Ipi tofauti ya ukuaji wa kiroho na karama za Roho?

Biblia kwa kina No Comments

Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele yote karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Ipo tofauti kubwa kati ya mtu ambae amekua kiroho na ana karama za rohoni na mtu ambae anakarama za rohoni lakini ni mchanga katika roho yaani hajakua bado.

Ni jambo ambalo linawachanganya Wakristo wengi wanashindwa kuelewa badala yake wanapoona mtu anafanya ishara na miujiza na kuponya wagonjwa,kuomba kwa Muda mrefu, nk wanafikiri moja kwa moja kwamba huyo mtu amesimama vizuri rohoni yaani amekua ni mtu mzima lakini jambo hili si kweli.

Mtu anaweza kuwa na matendo ya imani akahamisha milima nk. Lakini akawa ni mtoto rohoni kabisa.

Karama za rohoni ni nini?

Ni vipawa vya rohoni vinavyotolewa na Roho Mtakatifu kwa waamini wote kwa kusudi la kulijenga kanisa,kuhudumia wengine, na kudhihirisha nguvu za Mungu katika ulimwengu. 

Kulingana na maandiko zipo karama nyingi lakini hatutaziangazia kwa leo.

Karama hizi kila Mkristo anapewa wala hakuna Mkristo asiyekuwa na karama labda hajatia bidii na nia ya kujua karama yake na Roho Mwenyewe ndio anamgawia mtu kwa kadili apendavyo yeye wala mtu hachagui kuwa na karama fulani la!.

Ukuaji wa kiroho ni nini?
Ni mchakato wa ndani ya mtu aliemwamini Yesu Kristo kukua katika uhusiano wake na Mungu kufanana na Yesu katika Tabia,mwenendo,nk.

Ukuaji wa kiroho ni mchakato si jambo la haraka haraka tu. Ni kama mtoto mdogo anavyozaliwa anapitia hatua kwa hatua kufikia umri wa kujitambua na kufanya maamuzi mwenyewe yaani kujisimamia katika maisha yake.

Mkristo anaesimamiwa katika mambo yake ya msingi kama Maombi, kusoma neno,kuhuburi,nk ni ishara kuwa bado hajakua.

Ili kulielewa hili jambo tulitafakari kanisa la Korintho.  Ni kanisa pekee ambalo mtume Paulo alifundisha kwa upana sana juu ya karama za rohoni,  na ukweli ni kwamba katika makanisa yote kanisa hili la Korintho lilithirisha kiwango cha hali ya juu sana juu ya karama za rohoni.

Katika ibada watu watatu au sita ilikuwa ni kawaida kutoa unabii wa kweli kwa muda mmoja na katika zote zilikuwa ni kweli.

Kanisa hili lilifanikiwa sana katika kudhirisha karama za rohoni vyema lakini pamoja na hayo Paulo anawaita ni watu wa mwilini na si wa rohoni unajua kwa nini?  Tutaona hapa jinsi kanisa hili lilivyokuwa mwenendo wake.

1 Wakorintho 3

1 Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo.

2 Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,

3 kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

Unaona hapo! Paulo anasema hakuweza kuzungumza nao kama watu wa rohoni bali mwilini.  Moja ya sababu hizo walikuwa na matengano wao kwa wao, kuna wengine walikuwa wanasema wao ni wa Apolo  wengine wa Paulo.

1 Wakorintho 3

4 Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu?

5  Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa.

Watu wanaweza kuwa ni waombaji kila siku, nk lakini wakawa watu wa Mwilini mstari wa tatu anasema…. “ kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

Walikuwa ni watu waliojaa fitina,husuda,wivu,mashindano, mambo ambayo ni ya watu wa mwilini kabisa..

Ikiwa ni kutoa unabii kila mtu Alitaka aonekane kuwa yeye ndiye kuliko wenzake hakukuwa na maelewano kabisa. Maana yake watu hawa walikuwa ni wa mwilini kabisa.  Wanakarama kweli ndani yao na zinafaya kazi lakini si kwamba wamekua kiroho.

Sasa Mtu aliekua kiroho na, ana karama ndani yake kuna sifa kadhaa ziko kwake na ikiwa zipo basi jua uko katika mchakato endelevu ikiwa hakuna basi fanya hima kubadilika usidumae.

1.kumuona mwenzako ni sehemu katika mwili wako.

Paulo anawafundisha Wakorintho ya kuwa wao (kanisa ) ni mwili wa Kristo maana yake sisi ni viungo katika mwili huo.

Huyo Mshirika Mwenzako unaeabudu naye si mshirika tu lakini muone ni sehemu katika mwili wako maana yake ukimsema vibaya,ukimchukia,kumseng’enya, kumuonea vivu,kufurahia unapoona amefeli nk jua unausema vibaya mwili wako,unauchukia mwili wako(na mwili wa Kristo) unaposhindana na ndugu yako unashindana na mwili wako mwenyewe..

Yaani ni sawa sawa na mkono wako wa kulia kushindana na mkono wako wa kushoto na mkono wako wa kulia ujione kuwa ni bora kuliko wa kushoto je jambo hili linawezekana? La!.

Mthamini sana huyo ndugu unaeabudu nae hapo muone ni wa thamani usiwe na mashindano nae nk.

Wafilipi 2

3 Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

2. Kuwaombea wengine.

Mtu aliekua kiroho hachukui muda mwingi sana katika kujiombea mwenyewe tu(sisemi kujiombea ni vibaya la! Jiombee sana pia) lakini chukua muda wako kuwaombea wengine kwa kuzama kabisa ndani katika matatizo na changamoto walizonazo waombee(huenda kuna wengine wamerudi nyuma,wengine wamedumaa hawakui hawajui hata wajibu wao na wako katika kanisa kwa muda mrefu nk)..

Kadili unavyoshughulika na watu kuwaombea na kutaka waendelee zaidi katika imani ndivyo Mungu pia anakutua mizigo yako mingi sana pale unapowambea wengine hasa kanisa.

Unapoliombea kanisa washirika na wachungaji wako unaanza kuingia katika ulimwengu mwingine ambao Mungu atasema na wewe mambo mengi sana utaanza kuona jinsi mambo yanavyofanyika utaanza kuelewa zaidi hutakuwa mtu wa kawaida kama hapo mwanzo.

Ni sawa sawa na wafanyakazi wa kawaida benki wao wanafanya kazi tu kawaida lakini kuna mambo mengi yanayoendelea  hawajui ila siku kama wakipandishwa daraja la juu zaidi kuna mambo mengi watayafahamu ambayo hawakuwahi hata kuyasikia wala kudhani..

Kama vile Epafra alikuwa ni mtu ambae anatumia Muda mwingi sana kuliombea kanisa lisimame liimarike na mtu aliekuwa kiroho si wingi wa maombi mengi la!,  bali ni jinsi anavyoweza kusimama mahali palipobomoka kuhakikisha kanisa linakaa katika utulivu.

Wakolosai 4

12 Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.

13Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli.

Unaona jinsi huyu mtu alivyokuwa hakuwa ana ombea tu kanisa lililokuweko Kolosai bali pia na Laodikia na wengine waliokua Hierapoli. Unaweza kuona huyu mtu alikuwa hajishughulishi sana na kupeleka shida zake binafsi kwa Mungu.

Alifahamu Mungu anaweza kuzitatua shida zake kwa yeye kujishughulisha na kanisa la Kristo lisimame imara,  mtu kama huyu ambae anasimama kwa ajili ya kanisa unafikiri Mungu anaweza kumuangalia kwa jicho la kawaida?

Unadhani Mungu anaweza ruhusu apatwe na mabaya. Maana ikiwa hivyo nani atasimama katika sehemu yake. Hivyo shugulika na matatizo ya wegine Mungu atashughulika na ya kwako ndugu.

Mungu anawaangalia kipekee sana watu wanaosimama na kuomba katika Roho na kweli kwa ajili ya kanisa, kumbuka unapoliombea kanisa unauponya mwili wa Kristo maana yake wewe si mtu wa kawaida kabisa katika roho na kuna viwango vikubwa sana utaenda vya kumuelewa Mungu.

Je! Umewahi kuwaza kufanya hivyo au kufunga na kuomba kwa ajili ya kanisa?

1 Samweli 12:23
“Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi ; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka”

Kuna hatua ukifika ukaanza kuona kutokuwaombea wengine ni dhambi na unasikia kuugua ndani yako basi tambua kabisa Mungu anakusudia usimame mahali palipo na gepu. Fanya hivyo kwa kuliombea kila siku kanisa.

Hizo shida zako ni ndogo kwa Bwana atazitatua kwa namna hata usiyojua itakuwa ni suprise tu kwako.

Hivyo ukuaji wa kiroho upo katika maeneo mengi sana jinsi unavyofikiri,kutoa maamuzi,kutenda ndio ukuaji wa kiroho pia unaonekana unafikiri sawa sawa na Yesu Kristo, unatenda sawa sawa na Yesu Kristo, unatoa maamuzi/kuhukumu kupitia neno la Mungu na kwa msaada wa Roho Mtakatifu na sio kulingana na hisia zako tu zinavyokutuma. Na mambo mengine mengi kadili Bwana atakavyotupa neema tutazidi kujifunza.

Ubarikiwe sana.

Maranatha.

Mawasiliano: 0613079530

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *