Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu..
Upo umuhimu mkubwa wa wewe mzazi au mlezi kumlea mtoto wako Katika njia inayompasa, kwasababu hataicha kabisa, ndivyo maandiko yanavyotujuza,na Neno la Mungu halisemi uongo,ina maana malezi unayomlea Mtoto wako saivi, yale ya kumpenda Mungu na kuzishika sheria za Mungu, na kumfundisha kuenenda Katika njia zake, fahamu kabisa matunda hayataishia kwa mwanao tu bali yatakwenda hadi kwa wajukuu, na hiyo inatokana na vile alivyoona mwenendo wako wewe mzazi, sasa hapo mnajikuta kizazi chako chote mpka cha nne kinamtumikia Bwana, tena chenye baraka mbele za Mungu..
Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”
watu wengi wamekuwa wakiwalaumu au kutoa mashutumu kwa Watoto au wajukuu wakijua chanzo ni wao, lakini sivyo, ukiona shida ipo kwa mjukuu basi fahamu chanzo kilitokea kwa bibi na babu, kwasababu wao ndio walishindwa kuwalea watoto wao kwenye misingi mizuri ivyo ikapelekea mpaka na wajukuu wao kuharibika pia, lakini kama bibi na babu wangewalea watoto wao kwenye njia inayowapasa na wajukuu wangekuwa kwenye njia hiyo hiyo kwa kuwa tayari walishafanyika kama kielelezo kwa watoto wao..
Ipo mifano mingi kwenye maandiko ya wazazi waliowalea watoto wao kwenye njia zinazowapasa hivyo ikapelekea wajukuu kusimama vema kwenye njia hiyo hiyo,
Wengi tunamsoma timotheo lakini hatukisomi chanzo chake mpaka yeye kuja kuwa askofu wa makanisa, na kuaminiwa na mtume Paulo,
Chanzo chake tunakiona kwa bibi loisi ambaye alikuwa na Mtoto wa kike aliyeitwa Eunike, sasa huyu Eunike ndiye aliyemzaa timotheo tunayemsoma, yani Eunike ni mama wa timotheo..
2Timotheo 1:4 “Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha;
5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo”.
Umeona hapo, mtume Paulo anamuelezea timotheo msingi wa imani yake kwa Yesu Kristo, kumbe hakuanza nayo yeye kama yeye, chanzo kilitokea kwa Bibi yake,kikaja kwa mama yake Eunike ndipo kikamfikia yeye mwenyewe, hapo ndo tunaona umuhimu kwasababu hata alipoisikia injili hakuwa na ukakasi ndani yake, akaaminika kwa mtume Paulo hata kufikia kuwa askofu Katika makanisa, kitendo cha timotheo kumpenda Mungu kilianzia kwa bibi yake loisi..
ijapokuwa hakuwa wa kabila la Israeli, kwasababu maandiko yamemtaja baba yake kuwa ni myunani lakini hilo halikumzuia bibi yake kumfunza mwenendo mwema wenye kumpendeza Mungu..
Matendo 16:1 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani.
2 Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio.
3 Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani
Tunapoyaona haya tunajifunza nini, leo tunamfurahia timotheo lakini chanzo cha yeye mpaka kuwa hivyo hatukitaki, kaa chini utafakari hapo ulipo pamoja na umri ulionao,je kitu gani umewarithisha watoto wako, ni nini cha ziada umekipanda ndani yao, tunakimbilia kuwapa elimu ya shuleni bila kufahamu msingi mkuu ni nini, Bibi yake timotheo alilijua mapema, akaanza kumjengea misingi bora binti yake Eunike akijua kabisa matunda atayaona kwa mjukuu wake, na ndivyo ilivyokuwa, kupitia malezi bora aliyomlea Eunike ndiyo hayo tunayaona kwa timotheo zaidi..
Utafakari mwenendo wa timotheo, ujiulize kipindi chake alichokuwepo je kulikuwa hukuna vijana watanashati wenye elimu kubwa zaidi yake, lakini wako wapi, mbona hatuwaoni kama timotheo, pengine kulikuwa matajiri wenye fedha na mali tena wenye umri sawa na yeye lakini hawakukipata hichi alichokipata timotheo, wamepotea Kabisa, kumbukumbu lao halipo, ila kwa timotheo tunazisoma habari zake na zimekuwa shuhuda kwa ulimwengu mzima,
Hapo hapo jiulize katika kipindi cha bibi loisi je kulikuwa hakuna mabibi na wamama wa kuigwa, walikuwepo! lakini habari zao hazikuweza kufanya kitu kwenye Ufalme wa Mungu zaidi ya huyu bibi na binti yake tunayewasoma mpaka leo, waliweza kutumia vema nafasi zao ili kuhakikisha wanamsimamisha Mtumishi wa Mungu, na hakika tunalithibitisha hilo kwa askofu timotheo..
Nafasi uliyonayo leo inaweza kufanya chochote kwenye familia yako, uzao wako,na kizazi chako, kwasababu maandiko yanasema Mungu ni yule yule hajabadilika, ni wewe kuanza kuwafundisha wanao Katika misingi ya kiMungu, kuwalea kwa namna inayompendeza Bwana,uzao wako wote hata wa mwisho, na ndivyo Bwana atakavyoliachia kumbukumbu lako kwa kazi uliyoifanya,
Chukua hatua sasa, wafundishe umuhimu wa kumtumikia Mungu, kuzishika sheria zake na maagizo yake, waundie utaratibu wa kuwa waombaji,kuhubiri, na kulisoma Neno la Mungu kila siku, wazoeshe umuhimu wa kuhudhuria ibdani tena bila kukosa wala kuchelewa, kwa kufanya hivyo utawajengea misingi mizuri itakayokuja kuwasimamisha imara mbeleni,utamsimamisha zaidi ya timotheo..
Bwana akubariki,
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.