Ufunuo 14:13
[13]Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; KWA KUWA MATENDO YAO YAFUATANA NAO.
Nakusalimu katika jina tukufu la Bwana Yesu Kristo Mwokozi wa ulimwengu.
Hivi umewahi kujiuliza mtu akifa Nini kitamtokea huko aendako?
Kama hukuwahi kulijua hilo, basi leo ni vema utafakari sana maana kama tunavyojua kifo hakiepukiki..tupende tusipende, kuna siku tu kifo kitatukuta, bila kujalisha umri au mazingira tutakayokuwepo kwa wakati huo, na hatari ni pale ambapo kinakuja bila kutarajia ..saa na siku tusiyojua, ni muda wowote lolote linaweza kutokea,
sasa leo hatutatazama zaidi kuhusu habari ya kifo..ila ninachotaka ufahamu ni juu ya hatima ya mwanadamu baada ya kufa, Nini kinamtokea huko aendako?
Biblia imeweka wazi kuwa baada ya kifo ni hukumu, tunalithibitisha hili katika kitabu cha waraka kwa Waebrania 9:27, Neno la Mungu linasema..
Waebrania 9:27 ”Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa ni hukumu;
Umeona hapo! baada ya kufa ni hukumu, huo ndio ukweli, ukisikia elimu nyingine inayosema hakuna hukumu na mtu akifa anakua amepotea..huo ni uongo unaotoka kwa yule mwovu, ukifa leo au siku zinazokuja, fahamu kabisa kuwa utakutana na hukumu ya Mungu ndivyo Neno la Mungu linavyosema.,
Sasa hiyo hukumu itakuwaje?
Maandiko yanasema Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa MATENDO YAO YAFUATANA NAO. (Ufunuo 14:13)
Kinyume chake cha hilo andiko linaweza ikawa hivi “Ole wao wafu wafao katika dhambi, kwakuwa matendo yao yafuatana nao.”
Umeelewa hapo! Maana yake mtu akifa kinachomfuata ni matendo yake, na hayo ndiyo yatakayoenda kuhukumiwanayo huko aendako. Ana heri kama matendo yake ni mema maana atapata hukumu ya kupumzishwa vizuri, ila ni Ole wake ikiwa matendo yake ni mabaya maana hukumu yake itakuwa ni jehanum ya moto ambapo huko hakuna kupumzika bali kuna mateso yasiyoelezeka.
Ndio maana biblia inasema..
Zaburi 49:16 Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
17 Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka UKIMFUATA.
Umeona hapo…mtu anapokufa, utajiri wake, fahari yake, umaarufu wake, n.k, havitamfuata bali ni MATENDO yake ndiyo yatakayomfuata sawa sawa na Ufunuo14:13,
Hivyo kuanzia leo mimi na wewe tunajukumu la kuhakikishia matendo yetu yanampendeza Mungu, tuhakikishe tunamzalia Mungu matendo(matunda) mema ili tukiondoka hapa duniani tukapate pumziko la amani,
Na matendo mema ni yapi ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:22 na yanayofanana na hayo ambayo kwa pamoja yanatengeneza utakatifu.
Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo hayo hakuna sheria.
Sasa hayo ndiyo matendo mema yanayompendeza Mungu ambayo kila mtu anatakiwa awenayo, na haya hayaji kwa jitihada zetu wenyewe bali kwa Roho wa Mungu, Roho Mtakatifu, na tunampokea Roho Mtakatifu kwa kutubu na kubatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi, baada ya hapo ataanza kwenye matendo mema yanampendeza Mungu..
Shalom, Mpokee Yesu Kristo leo..
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.