NA TUMWEKE MTU MMOJA AWE AKIDA, TUKARUDI MISRI

Uncategorized No Comments

NA TUMWEKE MTU MMOJA AWE AKIDA, TUKARUDI MISRI

Jina la Mwokozi Yesu, libarikiwe. Karibu tujifunze maandiko, Neno la Mungu wetu ambalo ndio taa iongozayo miguu yetu, na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Safari ya wana wa Israeli ni funzo tosha, kwetu sisi tunaosafiri kutoka katika ulimwengu kwenda Kaanani yetu (yaani mbinguni). Hivyo tukijifunza kwa undani, jinsi safari ile ilivyokuwa tutaweza kujua tahadhari na sisi tunazopaswa kuzichukua katika safari yetu ya kwenda mbinguni.

Maandiko yanasema wana wa Israeli, walitolewa Misri kwa mkono hodari, lakini walipokuwa jangwani katika safari yao ya kwenda Kaanani, walikutana na changamoto chache, ambazo hizo ziliwafanya wamnung’unikie Mungu, na hata kufikia hatua ya kutamani tena kurudi Misri, walikotoka, wakasema..

Hesabu 14:3 “Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; JE! SI AFADHALI TURUDI MISRI?

4 Wakaambiana, NA TUMWEKE MTU MMOJA AWE AKIDA, TUKARUDI MISRI”.

Hesabu 11:4 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango,na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. ”.

Kama vile ilivyokuwa kwa wana wa Israeli kule jangwani, ndivyo hata sasa ilivyo ndani ya kanisa, watu wengi wanarudi sana nyuma.

Wanajiwekea watu wao (wachungaji wao, mitume wao, manabii wao, walimu wao) ili warudi Misri (ulimwenguni).

Ndio maana imekuwa kawaida sasahivi watu kuwasifu hao viongozi wao na kuwasikiliza kuliko hata Neno la Mungu.

Utakuta mtu amevaa kivituko, amejichora na kutoboa tobao mwili wake ili aonekane kuwa amejiremba, na ukimhubiria kuwa hayo mambo ni machukizo kwa Mungu, kuvaa suruali kwa mwanamke na nguo zote zisizona adabu ni machukizo makubwa..Neno la Mungu linasema hivyo, atakuambia mchungaji wetu amesema Mungu hana shida anaangalia moyo wako.

Ukimwambia biblia inasema wanawake wa kikristo hawapaswi kusuka nywele, kuvaa hereni, nywele bandia, kucha bandia, kutumia mikorogo, na mapambo aina yoyote, na kwamba wanawake wa kikristo wanapaswa wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri na mapambo ya ndani (1Timotheo2:9-10 & 1Petro3:3-5).. anakuambia Nabii wetu amefunuliwa kuwa hizo vitu havina shida.

Ni kwasababu gani? Ni kwasababu wamemweka huyo nabii, huyo mchungaji kuwa kama akida ili awaongoze kurudi Misri (ulimwenguni).

Wakristo wengi ambao mwanzoni walianza vizuri, walitii wito wa toba, wakatubu, wakabatizwa, wakaendelea mbele na safari ya Imani, lakini kama vile ilivyokuwa kwa wana wa Israeli walitoka misri, wakabatizwa katika bahari ya Shamu, wakapewa mana katika safari yao lakini walishindwa kufika kwasababu waliona Misri kuna raha zaidi ya ile nchi wanayoiendea, WAKAAMBIANA NA TUMWEKE MTU MMOJA AWE AKIDA TUKARUDI MISRI.

Maandiko yanasema kwa kunung’unika huko, na kwa kutamani huko kurudi Misri, tayari walisharejea Misri katika mioyo yao, ijapokuwa katika mwili bado wapo jangwani.

Matendo 7:39 “Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, NA KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI,

40 wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, ALIYETUTOA KATIKA NCHI YA MISRI, hatujui lililompata”.

Ndio maana katika wote walionung’unika na kutamani kurudi Misri,hakuna hata mmoja aliyeingia nchi ya Kaanani, wote walikufa jangwani.

Kwanini?, kwasababu katika mwili walikuwa wametoka Misri lakini katika roho/moyo walikuwa wapo Misri. Na kwasababu nia ya ndani inazungumza Zaidi kuliko mwonekano wa nje, wakaangamia wote jangwani bila kufika kule wanakokwenda.

Kadhalika na wakristo wengi leo hii wanarudi nyuma na kuacha imani waliyoanzanayo, wamekinai Neno la Mungu kama vile wana wa Israeli walivyokinai ile mana wakamnung’unikia Mungu na kuamua kurudi Misri.

Ndugu/Dada kumbuka tupo mwisho wa safari yetu ya imani, Bwana Yesu amekaribia kurudi na alisema..

… walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? (Luka 18:8)”

Mwanzoni ulikuwa moto, ulianza vizuri, ulikuwa unachukia udunia, ulikuwa unavaa mavazi ya heshima na adabu, ulikuwa unatii Neno la Mungu, ulikuwa unafunga na kuomba kila week, ulikuwa hata unawashuhudia wengine habari njema ya wokovu, lakini sasa umegeuka na kuupenda ulimwengu, umegeuka na kusema kule Misri nilipokuwa nilikuwa nakula vizuri, naishi vizuri, umegeuka na kuona maagizo ya Mungu kwako ni sheria ngumu, na kwakuwa umeona kule Misri ndio kuna raha..basi umeungana na wenzako mkaambiana na TUMWEKE MTU MMOJA AWE MCHUNGAJI/NABII/MTUME atuongoze turudi zetu Misri.

Ndio maana unamsifu huyo nabii anayekutabiria na kukudanganya kuwa huko Misri kuna raha, huyo anayekuambia Mungu haangalii mwili anaangalia tu moyo na wewe unamsikiliza..tayari huyo ni Akida wako ambaye mmemweka awarudishe Misri.

“Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka, ukatubu na kurudi katika imani uliyokuanayo ambayo inakuelekeza utii Neno la Mungu.”

Tunaishi ukingoni kabisa mwa siku za mwisho, huu sio wakati wa kurudi nyuma..ni wakati wa kukaza mwendo.. maana Bwana amekaribia kurudi na anataka aje akute ile imani tuliyopokea kwa mababa zetu (mitume), usijidanganye kuwa kule Misri kuna raha, maandiko yanasema.

Yeremia 44:14 “Hata katika watu wale wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili wakae huko, hapatakuwa na mtu ye yote atakayepona, wala atakayesalia, na kupata kurudi nchi ya Yuda, ambayo wanatamani kurudi ili kukaa huko; maana hapana atakayerudi, ila wao watakaopona.

[27]Tazama, nawaangalia niwaletee mabaya, wala si mema; nao watu wote wa Yuda, waliopo hapa katika nchi ya Misri, wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa, hata wakomeshwe kabisa.

Misri ni ulimwenguni, wewe ambaye unatazamia kurudi huko, na kupumbuzwa na raha za kidunia.. fahamu kuwa huu ulimwengu umekwisha hukumiwa, na sasa hukumu yake imekaribia.

Hivyo ndugu usirudi duniani, usiwe kama mbwa aliyerudia matampshi yake.

2 Petro 2:20-22 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.

[21]Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.

[22]Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni”.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *