Je! umeweka kweli nia kumtafuta Bwana.
Kama we ni msomaji wa biblia utafahamu kuwa kuna kipindi Israeli iligawanyika na kuwa na pande mbili yaani upande wa kaskazini ambako kulikuwepo na yale makabila 10 chini ya Yeroboamu na lile la Yuda na Benjamini ambalo lilikuwepo upande wa kusini chini ya Rehoboamu, leo hatutazungumzia kwa urefu kuhusu habari hiyo. Ila ukitaka kupata kwa urefu na kujua sababu zilizopelekea hayo makabila 12 ya Israeli kutengana soma 1Wafalme11-12,
Lakini sababu kubwa zilizopelekea Israeli kugawanyika, ni kukengeuka kwa Sulemani ambaye alikuwa ni mfalme wa Israeli. Mfalme Sulemani alipewa na Mungu ufalme kutoka kwa baba yake Daudi na mwanzoni alimpendeza Mungu sana na akapewa hekima kuzidi wafalme wote wa dunia pia alikuwa na utajiri mwingi sana kiasi kwamba mpaka sasa hajawahi kutokea tajiri kama Sulemani.
Ila baadaye Sulemani alikuja kukengeuka na kuacha sheria za Mungu, alikuja kuoa wanawake wa kimataifa ambao Mungu alikuwa amekataza watu wake wasichangamane nao kwani wangewageuza mioyo yao na kugeuka kuabudu miungu yao jambo linalomchukiza Mungu. Na ndicho kilichomkuta Sulemani baada ya kuoa wanawake wa kimataifa aligeuzwa moyo na akajikuta anaingiza miungu katika Israeli na kuabudu.
1Wafalme 11:1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa wasidoni, na wa Wahiti,
2 na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.
3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.
6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.
Sasa baada ya hapo, Mungu alimghadhibikia Sulemani na akaapa kumuondolea ufalme na kumpa mtumishi wake aliyeitwa Yeroboamu, lakini kwa ajili ya Daudi babaye ambaye alikuwa amempendeza Mungu, aliachiwa kabila moja tu ili nyumba ya Daudi isikose urithi sawa sawa na agano aliloingia Mungu na Daudi.
1Wafalme 11:9 Basi BWANA akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha BWANA, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,
10 akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru BWANA.
11 Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.
13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.
Sasa jambo hilo nilikuja kutokea mbeleni kama Bwana alivyonena, baada ya Sulemani kufa mwanawe Rehoboamu alitawala, na hapo ndipo makabila 12 ya Israeli yalitengana, makabila 10 yalimfuata Yereboamu (mtumishi wa Sulemani) na makabila mawili yalimfuata Rehoboamu mwana wa Sulemani, kwakuwa ndivyo BWANA alivyomwambia Sulemani kwa kosa lake na ni kwa ajili tu ya Daudi asingebakiziwa hata kabila moja.
Sasa kilichotokea baada ya Israeli kutengana.. Yeroboamu ambaye alikuwa na makabila 10 huko upande wa kaskazini, pamoja na kuona makosa yote aliyoyafanya Sulemani ya kuabudu miungu.. yeye naye alienda kufanya machukizo zaidi ya Sulemani kwani alitengeneza sanamu za ndama na kuamuru Israeli waabudu, tena alifanya na machukizo mengine mengi tu ikiwemo kuondoa mahukuhani walioteuliwa na Mungu wafukize uvumba, akaweka watu wengine mahali pa juu aliyoitengeneza na kuvukiza uvumba kinyume na sheria ya Mungu, pia akaamuru Israeli wasiende kumfanyia Mungu ibada kule Hekaluni bali waabudu katika madhabahu yake aliyoiweka mwenyewe. Na akafanya na machukizo mengi tu kuliko wafalme wote waliotangulia na waliomfuata baada yake.
1 Wafalme 14:5 BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine.
[6]Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito.
[7]Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli,
[8]nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu;
[9]lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako;
Lakini katika watu wake walitokea watu ambao walikuwa na mioyo ya kumpenda Mungu na wakajikaza nia kumtafuta BWANA, wakaenda kule Yerusalemu ambako kulikuwepo na nyumba ya Mungu, wakaenda kuungana na yale makabila mawili ya Yuda na Benjamini ambao wao walikuwa wakimwabudu Mungu kwa usahihi japo na wenyewe baadaye walikuja kunajisiwa na hizo miungu za kigeni.
Watu hao ni pamoja na hao makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote..waliacha malisho yao, na milki yao, wakaja Yuda na Yerusalemu ili kumwabudu Mungu wa kweli. Sasa biblia inasema watu hawa walijikaza nia kumtafuta BWANA.
Na somo letu leo linasema je! umeweka nia kumtafuta Mungu? Kama hao watu wachache waliokataa kuabudu masanamu, kumbuka waliacha malisho yao na milki zao. Kuonyesha kweli walikuwa wameweka nia ya kumtafuta BWANA.
Hebu tusome hiyo habari kwa umakini.
Mambo ya Nyakati 11:5 Naye Rehoboamu akakaa Yerusalemu, akajenga miji yenye ngome katika Yuda.
[6]Akajenga na Bethlehemu, na Etamu, na Tekoa,
[7]na Bethsuri, na Soko, na Adulamu,
[8]na Gathi, na Maresha, na Zifu,
[9]na Adoraimu, na Lakishi, na Azeka,
[10]na Sora, na Aiyaloni, na Hebroni, iliyoko katika Yuda na Benyamini, miji yenye maboma.
[11]Akazifanya imara hizo ngome, akaweka majemadari humo, na akiba ya vyakula, na mafuta, na mvinyo.
[12]Na ndani ya miji yote mmoja mmoja aliweka ngao na mikuki, akaifanya kuwa na nguvu nyingi mno. Yuda na Benyamini ikawa milki yake.
[13]Wakamwendea makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote, kutoka mpaka wao wote.
[14]KWANI WALAWI WAKAACHA MALISHO YAO, NA MILKI YAO, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwatupa, ili wasimfanyie BWANA ukuhani;
[15]naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa wale majini, na wa zile ndama alizozifanya.
[16]NA KUTOKA KATIKA KABILA ZOTE ZA ISRAELI, WAKAANDAMWA NA HAO WALIOJIKAZA NIA KUMTAFUTA BWANA, Mungu WA ISRAELI, WAKAJA YERUSALEMU, ILI WAMTOLEE DHABIHU BWANA, MUNGU WA BABA ZAO.
[17]Hivyo wakaufanya imara kwa miaka mitatu ufalme wa Yuda, na kumtia nguvu Rehoboamu mwana wa Sulemani; kwa maana muda wa miaka mitatu wakaiendea njia ya Daudi na Sulemani.
Swali :Je! umekaza nia kweli kumtafuta Bwana?
Maandiko yanasema mtafuteni BWANA maadamu anapatikana (Isaya 55:6)
Katika siku hizi za kumalizia, yaani siku za mwisho…hizi ni siku za kunga’ang’ana kumtafuta Mungu kwa kudhamiria kweli kweli, ikiwa unataka kuepukana na ghadhabu ya Mungu ambayo ipo karibu, sio wakati wa kutazama nyuma na kutamani raha za dunia kama mke wa Lutu, hizi ni siku za kuweka bidii, kuweka nia ya kweli kumtafuta Mungu wa kweli.
Huu sio wakati wa kuangalia ndugu, dhehebu, dini, shangazi, au mzazi wako anasemaje; sio wakati wa kujitumainia na wingi wa watu wanaopita katika njia ya upotevu, sio wakati wa kusema dhehebu letu liko hivi na hivi au mchungaji wetu amesema kusuka haina shida, kuvaa suruali, vimini na kujitia mekaup usoni haina shida maana Mungu anaangalia roho, na huku hujui Neno la Mungu, huu sio wakati wa kusikiliza mafundisho ya mashetani.
Kubali kutupwa nje na ulimwengu kwa ajili ya kumtafuta Mungu, ndivyo watu hawa walivyofanya.. soma tena hapo mstari wa 14 unasema..
14 “..KWANI WALAWI WAKAACHA MALISHO YAO, NA MILKI YAO, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwatupa, ili wasimfanyie BWANA ukuhani;
Umeona hapo, hata yule kipofu wa Siloamu alikubali kutupwa nje na ndipo akakutana na uso wa Bwana..
Yohana 9:35 Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?
[36]Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?
[37]Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.
[38]Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.
Watu wote ambao waliweka nia ya kweli kumtafuta Mungu hawakueleweka na ulimwengu, sasa kwanini wewe ueleweke? Ukiona bado ulimwengu unakupenda na wewe unaupenda fahahu kuwa bado hujaweka nia kumtafuta Bwana.
Waebrania 11:36 wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
[37]walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;
[38](watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.
[39]Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;
[40]kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Ukiokoka na ukaweka nia ya kweli kumtafuta Mungu, tarajia kutengwa na ulimwengu, kutengwa hata na ndugu wa karibu, kuachwa na marafiki, kufukuzwa kazi, kupitia dhiki nyingi, lakini upitiapo hali kama hiyo unapaswa ufurahi ukijua dhawabu yako ni kubwa mbinguni na ndiyo njia waliyopitia watakatifu wote.
Mathayo 5:11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
[12]Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
Anza kutafuta Mungu kwa bidii, usikubali kukosa mbingu kwa ajili ya mtu…anza kijikana nafsi yako na kuchukua msalaba wako mwenyewe na kumfuata Yesu kwa kudhamiria kabisa.
Maandiko yanasema..
2Wakorintho 8:12 Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.
Swali ni lile lile ndugu; Je! unayo nia kweli ya kumtafuta Mungu? Bwana alisema..
Luka 14:26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Kama bado hujaweka nia ya kumtafuta Mungu kweli kweli, basi anza leo, anza kutia bidii kutafuta utakatifu, anza kuweka bidii ya kuomba walau saa limoja kwa siku, anza kuweka bidii ya kusoma Neno na kusikiliza mafundisho, usisubiri tu mpaka jumapili ndio unafungua biblia, weka bidii katika kufunga na kukesha. Ukiweka bidii ya kumtafuta Mungu namna hiyo hakika Bwana atajidhirisha kwako na kukuonyesha mambo ya ajabu usiyoyajua.
Kumbuka tunaishi katika muda wa nyongeza.. muda tuliyobakiwa nayo ni kidogo sana.. Bwana Yesu yupo mlangoni.
Luka 13:24 Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;
26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulitufundisha katika njia zetu.
27 Naye atasema, Nawaambia Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.
28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.
Maran atha
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.