JIWE LILILO HAI

Biblia kwa kina No Comments

JIWE LILILO HAI

Jiwe lililo hai ni lipi?

Bwana Yesu asifiwe mtu wa Mungu. Karibu tujifunze biblia…Neno la Mungu wetu lililo Taa na Mwanga wa njia zetu (Zab 119:105)

Kwa kawaida hakuna jiwe lililo na uhai kwa asili yake … maana halina uhai ndani yake (non-living) ila lipo jiwe moja ambalo linatajwa katika biblia ambalo ni jiwe lililo hai tena ni jiwe teule, lenye heshima na thamani kubwa. Je! unalifahamu ni jiwe lipi hilo?

Tusome kitabu cha Petro wa kwanza..sura ya pili tutaliona.

1Petro2:3 ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili.

4 Mwendee yeye, JIWE LILILO HAI, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima.

YESU KRISTO ndiye jiwe lililo hai, ndiye Mfalme mwenye enzi yote, ndiye Mkuu wa wakuu wote na Bwana wa mabwana, anastahili sifa, heshima na utukufu.. Haleluya;

Ndiye jiwe walilokataa wajenzi lakini sasa limekuwa jiwe kuu la pembeni (Mathayo 21:42), na sio jiwe tu kama jiwe bali ni jiwe lililo hai, na lenye heshima na lililo gumu  kama mwamba, Yesu Kristo ndiye mwamba imara, Haleluya;

1Petro2:7 “….Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

8 Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha….”

1Wakorintho 10:4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.

Swali ni je! umelisimamisha hilo jiwe? au umelilalia?

Mwanzo 28:10 Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani.

11 Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.

12 Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.

13 Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako.

14 Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa.

15 Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.

16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.

17 Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.

18 Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, AKALITWAA  LILE JIWE ALILOLIWEKA CHINI YA KICHWA CHAKE, AKALISIMAMISHA KAMA NGUZO, na kumiminia mafuta juu yake.

Je! ni jiwe gani umeweka chini ya kichwa chako na kulalia kama mto?

Yamkini elimu yako ndiyo jiwe lako kwa sasa ambalo unalitegemea na ndiyo umeilalia kama foronya ili upate raha, au  ni biashara yako, au ni bosi wako, au ni ndugu na marafiki, au ni mume/mke wako ndiye anayekupa raha na umeweka matumaini yote kwake, nataka nikuambie hayo ni mawe yasiyo na uhai, jiwe ni moja tu lililo hai naye ni YESU KRISTO, ndiye lile jiwe ambalo Yakobo alilisimamisha, na Samweli pia akalisimamisha, na Daudi naye akalisimamisha, na Yoshua naye akalisimamisha, na wewe leo unapaswa kusimamisha jiwe hili, liwe nguzo kwako katika mambo yote,

1Samweli 7:11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari.

12 Ndipo Samweli AKATWAA JIWE, NA KULISIMAMISHA kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akasema, Hata sasa BWANA ametusaidia.

Yoshua 24:26 Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; KISHA AKATWAA JIWE KUBWA, AKALISIMAMISHA HUKO, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu  pa BWANA.

27 Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya BWANA aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu.”

Yawezekana kichwani mwako unamjua Kristo na yamkini unaenda kanisani kila week, na unamtolea Bwana, ila bado hofu za wachawi zinakunyima raha, bado hofu ya kifo inakutetemesha, hofu ya majini, n.k zinakuogopesha, usiku ukilala ndoto unazoziota ni kukimbizwa tu, na umehangaika huku na huku kwa manabii kutafuta msaada wa maombi, na umeombewa vya kutosha, umetumia mafuta ya upako, na maji, ila bado tatizo unalo?

Au yamkini  umesumbuka sana na huo ugojwa sugu na madakitari wameshindwa, au pengine umekuwa mtu wa hasira, wivu huwezi kujizuia, umeshindwa kuacha ulevi, wizi, uongo, usengenyaji, uasherati, kujichua, na mambo yote mabaya ambayo dhamiri yako inakushudia kuwa hayampendezi Mungu,

Yawezekana ni ndoa yako ina shida, au unatafuta mafanikio, au umekosa ada ya shule, au unakumbwa na kila aina ya matatizo na huoni msaada, nataka nikuambie huwezi kupona, na hayo mambo yote hayawezi kukuacha kwa kuishia tu kumjua yule Yesu unayemjua kichwani, yule Yesu wa jina tu, leo nataka nikuambie yupo Yesu ambaye ni jiwe lililo hai, gumu na lililo kuu ambalo ukilipata, basi tabu zote na shida zote zinakuacha, huzuni, hofu, magonjwa, ulevi, ujambazi, masturbation, tamaa zote za mwili zina kufa ama zinaondoka kabisa, yamkini unalo hilo jiwe na umelilalia chini ya kichwa chako lakini leo fanya maamuzi ya KULISIMAMISHA! ili upone.

Sasa jiwe hili utalisimamishaje?

Ni rahisi, Utalisimamisha kwa kuamua kutubu dhambi huku ukiwa umemaanisha kabisa kuziacha na kubatizwa kwa maji tele (Yohana 3:23), na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38), na kujazwa Roho Mtakatifu..hapo ndipo utakuwa umelisimamisha hilo jiwe; na wewe utafanyika kuwa jiwe lililo hai,

Je! upo tayari kulisimamisha hili jiwe? Kama jibu ni ndiyo, basi amua kuacha dhambi unazozifanya zote, amua kwa vitendo, choma mavazi yote yasiyo na adabu mbele za Mungu na kwa jamii, mfano wa hizo suruali, vimini, na nguo zinazochora maungo yako choma zote wala usimpe mtu mwingine! futa picha zote chafu kwenye simu yako, miziki za kidunia, amua kuacha mekaup, na vipodozi vyote, hizo hereni, wanja, lipustick, wigi, kucha bandia na vitu vyote bandia amua kuviteketeza zote bila kuangalia mtu, kumbuka hii sio dini mpya, wala sheria bali ni ukweli wa maandiko!

Ili uweze kulisimamisha hili jiwe huna budi kufanya hayo maamuzi magumu na utaona faida zake! Fahamu pia si kwamba utapona tu! au utafanikiwa tu! Ila pia utaepuka hukumu ya ziwa la moto; hivyo amua kuacha ukristo jina, amua kuacha uvugu uvugu.

Kuhudhuria ibadani, na kuhangaika kuwekewa mikono, kupewa mafuta ya upako, chumvi n.k huku hujasimamisha jiwe (yaani hujatubu), haikusaidii kitu! Na wala huwezi kupona, huwezi kushindana na shetani, utabaki tu kuwa mtumwa wa dhambi na mwisho utaenda jehanum.

Mpokee Bwana Yesu jiwe lililo hai ili nawe ufanyike jiwe kati ya mawe yaliyo hai, acha kutegemea na kulalia mawe yasiyo na uhai..havitakusaidia, ukristo wa kwenda kanisani na kurudi, haiwezi kukusaidia ni kujidanganya tu nafsi yako mwenyewe, elimu yako hata kama ikiwa kubwa kiasi gani bila kufanyika jiwe lililo hai, wewe sio kitu ni sawa tu na mawe yasiyo na uhai, vivyo hivyo na vitu vingine unavyovitegemea havitakusaidia maana ni mawe yasiyo na uhai, haviwezi kukupa uzima wa milele, ni Yesu Kristo tu ndio tumaini la maisha haya, na maisha baada ya hapa..Mwendee yeye jiwe lililo hai, Mwendee kwa kudhamiria kutubu, na kubatizwa ubatizo sahihi, na kuomba na kufunga, mwendee kwa kusoma Neno lake kwa bidii, hapo utakuwa umejengwa juu ya hilo jiwe kuu la pembeni, lenye heshima na thamani.. Yesu Kristo Mwokozi wa ulimwengu.

1Petro2: 3 ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili.

4 Mwendee yeye jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima.

5 Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *