Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.

Dhambi No Comments

 

Shalom, ni kwa Neema za Bwana tuyatafakari Maneno yake ya uzima…

Leo natamani tujifunze kitu kingine pengine unakifahamu lakini naamini utaongeza maarifa zaidi,

Wengi wetu hasa watu wa Mungu wamekuwa wakiogopa kitu kinachoitwa dhambi, jambo ambalo ni jema sana tena linalompendeza Mungu, kwasababu hata Neno lake linatutaka tukae mbali na dhambi,kwa kuwa ni machukizo kwa Mungu Wetu,

Lakini nataka tusome hili andiko kuna kitu kipya tutajifunza…

Yohana 8:34

[34]Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni MTUMWA wa dhambi..

Ulishawahi kutafakari hilo neno mtumwa” mtumwa maana yake ni mtu/ kitu, aliye chini ya mamlaka fulani anayeongozwa na kutumikishwa kwa shuruti,

Katika agano la kale sana sana ndio inaelezea habari za watumwa, jinsi kazi zao zilivyokuwa na upatikanaji wao ulivyokuwa, ila kwa ufupi kazi yao kubwa ilikuwa ni kutumika kwa bwana zao, wakifanya kazi zote na walipatikana kwa fedha maana yake walikuwa wanauzwa kama bidhaa,mwisho wa siku ukimnunua anakuwa kama ni milki yako, watu wakubwa wa kipindi hicho walikuwa na watumwa, Ibrahimu,Ayubu, wafalme..

Utakumbuka pia hata kipindi cha wana wa Israeli kabla hawajatolewa Katika nchi ya misri walifanyika watumwa iwe walipenda au hawakupenda , walitumikishwa kwa kazi nyingi na mapigo kila siku yalikuwa yanaongezeka mpaka kupelekea huruma za Mungu kushuka ili kuwakomboa, ila ulikuwa ni utumwa mzito ulisiozoeleka, walifanyishwa kazi kwa nguvu,kwa kupigwa, kwa uonevu na mateso makali kwa miaka mingi sana,

Kutoka 3:7

[7]BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;

Kutoka 5:5-11,14,19

[5]Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao.

[6]Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema,

[7]Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe.

[8]Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.

[9]Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo.

[10]Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani.

[11]Enendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.

[14]Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza?

[19]Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wa katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza hesabu ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku.

Umeona utumwa jinsi ulivyo mbaya, sasa na maandiko yanasema kila atendaye dhambi ni MTUMWA, Yani unapofanya dhambi, shida sio dhambi uliyoifanya,tatizo kubwa linakuja pale ambapo tayari umeshakuwa mtumwa wa hiyo dhambi,maana yake tayari umeshakubali kuwa chini ya hiyo dhambi,yani dhambi imeshakununua na itaanza kukutumikisha na kukupeleka kama inavyotaka yenyewe..hili ni jambo la kuogopa sana..

Leo utashangaa vijana wengi ni wazinzi au wanafanya mambo ya kizinzi na wanasema wameokoka, shida haipo kwenye uzinzi wanaoufanya, shida kubwa ipo kwenye utumwa waliojiuza pale walipoanza kufanya mambo ya kizinzi, na hapo hapo dhambi ya kizinzi ikapata nguvu ya kuwapelekesha na kuwatumikisha, utafika muda utatamani utoke, lakini baada ya siku mbili unarudia tena,

utajifanya umegeuka kama Daudi lakini baada ya kipindi kifupi mnajikuta mnarudia tena uovu, hapo fahamu tayari hiyo dhambi imeshaanza kupata nguvu ya kuwatumikisha, unajishangaa mbona huoni tamaa ndani yako, lakini unajikuta unataka kufanya jambo fulani la kizinzi, hapo tayari hiyo dhambi imeshaanza kupata nguvu nayo inataka kukutumikisha..

Na sio dhambi hiyo tu,ni dhambi zote, huwa haziji tu ndani ya mtu, huwa zipogo kila mahali lakini zinatafuta upenyo fulani ndani ya mtu, na usipokuwa makini utajikuta unakuwa mtumwa wa dhambi siku zote,na zitakutumikisha Mpaka zipate faida iliyokuwa inataka, ndo mana maandiko yanasema..

Warumi 6:23

[23]Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Umeona, mwisho wa utumwa wa dhambi ni kifo, dhambi inakutumikisha Mpaka ihakikishe umekufa katika hiyo dhambi,au umepotea kabisa,

Ndugu yangu,kaa mbali na utumwa wa dhambi,ni mbaya kuliko dhambi yenyewe, utumwa wa dhambi unakufanya sehemu yako iwe ni kwenye ziwa la moto, kwasababu yenyewe haina huruma, jiweke mbali na vichochezi vyote vya dhambi, jiepushe na utumwa wa dhambi, unaanza kidogo kidogo lakini unavyozidi kutenda ndivyo inaongeza nguvu ya kukutumikisha,ukishaingia kwenye huu utumwa jua si kazi rahisi kujinasua kwa nguvu zako mwenyewe, jitenge hata na watu unaowaona wana namna hiyo,itakusaidia..

Kuwa msomaji wa maandiko sana, mtu wa maombi na ibada,na kuwashuhudia wengine na kujibidiisha Katika Bwana,utaifunga Milango ya utumwa wa dhambi, lakini fahamu ikiwa ujaokoka huwezi kutoka kwenye utumwa huo, kwasababu hata wana wa Israeli walishindwa kutoka kwa farao mpaka Mungu aliposhuka kuwakomboa,

Na sisi tunaye YESU KRISTO Mwokozi wetu anayetuokoa na huu utumwa, mkabidhi maisha yako kwa kutubu na kubatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi,na upokee Roho Mtakatifu sawa sawa na maandiko ili uwe huru na utumwa wa dhambi, na kama umeokoka fahamu bado unahitaji Neema ya Mungu kukuwezesha usijikwae tena na kurudi kwenye utumwa huu..

1 Wakorintho 7:23

[23]Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu.

Shalom..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *