea ule mzigo uliokulemea, lile kongwa zito ambalo umekuwa ukilibeba kwa muda mrefu.
Yeye anasema, nira yake ni laini, na mzigo wake ni mwepesi… hivyo tukajifunge kwake.
Kwahiyo ndugu yangu, nakusihii leo mpokee Yesu ili akuweke huru, avunje hilo kongwa ambalo umefungiwa na adui.. kubali kutubu dhambi na kukana nafsi na kumfuata yeye kweli kweli, kubali kuacha ulimwengu, kubali kuacha kazi za ibilisi maana mwisho wake ni uchungu, kubali leo hii Bwana avunje nira zote ndani yako ambayo ni kinyume na mapenzi yake.
Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Kumbuka..
Kwa Yesu lipo tumaini la uzima wa milele.
Kwa Yesu Unapata utulivu wa nafasi na faraja. Alisema.
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.
Kwa Yesu zipo Baraka, Na kwa Yesu upo msahama wa kweli:
Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”.
Kwa hiyo unapokuja kwake leo hii kwa kumaanisha, ujue kuwa hiyo mizigo ya dhambi uliyonayo haijalishi ni mingi kiasi gani ataitua mara moja, haijalishi uliuwa watu wengi namna gani, haijalishi ulizini nje ya ndoa mara nyingi kiasi gani, haijalishi ulikwenda kwa waganga mara nyingi namna gani..Ikiwa tu upo tayari leo kumkaribisha Yesu moyoni mwako basi ataitua, na kukusamehe kabisa kana kwamba hakuna chochote ulichowahi kumkosea..Na atakupa amani.
Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwake, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa..
Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..
Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.
Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Hongera kwa kuokoka.
Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.