FANYENI MAMBO YOTE KWA UTUKUFU WA MUNGU.
Jina kuu la Yesu Kristo Mfalme Mkuu libarikiwe sana. Karibu tujifunze biblia.
Neno la Mungu linasema katika..
1Wakorintho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.
Biblia imetuagiza tufanye mambo yote kwa utukufu wa Mungu. Hii ikiwa na maana kuwa upo uwezekano tukafanya kwa utukufu wetu wenyewe au kwa utukufu wa wanadamu wenzetu jambo ambalo litamchukiza Mungu.. Ndio maana alituandikia hivyo mapema, kwamba neno lolote tulitendalo iwe ni kwa utukufu wake tu.
Kuvaa kwetu, kula kwetu, kuongea kwetu, n.k iwe ni kwa utukufu wa Mungu tofauti na hapo tutakuwa tunaabudu sanamu (mungu mwingine).
Ukivaa vazi lolote ili uonekane na watu.. unaabudu sanamu hata kama hujui, kwasababu umemvalia mtu badala ya Mungu wako aliyekuumba. Na ndio maana unavaa tu utakavyo au itakavyo dunia…na sio atakavyo Mungu.
1 Petro 3:3 Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na KUVALIA MAVAZI;
Wanawake wengi wanaojipamba kwa mapambo ya kidunia (mekaups, lipustiks, wanja, kucha bandia, nywele bandia, bangili, vipini, hereni n.k) na kuvaa vimini, na masuruali kama wanaume, wengi wao sio kwamba wanavaa ili wajiuze au watamaniwe.. wengine wana nia hiyo, Lakini wengi ni kwasababu wanataka tu nao waonekane kuwa wanaenda na wakati, wanataka wasifiwe na watu kuwa wapo vizuri..ndio furaha yao.
Wanafahamu kabisa kuwa hayo mapambo na mavazi ya kidunia hayampendezi Mungu, lakini kwasababu wanatafuta utukufu kwa wanadamu wanakusudia kufanya hivyo, wanamkana yeye aliyewafia msalabani.
Yohana 12:42-43 Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.
[43] KWA MAANA WALIPENDA UTUKUFU WA WANADAMU KULIKO UTUKUFU WA MUNGU.
Vijana wengi hawataki kuacha uhuni na udunia kwasababu wanaogopa kutengwa na vijana wenzao, wengine wanakataa wokovu wa kweli kwasababu hiyo hiyo ya kuogopa kutengwa aidha na ndugu, au marafiki. (Wamependa utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu).
Mabinti wengi na wanawake hawataki kuvaa sketi ndefu na magauni marefu yanayostiri miili yao kwasababu wanaogopa kuitwa washamba, na wakizamani, utakuta ni binti anasema sitaki kuitwa bibi, Kwahiyo acha niendelee kuvaa hizi vimini ndio nitaonekana. (Sababu ni hiyo hiyo wanatafuta utukufu kwa wanadamu)
Na sio tu uvaaji, biblia inasema ”neno lolote ” tufanye kwa utukufu wa Mungu.
Hivyo hebu anza kujitadhimini ndugu, je! biashara/kazi unayofanya ni kwa utukufu wa nani? Elimu unayotafuta ni kwa utukufu wa nani?
Leo hii unafunga na kuomba Bwana akupe gari, au nyumba, au mke/mume mambo ambayo ni mazuri kuwanavyo, lakini je ni kwa utukufu wa nani?
Na halikadhalika angalia ni kitu gani unaingiza kwenye mwili wako? Je kweli hiyo pombe unayokunywa ni kwa utukufu wa Mungu? Je hayo madawa ya kulevya unayotumia ni mapenzi ya Mungu kweli?
We dada, hizo rangi unazopaka mdomoni, kwenye kucha, na hayo masikio ambayo umetoboa..je unafanya hayo kwa ajili ya nani? Je ndivyo kweli Mungu alivyokusudia tangu mwanzo?
Hebu leo, amua kujikana nafsi yako mwenyewe na kuchukua msalaba wako na kumfuata Yesu ili uokoke na hukumu ya ziwa la moto.
Ni heri uonekane mshamba, asiye na akili, na ndugu wakutenge kuliko kusifiwa na wanadamu na kuonekana wa kisasa na huku unaenda kutupwa motoni. Itakufaidia nini?
Marko 8:34-36 Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
[35]Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.
[36]Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
Tafuta utakatifu kwa bidii (utakatifu ndio utukufu wa Mungu).
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.