Mbinu tatu anazozitumia Shetani kumuangusha Mkristo

Biblia kwa kina No Comments

Nakusalimu katika jina la mwokoziwetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi wetu Yesu Kristo.

Tulijifunza hapo nyuma kidogo juu ya somo linalosema ”fahamu utendaji kazi wa shetani katika kuwaangusha watoto wa Mungu” kama hukufanikiwa kulisoma nakushauri ulipitie hata kama utakuwa umeshalisoma lipitie tena litakuongezea kitu kikubwa.

Katika somo hili la leo tutakwenda kuangalia mbinu kuu tatu ambazo shetani anatumia kumuangusha adui yake ambaye ni Mkristo wa kweli kabisa. Mbinu hizi anazitumia ili kuiba roho yako kisha kuipeleka kuzimu.

Lakini pia tutajifunza ni kwa namna gani utaweza kupambana nae na kumshinda kabisa wala asikuweze. Ni muhimu sana Mkristo kwa wewe kuyafahamu haya kwa undani yatakusaidia kumpinga shetani na hila zake na utabaki kuwa salama kabisa.

Kuna msemo mmoja unasema “kama ukishindwa kupanga; umepanga kushindwa” hili ni jambo la mwilini kabisa vivyo hivyo na Rohoni pia iko hivyo. Maisha ya mwilini ni kivuli au uhalisia wa mambo ya rohoni.

Nasema hivi kwa sababu anatumia mikakati na mbinu zile zile toka kuumbwa kwa ulimwengu huu ili kuwaangusha wanadamu.kifupi shetani hana mbinu mpya zile zile alizozitumia zamani ndio hizo hizo anazitumia hata sasa. Maandiko yanatupa tahadhari dhidi ya adui yetu huyu mkubwa katika kitabu cha..

1 Petro 5:8-9 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.

9 Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.

10 Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo,mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatianguvu.

hili ni onyo la kweli, je tunajua mikakati halisi ambayo shetani hutumia kutuharibu? kama tungelikuwa tunajua tungeweza kuepuka mitego yake, na kuendelea mbele kukua kiroho badala ya kutumia muda mwingi kuzijenga nafsi zetu ambazo kila siku anatuvuruga.

Katika mistari hiyo utaona maandiko yanasema “mwe na kiasi na kukesha..” mana yake ni jambo ambalo linatakiwa kuwa endelevu.. lakini anaendelea kusema.. “mshitaki wenu kama simba angurumaye akitafuta mtu ammeze..” maana yake pia kazi ya Shetani ni endelevu hachoki wala hakati tamaa ni kitu anachokifanya kila siku.!

MBINU ANAZOZITUMIA SHETANI

1. Mbinu ya kwanza ni uongo.

Bwana Yesu alimuita shetani ni baba wa uongo maana alikuwa muongo tokea hapo mwanzo hata akawadanganya malaika wengi wakaasi na ndio anaewadanganya wanadamu na kuwashambulia toka mwanzo (Yohana 8:44).

Turudi katika mazungumzo kati yake yeye na Hawa pale Edeni ndio yanayothihirisha na kutupa ufahamu mpana zaidi. hata  sasa uongo huo huo anautumia hata sasa. Na uongo wa namna hiyo anaoutumia ni huu..

mazuri ni mabaya na mabaya ni mazuri.

kazi kubwa anayofanya hapa Shetani ni kutaka kubadilisha na kukuaminisha kuwa mabaya ndio mazuri kama alivyomdanganya Hawa?

mwanzo 3:1 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?”

unaona hapo? kama ukisoma kwa makini anaanza kwa kumuuliza ubaya wa hilo tendo likifanyika ni nini kitatokea? hapa anaanza kwa kuweka mashaka akilini mwake kana kwamba hakuelewa vyema juu ya hicho alichowaambia Mungu kwa kutoa mapendekezo yake kuwa huenda Hawa hakuelewa vizuri  na kwama haikuwa dhambi kweli kwa yeye kufanya kitendo kile. na anamuaminisha kuwa jambo hilo linawezekana na wala si dhambi ni jambo la kawaida tu.

Shetani anatabia ya kubadilisha dhambi ziliozokuwa dhambi awali na kufanya kuonekana kama mambo yanayokubalika kabisa.

kama uvaaji suruali kwa wanawake, kuweka mapambo na kuvaa mawigi nk ni vitu ambavyo shetani kafanikiwa kuvifanya vionekane ni vitu vinavyokubalika kabisa.

lakini kumbe ni dhambi hapo utasikia anakwambia “yaani usiende mbinguni kisa kuvaa hereni,kuweka nywele bandia,kuvaa suruali au kunyoa kiduku haiwezekani…nk”

ndugu unaesoma ujumbe huu geuka shetani kashakudanganya na kakuaminisha kama Hawa. Maana ni tabia yake kuifanya dhambi ionekane ni kitu cha kawaida tu.

uzinzi(kuishi bila kufunga ndoa)

kitendo hiki badala ya kukiita dhambi kinaonekana kama ni haki ya mtu binafsi au chaguo la maisha.

mahusiano ya jinsia moja(ushoga).

leo hii Shetani kawadanganya watu kuona kuwa ni haki kwa mtu kufanya hivyo na anazidi kabisa kuwafanya kuona ni haki ya kijamii na wanatambuliwa bila kukemewa na wanapewa haki zao jambo ambalo ni kinyume kabisa. Na imeenda mbali hata baadhi ya makanisa yana halalisha ndoa hizo.

mauwaji(utowaji wa mimba)

kitendo hiki badala kiitwe uwaaji na ukatili. kwa sasa kinaonekana kama haki ya mwanamke ya kuamua kuhusu mimba, kinaonekana kama njia ya kudhibiti uzazi na kumudu gharama za kuishi.kinaonekana kitendo cha kawaida na hata nchi hazikemei kabisa tendo kama hili linaonekana la kawaida na si la ajabu badala ya kuitwa mauwaji ya watoto(yanaitwa kutoa mimba).

upo uongo mwingi sana shetani anatumia kuwaangusha watu.

2.Dhambi haina matokeo.

Huu ni uongo ambao alimdanganya Hawa pale Edeni, akamwambia….

Mwanzo 3:4” Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,”

Unaona hapo? Anamwambia hata ukila hautakufa  yaani ataendelea kuishi anaibatilisha kauli ya Mungu amabyo alimwambia Adamu kuwa hakika siku watakayokula watakufa.(mwanzo 2:17).

Ni uongo anaoendelea kuutumia hata leo hii kwa kukudanganya kuwa hata ukizini,ukiiba,ukitukana,ukisema uongo nk hakuna shida yoyote ile Mungu anaelewa wewe ni mwanadamu.lakini ni kitu ambacho ni uongo na tunafahamu hata katika maisha ya kawaida kuwa

Kila tendo lina matokeo.

Kila chaguo tunalolifanya huanzisha mchakato ambao utatuathiri kwa namna moja au nyingine yaani utakua na matokeo hasi au chanya.

Maana yake ni kwamba katika kila jambo la kimwili au la rohoni linakuwa na matokeo kwetu

3. Mungu yuko kinyume na wewe.

Hiki ndio kitu moja wapo kikubwa kilichomshawishi Hawa. Shetani alimdanganya kuwa Mungu hataki uwe kama yeye ndio maana alizuia msile hilo tunda. Alizidi kumdanganya na Hawa akaona kumbe Mungu hataki nifurahie vitu vizuri anataka niendelee kukaa hivi hivi tu.

Mwanzo 3:5” kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho,nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

Hapa shetani anachojaribu kufanya uone maamuzi yako na matanio yako ni bora zaidi kuliko ya Mungu. Uone njia zako ni sawa hazina makosa yoyote lakini sivyo.

Uone Mungu anaposema usizini,usinywe pombe, usivute sigara,usichole tattoo,usiweke nywele za bandia kucha nk. Anachotaka uone kuwa Mungu anakuonea wivu.. lakini sivyo ni kwa faida yako.

2.Mbinu ya pili: kukutenga.

Shetani akitaka kukuangusha ni lazima kwanza atafute namna ya kukutenga ikiwa umezungukwa na wapendwa wenzako katika Kristo iwe ni kanisani ama iwe katika kikundi cha maombi. Hii ni mbinu wanayotumia hata wanyama kama simba pale wanapotaka kukamata nyumbu au swala huangalia mnyama yupi ni dhaifu kisha wanamuwekea mikakati namna watakavyotokea na kumfukuza ili wamtenge mbali na kundi.(huwa hawakurupuki tu wanaanza kukimbiza yoyote yule hapana).

Jambo hili lilitokea kwa Daudi baada ya wenzake wote kwenda vitani yeye akabaki mwenyewe na katika kutembea kwake kule akamuona Bethsheba akamtamani akazini nae(2 Samweli 11:1-5).

Na kujitenga kupo kwa aina tofauti tofauti..

kuwa busy na kazi kuliko Mungu.(jumapili kwa jumapili kanisani na uko busy huna muda wa maombi na kusoma neno)

Kutokuelewana na wenzako katika jambo Fulani na kuamua kujitenga.

Kuumizwa,upweke,udhaifu/madonjwa, nk

Kujitenga sio dhambi lakini ni ishara kuwa shetani ni rahisi kukunasa maana ukiwa mwenyewe ni rahisi sana kuanguka katika dhambi,

3.mbinu ya tatu: Tamaa yako(Msisimko)

Katika tamaa uliyonayo ndio udhaifu pia Shetani anautumia kukunasa. Kama vile mke wa Lutu tamaa yake ilikuwa ni kubaki Sodoma japokuwa alikuwa ameshaokolewa kabisa lakini Shetani alijua udhaifu wake huyu anatamani kurudi kule na akafanikiwa sana kumshawishi katika fahamu zake atazame kuna nini na likawa kosa akawa nguzo ya chumvi.

Katika mambo unayoyawaza sana akilini mwako shetani anayatumia hayo hayo kukuangusha.

Vivyo hivyo hata Dema alikuwa anazidi kukua katika imani na katika huduma akitembea na Paulo lakini alikuwa pia anatamani mambo ya uliwengu huu mwisho akamuacha Paulo akaenda kujifurahisha katika tamaa za ulimwengu huu za kitambo tu.(2 Timotheo 4:10).

NAMNA YA KUMSHINDA ADUI.

1.Mjue adui yako.

Huwezi kushinda vita ikiwa humjui adaui yako ni nani na hapa ni muhimu kufahamu kuwa adui yetu kama wakristo si mwanadamu bali ni falme za giza katika ulimwengu wa Roho Mtume Paulo kaliweka wazi jambo hilo. Soma Waefeso 6:12. Usipotee muda kuanza kumuombea mtu unaeona ni adui yako apatwe na shida unajichosha ndugu. Mjue adui yako na anataka nini na ni kwa namna gani anakuwinda?

2.fahamu ni lazima utashinda.

Ni jambo la muhimu kabisa ufahamu katika majaribu yote jua ni lazima utashida. Shetani kitu anachokuambia kuwa huwezi kushinda kamwe. Watu wengi wanamuamini shetani na wanaona hawawezi na wanaanza kusema “siwezi,nimeshachelewa,mimi ni dhaifu, nk’ ndugu tambua unaweza maana Yesu Kristo ndio akutiae nguvu alieshinda HALELUYA…

Maandiko yanasema 1 wakorintho 10:13 kuwa hakuna jaribu linalotupata lililo nje ya uwezo wetu.

Ukijua habisa sisi sio watu wa kwanza ambao tunapambana na majaribu wako ambao walishapambana na wakashinda kwa msaada wa Kristo.

Mungu anafahamu kiwango cha uvumilivu wetu na hivyo hawezi ruhusu tukajaribiwa kupita kiwango cha uvumilivu wetu haiwezekani.

Mungu mwenyewe atatengeneza njia ya kutokea katika jaribu hilo.. kwa nini ukate tamaa na useme huwezi.

3.jua namna ya kupigana.

Mtume Petro ambae anajua namna mtu anaweza kushinda vita ama kushindwa dhidi ya shetani anatuonyesha namna ya kukabiliana nae kikamilifu na kumuangusha.

Tofauti na watu wengi wanaingia kuomba maombi ya vita wanaanza kukemea tu naagusha ngome zote bila kujua ngome zipi unatakiwa kuziangusha?

1.Jinyenyekeze mbele za Mungu.(1 Petro 5:6-11)

Tunatakiwa kuwafahumu kuwa sisi ni rahisi kudanganywa na kujaribiwa na tunahitaji msaada wa Mungu kila siku na rehema zake katika vita vyetu dhidi ya shetani na dhambi.. moja ya njia ya kujinyeyekza mbele za Mungu ni katika kuomba,kusoma neno,kufunga nk. Unapofanya haya unaonesha unahitaji msaada wa Mungu.

2.Kuwa macho muda wote.

Si kwamba usilale usingizi la!, bali kuwa mtu wa kukesha katika roho kwa kuomba,kufunga na kujiweka mbali na dhambi.

Tunaanguka katika dhambi kwa sababu hatujali,hatusikilizi, na tunakuwa busy sana na ulimwengu jambo linalofanya tukose nguvu katika roho na uelewa mzuri. Ni lazima tuwe imara na tayari.

3.Simama imara.

Usikubali kuyumbishwa yumbishwa simama na neno la kristo wakati wote na majira yote huku ukizidi kuongeza juhudi katika mambo ya rohoni.

Tegemea kupokea taji baada ya yote hayo.

Jua kabisa kuwa kuna taji mbele imewekwa baada ya kuyastahimili yote hayo.kumbuka anaekupa taji hiyo sio mwanadamu au kiumbe chochote kile si malaika wala nani bali ni Mungu mwenyewe. Amabae atakukamilisha na kukufanya ufanane na Kristo

Hivyo kila siku ukatae ubaya na zidi kusonga mbele ukitarajia Taji iliyoko mbele yako isiyoharibika kaza mwendo kila siku ukijua bado sijafika na muda si mrefu jua kabisa unakaribia kufika.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *